Thursday 20 October 2016

SERIKALI YAHAKIKI DENI LA BILIONI 26 LA WALIMU

SERIKALI ipo kwenye hatua za mwisho za uhakiki wa madeni ya walimu yanayofikia sh. bilioni 26, ambazo zitalipwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2016/2017.

Malipo hayo ni mwendelezo wa kupunguza madeni ya watumishi hao, ambayo serikali imekuwa ikiyalipa kwa takriban miaka minne mfululizo, tangu 2011, yanayofikia sh. bilioni 61.1.

Kauli hiyo ilitolewa mjini Dodoma, jana na Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jaffo, alipokuwa akifafanua suala hilo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Jaffo alisema serikali haiwezi kumaliza kabisa madeni ya walimu kutokana na uhalisia kwamba, kila siku yanaibuka madeni mapya yanayotokana na malipo ya lazima ya likizo kwa watumishi hao.

Alisema licha ya kuyalipa madeni hayo, iko kwenye mkakati wa kuzuia matumizi yasiyo ya lazima, ambapo tayari serikali imewapiga marufuku wakurugenzi wa halmashauri nchini, kutokutoa uhamisho kwa walimu endapo hakuna fedha za kuwalipa.

"Deni la walimu ni endelevu, serikali inajitahidi kupunguza kadri fedha zitakapopatikana kutokana na kwamba, tunajua umuhimu wao.

"Lakini ili kupunguza ukubwa wa madeni, tumeshasema ni marufuku mkurugenzi kutoa uhamisho wa mwalimu kama halmashauri haina fedha ya kuugharamia," alisema.

Aidha, alisema ni ukweli usiopingika kuwa, kuna udanganyifu mkubwa kwenye madeni ya walimu, jambo lililoilazimu serikali kuyahakiki kabla ya malipo.

"Niliwahi kuona deni la mwalimu fulani kuwa ni shilingi milioni 60, lakini alipohakikiwa, kumbe anaidai serikali sh. milioni sita tu," alisema.

Kwa upande wao, wajumbe wa kamati hiyo, akiwemo Waziri mstaafu wa fedha, Saada Mkuya, aliunga mkono hatua ya serikali kuhakiki madeni ya walimu kabla ya kuwalipa.

Alisema ana ushuhuda kuhusu udanganyifu wa madeni ya watumishi wa kada mbalimbali, ikiwemo ualimu wakati akiwa waziri kwenye serikali ya awamu ya nne.

Kikao hicho cha kamati kilidhuriwa na baadhi ya watumishi wa Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC), ambapo kamati ilibaini mapungufu mengi kwenye sheria iliyotumika kuunda tume hiyo.

Magreth Sitta, aliihoji tume hiyo juu ya vigezo wanavyotumia kupandisha madaraja ya walimu kutokana na uwepo wa malalamiko mengi.

Alisema walimu wamekuwa wakilalamika kwa njia mbalimbali, ikiwemo kupitia chama chao, ambapo wengi wanadai kutopandishwa madaraja licha ya kuwa na vigezo.

Tume hiyo ilisema kisheria wana vigezo vitano, ambavyo ni utendaji kazi wa mtumishi, nafasi yake kazini, miundo ya kiutumishi, uwepo wa fungu kwenye bajeti na ikama, ambayo hutolewa na mkurugenzi wa halmashauri ya mtumishi husika.

Aidha, watumishi wa tume hiyo walikiri kuwepo kwa mapungufu kwenye sheria, ambayo imetoa dhamana kuanzishwa kwa TSC, hivyo kuwataka wabunge kuangalia namna ya kuifanyia marekebisho.

Venance Mwamoto, akichangia ombi hilo, aliishauri serikali kutoa kibali kwa wajumbe wa kamati yao ili waende kujifunza namna tume kama hiyo inavyofanya kazi kwenye nchi jirani, ikiwemo Kenya.

"Ifike wakati turuhusiwe kutoka kwenda kuona wenzetu wanafanyaje.
Tume kama hii ni muhimu, haina matatizo kama ilivyo kwetu, kwa sababu sheria tumeipitisha wenyewe wabunge, lakini awali tu matatizo yanaanza kuonekana," alisema.

Baadhi ya mkanganyiko uliobainika na wajumbe wa kamati hiyo kuhusu TSC, ni kuhusu mwenye mamlaka ya kupandisha cheo mtumishi, endapo ni mkurugenzi wa halmashauri au TSC wenyewe.

Pamoja na hayo, wajumbe wa kamati walihoji kuhusu ruhusa ya walimu kwenda kujiendeleza kimasomo, ambapo halmashauri hukataa kutoa ruhusa kutokana na ufinyu wa bajeti.

"Ni kwanini mwalimu hunyimwa ruhusa kwenda kujiendeleza kwa kisingizio cha bajeti katika halmashauri?" Alihoji George Lubeleje.

Kuhusu swali hilo, Waziri Jaffo alisema tayari serikali imeziagiza halmashauri kutenga fedha kwenye mwaka husika wa bajeti kwa ajili ya walimu kwenda kujiendeleza.

Kwa mujibu wa Jaffo, shule za serikali zina jumla ya walimu takriban 299,000, ambapo kati yao, 85,000 ni wa shule za sekondari.

No comments:

Post a Comment