Thursday, 4 August 2016
DIWANI CHADEMA AHUKUMIWA KWENDA JELA MWAKA MMOJA
DIWANI wa Kata ya Mkoma, wilayani Rorya, Lazaro Kitori (CHADEMA), amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja na kulipa fidia ya sh. 700,000.
Mshitakiwa amepewa hukumu hiyo baada ya kutiwa hatiani kwa kumshambulia na kumjeruhi askari polisi, Jacob Malambom, akiwa kazini wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu, uliofanyika mwaka jana.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Marther Mpaze, ambapo alisema kuwa mahakama imeridhishwa bila kuacha shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Upande wa mashitaka uliongozwa na Mwendesha Mashitaka wa polisi, Bukuru Bugombe, ambapo uliwasilisha mahakamani hapo fomu namba tatu ya matibabu (PF3).
Awali, Bugombe alidai mahakamani hapo kuwa, Oktoba 22, mwaka jana, wakati PC Malambo wa Kituo cha Polisi Shirati, akiwa kazini katika mikutano ya kampeni, ambao Kitori alikuwa mgombea udiwani wa CHADEMA, akiwa na wafuasi wa chama hicho, akiwemo mpambe wake, Richard Juma, katika kata ya Mkoma, kulitokea vurugu iliyosababishwa na wafuasi wao kumshambulia kwa kumpiga na kumjeruhi askari huyo na kumsababishia maumivu.
Hakimu Mpaze alisema kutokana na ushahidi ulitolewa na upande wa mashitaka, mahakama imeridhishwa na ushahidi huo na kwamba, inawatia hatiani washitakiwa Kitori na Juma, ambaye hakuwepo mahakamani hapo wakati wa hukumu.
Alisema washitakiwa hao kila mmoja atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela na kumlipa fidia ya sh. 700, 000, Malambo ili iwe fundisho kwa watu wengine, ambao wanakiuka sheria za nchi kwa kuwadhuru wenzao .
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment