Friday, 10 June 2016

RAIA WA TOGO ATUPWA JELA MAISHA



MAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi mkoani Kilimanjaro, imemuhukumu kwenda jela maisha, raia wa Togo, Josiane Dede Crippu (25), kwa kosa la kusafirisha dawa za kuleva zenye uzito wa gramu 1939.8, zikiwa na thamani ya sh.milioni 116.3.

Akisoma hukumu hiyo juzi, katika mahakama hiyo, Jaji Benedict Mwingwa, alisema upande wa jamhuri uliweza kuleta mashahidi tisa, ambao walitoa ushahidi ulioiridhisha mahakama hiyo bila kuacha shaka.

Jaji Mwingwa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Desemba 2, mwaka 2013, akiwa anataka kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ethiopia kuelekea jijini Dar es salaam.

Jaji huyo alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na mabegi mawili, moja jeusi na lingine rangi ya udongo, ambapo wakati yakipekuliwa kwa mashine, begi la rangi ya udogo lilihisiwa kuwa na kitu, lakini lilipopekuliwa, hakukuonekana kitu, hivyo maofisa wa polisi waliamua kulichana kitambaa cha ndani, ndipo walipokuta vipande viwili vya mito vikiwa na dawa hizo.

Alisema mtuhumiwa huyo aliwekwa chini ya ulinzi na dawa hizo zilifikishwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, ambapo alithibitisha kuwa zilikuwa ni dawa za kulevya aina ya heroen na cloradi, zenye uzito wa gramu 1,939.81.

Jaji Mwingwa alisema kutokana na jumhuri kutoa ushahidi pasipo kuacha mashaka, mtuhumiwa alitiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kwa sheria ya makosa ya jinai, kanuni ya 31, kifungu kidogo cha 6 ya mwaka 2012.

Baada ya kutiwa hatiani kwa mshitakiwa huyo,  Mwanasheria wa Serikali, Ignass Mwinuka, alidai hawana rekodi yoyote ya makosa ya nyuma yanayomhusu mtuhumiwa huyo na kuomba mahakama imhukumu kwa mujibu wa sheria za nchi.

Wakili wa upande wa utetezi, Davide Shilatu, alidai kwa kuwa mtuhumiwa huyo ni mwanafunzi wa Chuo cha Utalii nchini Togo na familia yake inamtegemea katika kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo, aliomba kupata unafuu katika hukumu itakayotolewa na mahakama hiyo.

No comments:

Post a Comment