Thursday 20 October 2016

POLISI WAUA MAJAMBAZI SITA DAR


MAJAMBAZI sita wameuawa jijini Dar es Salaam, kwenye majibizano ya risasi kati yao na Kikosi Maalum cha Polisi, wakati yakijaribu kufanya uporaji.

Imedaiwa kuwa, majambazi hayo yalipanga kufanya uporaji wa fedha kutoka kwa mfanyabiashara, aliyekuwa akitoka kuchukua fedha kwenye Benki ya Diamond Trust (DTB), Tawi la Barabara ya Nyerere, akienda mkoani Morogoro.

Aidha, jeshi hilo limefanikiwa kukamata miundombinu inayotumika kuunganishia umeme ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 61.

Mkuu wa Operesheni wa kanda hiyo, Kaimu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya, alisema baada ya polisi kupata taarifa ya kuwepo kwa majambazi hao, waliweka mtego kuwakabili.

Mkondya alisema majambazi hao walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota Carina, lenye namba za usajili T. 970 DGZ, ambapo walionekana kulifukuzia gari la mfanyabiashara huyo kisha kulipita na kulizuia kwa nguvu mbele.

“Majambazi wawili wakiwa na bastola walishuka kwenye gari hilo, lakini baada ya kugundua kuwa wameingia kwenye mtego wa polisi, walianza kufyatua risasi kwa polisi," alisema Mkondya.

Aliongeza: “Wenzao waliokuwa kwenye gari, walitoka huku wakifyatua risasi hovyo kuelekea kwa askari, ambapo askari walilazimika kujibu mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi hao.”

Mkondya aliongeza kuwa baada ya kuwapekua, walipata bastola mbili, moja ikiwa ya kijeshi aina ya Chinese, iliyokuwa na risasi moja, maganda sita ya risasi yaliyookotwa kwenye eneo la tukio na bastola nyingine aina ya Browing, iliyokuwa imefutwa namba.

Miili ya majambazi hayo imehifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku upelelezi wa kubaini mtandao wao ukiendelea.

Katika tukio lingine, wananchi wenye hasira kali walimuua jambazi aliyekuwa akijaribu kufanya uporaji kwa kutumia pikipiki.

Naibu Kamishna Mkondya alisema jana kuwa, jambazi hilo lilikuwa na wenzake wawili, wakati wakifanya uporaji kwenye duka la Abdallah Juma, eneo la Tegeta Masaiti.

Alisema baada ya wananachi kutoa taarifa kuhusu tukio hilo, polisi waliwafukuza majambazi hao, ambao walilazimika kutupa begi lililokuwa na silaha kisha kutelekeza pikipiki waliyokuwa wakiitumia yenye namba za usajili MC 370 BEY.

Hata hivyo, wananchi walifanikiwa kumkamata na kumuua jambazi mmoja huku wengine wakitoweka kusikojulikana.

MIUNDOMBINU YA TANESCO 

Polisi pia wamefanikiwa kukamata vifaa vinavyotumika kuunganishia umeme, mali ya TANESCO, vyenye thamani zaidi ya sh. milioni 61.

Vifaa hivyo, vikiwemo nyaya za kuunganishia umeme, vilikamatwa maeneo ya Salasala, baada ya kufanyika upekuzi kwenye nyumba zinazomilikiwa na Betrice Emannuel na Wilfred Baruti, wakazi wa Makumbusho.

Aidha, polisi kupitia kikosi chake cha usalama barabarani, kimekusanya zaidi ya sh. milioni 400, ikiwa ni fedha zitokanazo na faini za makosa ya usalama barabarani katika kipindi cha siku nne.

Idadi ya magari yaliyokamatwa ni 9,817 na pikipiki 708, kwa makosa 10,525.

No comments:

Post a Comment