Friday, 10 June 2016

WASOMI, WANASIASA WAIFAGILIA BAJETI YA SERIKALI


WASOMI na wadau mbalimbali wametoa maoni yao juu ya bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2016/ 2017, iliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango.

Katika maoni yao, wasomi wengi wamepongeza bajeti hiyo na kusema imelenga kuleta maendeleo ya Tanzania.

Aidha, wasomi hao wamesema iwapo kila mtendaji kwenye ngazi husika, atatekeleza wajibu wake ipasavyo, ikiwemo kudhibiti ukusanyaji wa kodi, bajeti hiyo itakuwa na manufaa makubwa.


PROFESA LIPUMBA
Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha CUF,  Profesa Ibrahim Lipumba alisema bajeti hiyo itakuwa na ahueni kwa wananchi kwa kuwa imegusa maeneo muhimu ya kiuchumi.

Hata hivyo, alisema ni vyema watendaji katika kila eneo wakasimamia ipasavyo ukusanyaji mapato na kuhakikisha kila fedha inatumika kulingana na malengo yake.

Profesa Lipumba, alikuwa akizungumza kwenye matangazo ya moja kwa moja yaliyorushwa na Televisheni ya TBC 1, wakati wa kusomwa kwa bajeti hiyo mjini Dodoma.

Alisema yapo maeneo, ambayo kimsingi yanagusa uchumi wa mtu mmoja mmoja, ikiwemo kwenye kilimo, hivyo kuondoa baadhi ya kodi kwenye mazao kutachochea ukuaji wa sekta hiyo na wakulima kwa jumla.

PROFESA BANA

Akichambua bajeti hiyo, Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema bajeti hiyo imejielekeza zaidi kutekeleza Ilani ya CCM kwa kudhibiti matumizi ya serikali, kurekebisha sheria ya manunuzi na kuwekeza zaidi katika miradi ya maendeleo.

Profesa Bana alisema japokuwa hakuna vyanzo vipya vya mapato zaidi ya serikali kuondoa misamaha ya kodi isiyo ya lazima, ikiwemo kodi za mishahara ya wabunge na kusamehe kodi kwa wakulima, bajeti hiyo imetoa matumaini makubwa kwa wananchi wa hali ya chini.

“Ni vizuri sasa bajeti hii ilenge zaidi wananchi wa pembezoni. Wapo watu Nkasi, Kibondo, Mrongo, Karagwe na Ngara wanaumizwa na ukubwa wa bei za bidhaa, ikiwemo vifaa vya  ujenzi. Bei hizo zidhibitiwe na hata watumishi wa maeneo hayo ni vizuri waongezewe posho, hasa wale wa sekta ya elimu, afya na kilimo,”alisema.

Msomi huyo alisema uwepo wa kodi za nyumba za kikoloni, zinazokinzana na sera ya makazi bora, ni tatizo na watakaoumia zaidi ni wapangaji huku kukiwa hakuna  matumizi bora ya kodi hizo, ikiwemo kuendeleza miundombinu ya majitaka.

Alisiifu serikali kwa kuendelea kudhibiti matumizi ya anasa, ikiwemo pombe, sigara na vinywaji baridi na kuongeza kuwa, ndio mfumo unaotumika kwa mataifa yote.

“Wakulima kuondolewa kodi peke yake haitoshi, sera ziboreshwe na kubuni njia za kufikia uwekezaji  huku benki ya kilimo nayo ikiongeza mitaji ya wakulima kwa kutoa mikopo nafuu katika sekta hiyo na wakuu wa mikoa na wilaya wasimamie kauli ya hapa kazi tu kwa kuhamasisha vijana vijijini kulima,”alisema.

Profesa Bana alisema ni vizuri bajeti hiyo ingebana mianya ya matumizi ya magari ya serikali kwa kuwa fedha nyingi zinapotea huko.

Alisema iwapo serikali itaamua gari za serikali zitumike na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pekee huku watumishi wengine wote wakitumia usafiri wa umma, ambapo itasaidia kupunguza pesa nyingi zinazopotea katika kugharamia magari hayo.

PROFESA MBENA

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana (St. Johns’ University), Profesa Emmanuel Mbena, alipongeza bajeti hiyo, hususani kwa kutenga fedha za kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi na kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Alisema ni jambo la faraja kwa serikali kukumbuka kuimarisha sekta za elimu na afya na pia kuboresha usafiri nchini.

“Sekta hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya nchi kwani watu wakiwa na afya bora na upatikanaji rahisi wa huduma za afya na wananchi kuelimika ipasavyo, hususani mpango wa elimu bure, taifa litasonga mbele. Kadhalika miundombinu ambayo inategemewa katika sekta za biashara, viwanda na kilimo,” alisema.

Aidha, alipongeza mikakati ya ukusanyaji fedha katika awamu hii ya tano kuwa ni mizuri kwa kuwa imezingatia kuwapunguzia wananchi kero za kodi ndogo zisizo za msingi, suala litakalosaidia kuleta maendeleo nchini.

“Nampongeza Waziri Dk. Mpango kwa bajeti nzuri, ambayo bila shaka inaelekezwa na kuongozwa na dira ya rais wetu aliyonayo ya Hapa Kazi Tu, ambapo kinachohitajika sasa ni  utekelezaji wake,” alisema.

Alisema ili utekelezaji kuonekana, ni lazima watu wajitoe na kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuunga mkono juhudi hizo na kuongeza kuwa amefurahishwa na muundo wake.

PROFESA NGOWI

Profesa Honest Ngowi wa Chuo Kikuuu cha Mzumbe, alisema bajeti hiyo kwa jumla ni nzuri kwa kuwa imeonyesha kuleta mabadiliko na maendeleo nchini.

Alisema asilimia 21, ya bajeti imeongezeka, ikilinganishwa na mwaka jana, kutoka zaidi ya bilioni 22 hadi bilioni 29, ambapo pia ipo changamoto ya kupata fedha zilizopotea.

Profesa Ngowi alishauri bajeti ya shughuli za kawaida (ziara, safari na vikao) kupewa kipaumbele, hata kama haitafikia ile ya shughuli za maendeleo, kutokana na unyeti wake.

Alisema bajeti ya maendeleo imechukua asilimia 60, ambapo ya shughuli za kawaida asilimia 40, na kwamba, ili shughuli za maendeleo ziweze kwenda vizuri, inabidi bajeti ya kawaida kutunishwa kwa kuwa inatengeneza shughuli  za maendeleo.

Msomi huyo alishauri kampuni za ndani kupewa tenda za ujenzi wa miundombinu mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa barabara na reli, kama ilivyoainishwa kwenye bajeti, ili kusaidia fedha kubaki ndani, badala ya kwenda nje, ambapo watazizungusha, ikiwemo  wazawa hao kuajiri Watanzania.

Profesa Ngowi alikosoa kuchajiwa kwa kodi ya ongezeko la thamani katika sekta ya utalii kwa asilimia 18, ikilinganishwa na Kenya na Afrika Kusini, ambayo inatoza asilimia 14. Aliasa kuwa, serikali inapaswa kutambua Kenya ndio mshindani mkubwa wa utalii katika ukanda huu wa Afrika.

Alishauri ili kupata fedha za kuongezea kwenye bajeti, lazima zifanyike juhudi za nguvu za ukusanyaji kodi na mapato mengine yasiyotokana na kodi.

PROFESA SHUMBUSO
Kwa upande wake, Profesa George Shumbuso wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema  iwapo bajeti hiyo itatekelezeka kwa asilimia 100, hatua ya serikali kuwekeza zaidi katika miradi ya maendeleo kuliko matumizi,  itakuwa na tija na kuzaa Tanzania mpya yenye uchumi imara.

Alisema ni wazi kuwa bajeti hiyo ina ahueni kwa wananchi kutokana na bidhaa muhimu kutopanda bei, lakini ipo haja mashine za kielektroniki (EFD), zisimamiwe ipasavyo na kuwapo mikakati mizuri ili zitumike kwa wafanyabishara wengi zaidi.

WABUNGE WAKOSHWA

MBUNGE wa Sengerema, William Ngereja (CCM), amesema bajeti hiyo ni nzuri na ikitekekezwa vyema, inaweza kukidhi haja na mahitaji ya Watanzania.

Alisema bajeti hiyo imegusa na imebana kila eneo na pia imeondoa utegemezi wa fedha kutoka kwa wafadhili na kujielekeza zaidi katika kutegemea fedha za ndani.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Makilagi, alisema bajeti hiyo ni ukombozi kwa wanyonge kwani inakwenda kuwatumikia wananchi walio wengi.

Kuhusu wabunge kukatwa kodi, alisema inawezekana wabunge wengine wasilipende, lakini kwa upande wake, analiona ni jambo zuri  kwani viongozi wanapaswa kuwa mfano na si kuwakandamiza wananchi pekee.

Philipo Mulugo, mbunge wa Songwe (CCM), alisema jambo la msingi ni kusimamia utekelezaji wa bajeti hiyo, badala ya kuishia kwenye machapisho na vinywani.

Mulugo alisema endapo bajeti hiyo haitatekekezeka, haitakuwa na maana, kwani kama ni kupanga na kuzungumza, imekuwa ikifanyika miaka yote, lakini kimsingi bajeti imekaa vizuri.

Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza, alisema bajeti hiyo ina mwelekeo mzuri na imelenga kumsaidia mwananchi wa kawaida.

Alisema kuna maeneo kodi imeongezwa ili kumsaidia wananchi na kuna maeneo, ambayo yamekatwa ili kuwasaidia watu wa kipato cha chini.

Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, alisema ni bajeti ya kufunga mkanda kwa sababu hakuna kiwango cha mabadiliko ambacho kimewekwa.

Kuhusu wabunge kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo, Maige alisema lazima ubishani mkubwa utakuwepo kuhusu kwa nini iwe kwa wabunge, wakati wapo wafanyakazi wengi wanaopata mafao na kwa kawaida hayakatwi kodi.

Alisema binafsi atakuwa tayari kwa kile kitakachoamuliwa, lakini ni bora wangefanya hivyo mapema kwa kukata kodi kwa posho za wabunge ambazo ni za kila siku.

Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, alisema bajeti hiyo ni nzuri na imegusa maeneo muhimu, hivyo wananchi wanapaswa kuiunga mkono serikali ili iweze kutekeleza malengo yake.

Ngonyani alisema kinachohitajika ni wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli katika ukusanyaji wa kodi.

Akizungumzia usajili wa magari yenye majina binafsi ya watu,
alisema anaunga mkono ada yake kuongezwa kwani lengo la serikali ni
kukusanya kodi ili kutekeleza miradi ya kijamii.

Mbunge wa Mufindi (CCM), Cosato Chumi, alisema kodi ya pikipiki ni kubwa sana na kuitaka serikali kuangalia upya ili kurahisisha vijana wengi kujiajiri.

Alisema kuongezeka kwa kodi hiyo, kutaumiza wananchi wote ambao wanatumia usafiri huo kama njia ya kurahisisha kufika kwao.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM, Hussein Bashe, alisema bajeti hiyo ni nzuri kwa kuwa katika kodi zilizoongezwa, hakuna inayomgusa mwananchi wa kawaida moja kwa moja.

Alisema kodi nyingi zilizoongezwa haziendi kuongeza gharama kubwa kwa wananchi.

“Kama nchi tuna changamoto ya kuongeza wigo wa kodi kwa kuibua vyanzo vya mapato. Wamesema kurasimisha sekta isiyo rasmi kuingia katika kodi, nayo ni mawazo mazuri,”alisema Bashe.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba  alisema bajeti imejielekeza katika mambo yanayoleta ufanisi na ni njia mbadala ya ukusanyaji wa mapato.

Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, alisema bajeti hiyo inafanana na Mpango wa Maendeleo, hivyo serikali inapaswa kuangalia masuala ya msingi, hasa mfumuko wa bei za bidhaa.

“Mfumuko wa bei unapaswa udhibitiwe ili kupunguza ugumu wa maisha. Bidhaa zinaongezeka bei kwa kasi,”alisema Shangazi.

Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Binto Binto alisema ana imani kuwa serikali imefanya utafiti wa kutosha juu ya sheria ya manunuzi kabla ya kupeleka hati ya dharura bungeni.

Mwanafunzi wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jenson Jingo, alisema bajeti hiyo imezingatia makundi yote na kwamba ni wakati wa vijana kuamka na kufanya kazi.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akizungumzia bajeti hiyo, alisema ni ya deni la Taifa kwa kuwa kiasi cha fedha sh. trilioni nane za makusanyo ya mapato, zitakwenda kulipa deni hilo.

“Makusanyo ya mwaka mzima ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni takriban shilingi trilioni 15, sasa trilioni nane zinakwenda kulipia deni la taifa na trilioni saba zinalipa mishahara. Ndio maana Waziri Mpango alikuwa kila mara akisema, 'ukiondoa deni la taifa' kwa sababu ni kubwa.

“Maana yake ni kwamba, fedha zinaporomoka, wasiwasi wangu ni uwezo wa serikali wa kuweza kukusanya fedha hizo inazotarajia. Inabidi tusubiri kwa mwaka mmoja tupime jambo hilo,” alisema.

Kuhusu msamaha wa kodi, Zitto ambaye ni mmoja wa wajumbe katika kamati ya bajeti, alisema walipendekeza isizidi asilimia moja ya pato la taifa.

“Wameondoa msamaha wa kodi kwenye taasisi za dini na jeshi, lakini ni kiwango kidogo mno cha msamaha. Kiwango kikubwa cha msamaha wa kodi kipo kwenye sekta ya madini, ambayo ni asilimia 75, lakini hakujaguswa,” alisema Zitto.

Kuhusu makato ya kodi katika posho za wabunge, alisema suala hilo limewekwa kisiasa na ingekuwa vyema lingefanyika mwaka 2020, wakati ambao wabunge wanamaliza muda wao.

“Limetamkwa ili kuwafurahisha tu wananchi, sheria inaeleza wazi posho za wabunge hazitozwi kodi. Tunalipwa malipo ya aina tatu, mshahara, posho ya siku (120,000) na ‘sitting allowance’ 220,000 ambayo sijui ilitokea wapi,"alisema.

Zitto alisema kwa upande wa kodi (VAT) kwa bidhaa zinazotoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar au Zanzibar kwenda Bara, zitazorotesha uchumi wa Zanzibar.

“Sijui mantiki ya makubaliano haya, sheria inasema lazima waziri kabla hajatangaza, akubaliane na mwenzake wa visiwani, nategemea mjadala mkubwa katika hili kwa sababu itaumiza uchumi wa Zanzibar, na ile VAT kwenye utalii inaweza kuathiri sekta nzima ya utalii,” alisema.

TGNP
Wakati huo huo, Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP), umeipongeza serikali kwa kuongeza fedha katika bajeti ya maendeleo katika bajeti kuu ya mwaka 2016/17.

Pongezi hizo zilitolewa Dar es Salaam, jana na Mwanaharakati wa TGNP, Janeth Mawinza, wakati akitoa tamko la wanaharakati hao kuhusu bajeti ya mwaka 2016/17.

Janeth alisema bajeti hiyo imeongezeka kuliko bajeti zilizopita katika masuala ya maendeleo wakati bajeti zilizopita, ziliegemea katika matumizi ya kawaida.

“Kwa bajeti ya matumizi ya maendeleo mwaka 2016/17, imevunja rekodi kwa ongezeko la asilimia 49.9, kutoka sh. bilioni 5,919.1 za mwaka 2015/16 hadi sh. bilioni 11,820.5 kwa mwaka 2016/17. Hii ni hatua ya kupongeza,"alisema.

Janeth alisema ongezeko hilo ni la kwanza katika historia ya bajeti za Tanzania na kwamba ni hatua inayopaswa kupongezwa.

Hata hivyo, alitoa angalizo kwa serikali kuwa, fedha zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo, zitumike ipasavyo ili zisaidie makundi yote ndani ya jamii, hususan yale yanayokabiliwa na lindi la umasikini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Lihundi, alisema wananchi wanatakiwa kuifahamu bajeti ya serikali yao iwapo imegusa kutatua kero zao.

Lilian alisema serikali haina budi kuhakikisha bajeti iliyotengewa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inajali huduma za uzazi salama,ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kuboreshwa


SHIRIKISHO LA VYUO VIKUU

Mwenyekiti wa  Shirikisho la Vyuo Vikuu Vya  Dar es Salaam (CCM), Imani Matabula, alisema  bajeti ya  mwaka huu imekuwa ya kiukombozi  kwa kuwa imeongeza matumizi ya  maendeleo na  kuwa na dhamira ya  kuikomboa  Tanzania.

Alisema anaipongeza serikali ya  Rais John Magufuli  kwa kuweka usawa kwa  wafanyakazi kwa kumtaka kila mtu kulipa kodi.

"Hii ni  bajeti iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu sana na  ni moja ya utekelezaji wa ahadi ya  Rais  John Magufuli  kwa  kuanzisha  mahakama ya mafisadi, lengo likiwa  kutokomeza ufisadi nchini,"alisema.

Matabula  aliitaka serikali kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri  na  zinaleta maendeleo  nchini kama zilivyokusudiwa.

Mwanafunzi wa  Chuo Kikuu cha  Muhimbili, Ludovick  Fredrick, alisema bajeti  iliyotengwa  ni  nzuri  kwani  imewekeza zaidi katika viwanda.

Mwanaharakati na Balozi wa Baraza la Vijana Tanzania, Godfrey Mbowe alisema wanaamini bajeti zilizotengewa kwa wizara zitakwenda kutumika kwa malengo sawa ya kuendeleza maeneo husika.

Alisema kwa upande wa wizara ya miundombinu, imetengewa bajeti kubwa, ambayo inatakiwa kutumika kwenye ujenzi wa miundombinu, reli na barabara zenye ubora na sio mbiundombinu iliyopo, ambayo imejengwa kwa kiwango cha chini na kusababisha fedha nyingi kupotea kwenye  marekebisho.

Alibainisha kuwa nchi haiwezi kwenda kwenye ujenzi wa viwanda au uchumi wa kati kama hakutakuwepo na barabara imara zilizojengwa kwa kiwango kinachotakiwa.

Mbowe alisema kwenye upande wa elimu, imetengwa bajeti ya sh. trilioni nne, ambazo wanahitaji kuona zikitumika kusaidia suala la elimu bure iwe elimu bora na sio bora elimu.

WENYE UALBINO WAIKUBALI

Mwenyekiti wa Taasisi ya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (TAS), Nemes Temba, aliipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kutenga bajeti nzuri na kubwa, ambayo imekuwa ni gumzo kila kona.

Alisema jambo la kwanza, ambalo limekubalika na litakuwa historia katika bajeti ya mwaka 2016/2017, kwa miaka yote ijayo ni kitengo cha watu wenye ulemavu kuwekewa bajeti, jambo ambalo halijawahi kufanyika kabisa hapa nchini.

Temba alisema pamoja na kwamba bajeti ni ndogo, wanampongeza Rais Dk.John Magufuli, kwa kutambua umuhimu wa idara hiyo na kwamba, wana imani kadiri miaka inavyokwenda mbele,
kutokana na changamoto zitakazojitokeza, itaongezwa.

Aneti Mushi (25), mkazi wa Dar es Salaam, alisema serikali ya awamu ya tano imejitahidi katika kurudisha nidhamu kazini, maadili pamoja na utengenezaji wa bajeti kubwa, ambayo haijawahi kutokea.

Alisema kama wasimamizi wa wizara watasimamia vizuri fedha zilizotengwa kwenye bajeti hiyo, baada ya miaka mitano, nchi itakuwa kwenye uchumi wa kati huku umasikini  ukiwa historia.

No comments:

Post a Comment