Tuesday 26 July 2016

RAIS MAGUFULI AANDIKA HISTORIA MPYA CCM

RAIS Dk. John Magufuli juzi aliandika historia mpya ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuibuka na ushindi wa kishindo wa asilimia 100.

Dk. Magufuli alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa CCM baada ya kupata kura zote  2,398, za wajumbe kutoka mikoa yote ya Tanzania, waliohudhuria mkutano huo.

Rais Magufuli amekuwa mwenyekiti wa tano wa CCM tangu Chama kilipozaliwa Februari 5, 1977. Wenyeviti waliomtangulia ni Mwasisi wa CCM Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Hii ni mara ya kwanza kwa mgombea wa nafasi hiyo wakati wa kupokezana uenyekiti wa CCM kupata kura zote za ndio bila kuwepo kwa kura ya hapana au iliyomkataa.

Katika uchaguzi uliofanyika Juni, 1990, kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, wakati Mwalimu Nyerere akimuachia uenyekiti wa Chama, Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, idadi ya kura zilizopigwa ilikuwa 1,851, ambapo Rais Mwinyi alipata kura 1,846. Kura tano zilikuwa za hapana na moja iliharibika.

Aidha, kwa upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti bara, marehemu Rashid Kawawa aliibuka mshindi kwa kupata kura za ndio 1,852. Kura nane zilikuwa za hapana na moja iliharibika.

Katika uchaguzi wa Juni 22, 1996, uliofanyika kwenye ukumbi wa Chimwaga, mjini Dodoma, Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa aliibuka mshindi kwa kupata kura 1,248 kati ya kura 1,259 zilizopigwa. Kura nane zilikuwa za hapana na tatu ziliharibika.

Katika uchaguzi uliofanyika Juni 25, 2006, kwenye ukumbi wa Chimwaga mjini Dodoma, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliibuka mshindi kwa kupata kura 1,812 kati ya kura halali 1,813 zilizopigwa. Kura moja ilisema hapana na hakukuwa na kura iliyoharibika.

Na sasa Rais wa awamu ya nne, Dk. Magufuli ameweka historia mpya baada ya kushinda kwa asilimia 100 huku kukiwa hakuna kura iliyosema hapana wala kumkataa.

Wakati Mzee Mwinyi akipokea uongozi kutoka kwa Mwalimu Nyerere, alizungumzia umuhimu wa kuendeleza misingi ya siasa yake ya usawa, haki na heshima kwa Watanzania wote.

Aidha, Mzee Mwinyi aliwataka wana-CCM kujidhatiti kwa kuimarisha juhudi za kukisafisha Chama ili kujenga na kudumisha imani ya umma. Pia alizungumzia umuhimu wa kuimarisha demokrasia ya umma kwa kusikiliza, kutathmini na kuzingatia maoni ya wanachama.

Pia aliwataka viongozi kuwa karibu na wananchi na kupiga vita ubadhirifu ndani ya CCM katika ngazi zote na kuhakikisha kuna usafi, uadilifu na uwajibikaji  kwa watendaji wake katika ngazi zake. Pia alitaka Chama kipunguze gharama za kuendesha shughuli zake ili zilingane na uwezo wa wanachama wake.

Kwa upande wake, Mzee Mkapa alizungumzia kuendeleza kasi ya kukisafisha Chama huku akitahadharisha kuwa, isingekuwa busara kufika mwaka 2000, huku wanachama wake wakiwa hawaridhiki na usafi wa CCM.

Mzee Mkapa alisema ili Chama kiendelee kuungwa mkono, hatua mbalimbali na madhubuti zitachukuliwa ili kiimarike kwani hawezi kuwa kiongozi wa Chama kitakachoshindwa katika uchaguzi mbalimbali.

Pia aliwataka wanachama wasiogope kufanya mabadiliko ndani ya Chama na kwamba, vyama vya TANU na ASP vilikuwa mfano mzuri wa kujisahihisha na kufanya mabadiliko pale inapobidi.

Mzee Mkapa pia alisisitiza umuhimu wa Chama kuongozwa na timu ya viongozi waadilifu na wenye upeo. Alionya kuwa CCM haiwezi kupata nguvu na dhamira ya kukemea viongozi wa serikali wanaotumia madaraka yao kwa kujinufaisha au kwa upendeleo iwapo walioko ndani ya Chama watakuwa na maradhi hayo hayo.

Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete naye hakuwa na mtazamo tofauti na ule waliokuwa nao Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa. Yeye alisisitiza umuhimu wa viongozi, watendaji na Jumuia za Chama kubadilika ili kuleta uhai kwenye Chama.

Kikwete alisema Chama imara ni kile ambacho viungo vyake vimekamilika na vinafanyakazi vizuri, kina wanachama wengi, viongozi wanaoitisha vikao na watendaji imara pamoja na rasilimali na jumuia imara.

Aidha, Kikwete alizungumzia umuhimu wa Chama kuwa na vyanzo vingi vya fedha ili kiweze kujiendesha. Aliwataka viongozi kuchuna bongo zao, kubuni mikakati, mbinu na mipango, ambayo itakiingizia Chama fedha na kukipa rasilimali za kufanyia kazi kwa uhakika.

Mikakati iliyotangazwa na wenyeviti hao wastaafu watatu haina tofauti na vipaumbele vilivyotangazwa na Rais Magufuli juzi, baada ya kukabidhiwa uenyekiti na Rais mstaafu wa awamu ya nne Kikwete.

Rais Magufuli amesema mkakati wake wa kwanza ni kuimarisha utendaji kazi ndani ya Chama, kujenga Chama chenye uwezo wa kuisimamia serikali na kwamba, viongozi wa Chama ndio watakuwa ‘mabosi’ wa watendaji wote walioko serikalini.

“Uwe makamu wa rais, waziri mkuu, waziri, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya  na hata katibu tarafa, utaongozwa na viongozi wa Chama na wana-CCM,”alisema na kuongeza kwamba, watendaji watakaoshindwa kujua mabosi wao ni viongozi wa CCM wajiondoe wenyewe.

Eneo lingine ambalo Mwenyekiti huyo mpya wa CCM alisema atalifanyia kazi ni kuangalia muundo wa Chama  na kuhakikisha kinakuwa na safu bora na kuondoa vyeo visivyo na tija kwenye Chama.

Dk. Magufuli alitolea mfano watoto wanaoijiunga na chipukizi, ambao ni kuanzia umri wa miaka 8 hadi 15, kutumika kwenye shughuli za kisiasa badala ya kwenda shule.

Alisema  kuna haja ya suala hilo kuangaliwa upya kwa kuwa kuna hatari kwa vyama vingine kuibuka na makundi ya namna hiyo, badala ya kuwaacha watoto hao kuendelea na mfumo wa elimu.

Aidha, mwenyekiti huyo alihoji umuhimu wa uwepo wa makamanda wa vijana, walezi wa jumuia na washauri wa wazazi huku wengi wenye vyeo hivyo wakiwa ni watu wenye fedha.

Pamoja na hilo, alihoji  mtindo wa wanasiasa kujirundikia vyeo huku akitoa mfano  wa waziri kuwa mbunge, kamanda wa vijana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, jambo ambalo alisema linawanyima fursa wanachama wengine kupata nafasi za uongozi.

Aliwataka wanachama wa CCM kuwa mfano kwenye kuongoza mabadiliko ndani ya Chama kwa kuwasimamia watendaji serikalini na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, hatua ambayo itawavutia wananchi kujiunga na chama, kwa kuwa msingi wa chama ni kuwa na idadi kubwa ya wanachama.

Dk. Magufuli alisema katika uongozi wake, atahakikisha anasimamia kanuni na maadili ya uongozi ndani ya Chama na kudhibiti wanachama maslahi na  wala rushwa ambao wamekuwa wakiharibu sifa ya Chama.

“ Chama chetu ni miongoni mwa taasisi ambazo zina tatizo la rushwa. Katika uongozi wangu, kiongozi anayesaka uongozi kwa rushwa, hatakuwa na nafasi.Mimi nitasema ukweli na ukweli utabaki kuwa ukweli,”alisema.

Alisema rushwa imekuwa chanzo cha CCM kupoteza nafasi mbalimbali kutokana na kuteua wagombea wasiokubalika baada ya kutoa fedha na kuwaacha wanaokubalika kwa wananchi wakishindwa kupata nafasi.

Dk. Magufuli alisema katika uongozi, yeyote atakayetoa rushwa hatachaguliwa ndani ya CCM na kurejea uzoefu alioupata wakati wa kinyang`anyiro cha kuwania nafasi ya kuteuliwa na Chama kuwa mgombea urais, ambapo alikumbana na changamoto hizo mkoani Iringa.

“Mimi nachukia rushwa na hata mwenyekiti wetu mstaafu anaichukia. Alituonyesha mfano kwa vitendo kwa kumchinjia mbali rafiki yake (Lowassa) bada ya kugundua ni mtoa rushwa na ni fisadi,”alisema na kuonya kwamba mwakani  kutakuwa na uchaguzi wa Chama, hivyo hatakuwa na simile kwa yeyote atakayetoa rushwa.

Mwenyekiti mpya wa CCM pia ameahidi kupambana na kukomesha usaliti ndani ya Chama huku akisisitiza ni kheri kuwa na mchawi kuliko msaliti kwenye chama. Aliwataka
wanachama wajirekebishe na kutubu kuanzi leo na kama wapo waache au waondoke hata leo.

“Baadhi ya watu ni wasaliti, mchana wako CCM, usiku wanakuwa CHADEMA. Mimi siamini kama wasaliti kama wana CCM wasaliti wanahitajika ndani ya Chama,”alisema.

No comments:

Post a Comment