Friday, 10 June 2016

SERIKALI KUPATA GAWIO LA BIL, 23/-



SERIKALI imepokea jumla ya sh. bilioni 23, kutoka kampuni tatu tofauti nchini, ikiwa ni gawio la mwaka 2015.

Kampuni hizo ambazo zina ubia na serikali ni Puma Energy Tanzania, iliyotoa gawio la sh. bilioni 4.5, Tipper sh.bilioni mbili na Benki ya NMB sh. bilioni 16.5.

Hafla ya makabidhiano ya gawio hilo ilifanyika jana, kwenye ofisi ya Msajili wa Hazina, mjini hapa na kuhudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Waziri wa Viwanda na Uwezeshaji, Dk. Charles Mwijage na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alizitaka kampuni zenye ubia na serikali kuiga mfano bora wa Puma Energy Tanzania, Tipper na NMB.

Dk. Mpango alisema kampuni hizo zimeonyesha uzalendo wa kutoa fedha, ambazo zitachochea uchumi wa taifa kwa manufaa ya wananchi.

Waziri huyo alisema fedha hizo zimetolewa katika kipindi mwafaka baada ya juzi, kusoma bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016-2017.

Alisema serikali imetenga sh. trilioni 11,820.503, sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ili kutekeleza miradi ya maendeleo katika mwaka ujao wa fedha.

Waziri huyo alisema baadhi ya kampuni, zikiwemo za nje, ambazo zina ubia na serikali, hazina mfumo bora wa kuweka hesabu zao vizuri,
hivyo kuinyima serikali mapato yasiyotokana na kodi.

"Huwezi kuniambia unafanya biashara kwa miaka 10 bila faida, haiwezekani. Kuanzia sasa nitaanza kuzifuatilia mimi mwenyewe kampuni zenye ubia na serikali, lakini hazitoi gawio kwa kisingizio cha kupata hasara, sitakubali," alionya Dk. Mpango.

Mwenyekiti wa Bodi ya Puma Energy Tanzania, Dk. Ben Moshi, alisema hadi kufikia Desemba 31, 2015, kampuni hiyo ilitengeneza faida ya sh. bilioni 31.5.

Dk. Moshi alisema kampuni hiyo iliwekeza kwa nguvu mwaka jana ili kuboresha miundombinu ya ndani na rasilimali kwa lengo la kukuza biashara yake.

"Bodi ya wakurugenzi imependekeza gawio la sh. bilioni 4.5, kwa mwaka ulioishia 2015, liweze kulipwa kwa serikali kutokana na utendaji mzuri wa kampuni. Mwaka 2014, gawio lilikuwa sh.bilioni tatu," alisema Dk. Moshi.

Mwenyekiti huyo alisema kampuni hiyo imekuwa ikifuatilia kwa karibu utendaji wa serikali ya awamu ya tano na imeridhishwa na kasi yake, hivyo Puma Enery Tanzania, itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha siku zote.

Dk. Moshi aliipongeza serikali ya Rais Dk. John Magufuli kutokana na mikakati yake ya kukusanya kodi na kutoa fursa kwa wawekezaji.

Hivi karibuni, Puma Energy ilishinda tuzo ya mwaka katika shindano lililofanyika Mei, mwaka huu, ambapo jumla ya nchi 47, duniani zilishindanishwa. Serikali na Puma Energy Tanzania, kila moja ina hisa asilimia 50.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru, alisema kuanzia sasa, wataanza kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa kampuni ambazo ni mbia na serikali ili kupata gawio la kila mwaka.

"Kunzia sasa serikali itakuwa makini sana na kampuni, ambazo ni mbia wake ili nazo zitoe gawio la kila mwaka, kama zilivyofanya Puma Energy, Tipper na NMB," alisema Mafuru.

No comments:

Post a Comment