Saturday, 30 July 2016

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU AJIRA ZA WATUMISHI WA MIKATABA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo mazito kwa halmashauri nchini, ikiwemo kuondokana na uwepo wa watumishi wa mikataba ili kuepukana na matundu ya watumishi hewa.

Aidha, amewataka madiwani na wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia vyema fedha zinazotolewa na serikali za maendeleo kwa kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa na miradi inajengwa katika kiwango kizuri.

Pia, amesema serikali imedhamiria kupunguza kero za watumishi, ambapo imepata muarobaini wa uwepo wa madeni ya walimu wanaopashindwa madaraja na ulipaji kwa kuwa na mfumo, ambao kuanzia sasa, baada ya kupandishwa vyeo watakuwa wakipatiwa mishahara mipya haraka.

Majaliwa alitoa maagizo hayo jana, mjini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na madiwani wa wilaya za Kigamboni na Temeke, wakurugenzi na watendaji wa halmashauri ya Temeke.

“Halmashauri ya Temeke inaongoza kwa kuwa na watumishi wa mikataba, ambao wapo 89,” alisema Majaliwa na kumnyanyua Kaimu Ofi sa Utumishi , Zaituni Hassani ili kutoa maelezo juu ya hilo.

Kaimu Ofi sa Utumishi huyo, alisema watumishi wengi wa mikataba ni madereva, jambo ambalo lilimfanya Waziri Mkuu kumhoji tena kwanini, ambapo alijibu hali hiyo imetokana na kutopata wale wenye sifa ambao wana vyeti kutoka VETA.

Waziri Mkuu Majaliwa alimhoji ofi sa huyo mwisho wa kutangaza nafasi za kazi ni lini, ambapo alijibu ni mwaka jana.

“Nenda kajiridhishe, nakupa mwisho Julai 30, mwaka huu, kawaajiri kama wana sifa, hayo ndiyo matundu ya watumishi hewa. Maelekezo haya nayatoa kwa idara zote za uhasibu, ujenzi ambako wengi wana mikataba,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kama watumishi wana sifa ya kuajiriwa, maofi sa utumishi waombe kibali cha kuajiri.

Pia, alisema kwa kufanya hivyo, kutawawezesha watumishi hao wa mikataba kujua mustakabari wa maisha yao iwapo wana sifa za kuajiriwa ama la, kwa kuwa wamekuwa hawana uhakika wa maisha yao kama vibarua.

“Watumishi kwenye halmashauri tunataka waajiriwe kama hawana sifa wajue,” alisisitiza.

Kuhusu fedha zinazotolewa na serikali, Majaliwa alisema ni vema sasa watumishi na wawakilishi wa wananchi kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi inatekelezwa tena kwa kiwango.

“Mkurugenzi mtendaji, mweka hazina ile fedha inayokuja ina maelekezo, hivyo lazima utoe taarifa kwa madiwani. Pia, lazima mapokezi ya fedha, taarifa imfi kie mkuu wa wilaya na matumizi yake,”alisema.

Aidha, alisema wakuu wa wilaya wana wajibu wa kujua fedha zilizoingia na shughuli yake na kuhakikisha zinatumika kwa kile kilichokusudiwa.

Akizungumzia kupunguza kero za watumishi, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imedhamiria kuzipunguza kwa kuyafanyia kazi madeni ya watumishi na maelekezo yametolewa ili kujua kiwango cha madeni kwa kila idara.

Alisema katika sekta ya elimu, wamebadirisha mfumo uliokuwepo awali, ambao ulikuwa unasababisha malimbikizo ya madeni.

“Kuanzia sasa ukipandishwa daraja, basi na mshahara mpya unapata bila ya kuchelewa kwa kuwa hapo awali kulikuwa na vyombo viwili ambavyo vilikuwa havina mawasiliano,”alisema.

Alisema kwa wale ambao walicheleweshwa kupandishwa vyeo, watapandishwa na kwa sasa mwalimu akipanda daraja na kupewa barua, anapata mshahara mpya haraka.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwasisitizawatumishi kuwa na nidhamu, uadilifu na uaminifu kazini na kushirikiana na kuahidi kwamba, serikali haitasita kumchukulia hatua mtumishi yeyote ambaye hatatekeleza wajibu wake.

Mbali na hayo, alizitaka halmashauri zote nchini ziimarishe upimaji wa makazi mapya na ziendelee kupanua vyanzo vya mapato, kukusanya vizuri mapato na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.

No comments:

Post a Comment