Friday, 10 June 2016
WASHITAKIWA 12 KESI YA BARCLAYS WAACHIWA HURU
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru washitakiwa 12, wakiwemo polisi na mameneja wa Benki ya Barclays, tawi la Kinondoni, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi wa zaidi ya sh. milioni 300, baada ya kuwaona hawana kesi ya kujibu.
Hata hivyo, washitakiwa hao baada ya kuachiwa huru jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, walikamatwa tena na polisi.
Akisoma uamuzi wa iwapo washitakiwa wana kesi ya kujibu au la kwa niaba ya Hakimu Warialwande, Hakimu Mashauri alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa jamhuri ulikuwa na mashahidi 20.
“Mahakama imeona katika mashahidi, ushahidi uliotolewa hauendani na mashitaka kwa kuwa mashahidi wote wanaelezea baada ya tukio na si wakati wa tukio. Mahakama inawaona washitakiwa wote hamna kesi ya kujibu na inawaachia huru,” alisema.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, washitakiwa walikamatwa tena na kupelekwa mahabusu, ambapo baadae waliondolewa kwenda kituo cha Polisi.
Washitakiwa hao ni Meneja wa benki hiyo tawi la Kinondoni, Alune Kasililika, Meneja, Neema Batchu na wafanyabiashara Kakamie Julius, Hamis Shaban, Iddy Khamis na dereva Manasi Genyeka.
Pia, wamo wafanyabiashara Maulid Seifu, Sezary Massawe, Boniphace Muumba, Ruth Macha na maofisa wawili wa polisi, Sajini Iddy na Bundala.
Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kusaidia kutenda kosa na kuwasaidia watuhumiwa kutoroka ili wasiweze kuchukuliwa hatua na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Katika mashitaka hayo, mshitakiwa Ruth anakabiliwa na shitaka la kumsaidia Seifu kutenda kosa huku maofisa hao wa polisi wakidaiwa kuwasaidia washitakiwa wenzao, isipokuwa Seifu, kutoroka ili wasikamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment