Monday, 8 August 2016

KIAMA CHA MADEREVA CHAJA

SERIKALI imetangaza kuweka mitego maalumu kwa madereva na askari watakaotoa na kupokea rushwa ili kubariki kupindishwa sheria za usalama barabarani.

Pia, abiria watakaoshawishi madereva kukiuka sheria na kutembea mwendo kasi, kutovaa mikanda na kofia ngumu, watachukuliwa hatua kwa kuwekwa mahabusu saa 24 na kufikishwa mahakamani.

Aidha, magari ya jeshi na mengine ya serikali yanayokiuka sheria za usalama barabarani na kutanua kwa makusudi na vigogo wanaomiliki mabasi na kutenga fungu la kuhonga polisi, wameonywa kuwa hizi ni zama zingine, hivyo wafuate sheria.

Pia, madereva walevi na wazembe sasa watafutiwa leseni na walinzi shirikishi wamepigwa marufuku kujihusisha kukamata vyombo vya usafiri, ikiwemo pikipiki barabarani huku askari atayefanya vizuri kuzawadiwa na atakayeachia gari ikiwa na makosa kuadhibiwa.

Hayo yalisemwa jana, jijini Dar es Salaam, wakati wa kuzindua mkakati wa baraza wa kukabiliana na ajali na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa  Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Hamad Masauni.

Alisema hatua hizo ni moja ya mikakati inayolenga kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani.

“Haiwezekani gari lina makosa, limepita kote huko linakuja kukamatiwa Kimara. Lazima askari wa Chalinze aliyekuwepo tumhoji lilipitaje? Kama alienda msalani au alikuwa na maslahi yake, atatueleza vizuri,”alisema Masauni.

Masauni alisema mkakati huo umeanza kufanya kazi jana na utakamilika Februari, mwakani, lengo likiwa kuleta mabadiliko ya kiusalama katika matumizi ya barabara.

Alisema serikali imebaini chanzo kikubwa cha ajali ni makosa ya makusudi ya kibinadamu, ikiwemo ulevi, uzembe, mwendokasi, miundombinu na ubovu wa vyombo vya usafiri, hivyo mkakati huo utadhibiti makosa hayo.

Masauni alisema lengo la mkakati huo ni kuwa na tija na matokeo ya kudumu katika kudhibiti ajali zisizo za lazima barabarani.

Pia, alisema wapo baadhi ya askari wanachafua sifa ya jeshi la polisi kwa kujihusisha na upokeaji rushwa barabarani, hivyo katika mkakati huo, kutakuwa na mitego kabambe ya kiintelejinsia, ambayo itawakamata wapokeaji na watoaji rushwa.

“Wananchi wajue atakayejipendekeza kushawishi askari kupokea rushwa na yeye hatutamuacha, ndio maana tunasema tutatumia intelejinsia ya hali ya juu. Hatuwezi kupunguza ajali kwa kuchekeana, nguvu kazi ya taifa inapotea, wakiwemo watoto na raia wasio na hatia,”alionya.

Aliongeza kuwa ili kutoa mwanya wa mkakati huo kutekelezeka ipasavyo, ipo haja ya kufanya marekebisho ya sheria mapema ili kuwa na wigo zaidi wa kudhibiti wanaojihusisha kuvunja sheria na kuongeza adhabu.

Masauni alisema askari wa kikosi cha usalama barabarani, madereva na wamiliki, watapewa mafunzo na kuelezwa madhara ya rushwa na jinsi ya kusahau tabia hizo ili kulinda usalama wawapo kazini na atakayekiuka hakutakuwa tena na simile.

“Walio mabingwa wa kuvunja sheria za barabarani, yatakayotokea yatawafunza, tunahitaji kushirikiana ili kumaliza changamoto za ajali,”alisema.

Masauni alisema wanazo taarifa za baadhi ya vigogo wanaomiliki vyombo vya usafiri, kutenga fungu la pesa ili kununua tochi  na kuwawezesha madereva kwa kuhamasisha uvunjifu wa sheria, hivyo waache kufanya hivyo au waache kufanya baishara hiyo kama haitawalipa wakifuata sheria.

“Hizi ni zama zingine, wamiliki wanaowaza kusaka pesa bila kujali uhai ni bora wabadili biashara au wafuate sheria, maana tutafuta leseni zao za biashara na kufungia leseni za madereva ili wafanye kazi nyingine,”alisema Masauni.

Naibu waziri huyo alisema katika mkakati huo pamoja na kurekebisha sheria,  abiria wanaoshawishi dereva kwenda mwendokasi, kutofunga mikanda, kuvaa kofia ngumu na kupanda pikipiki zaidi ya mtu mmoja (mishikaki), hawatasalimika na watachukuliwa hatua, ikiwemo kuwekwa rumande kwa saa 24 na kufikishwa mahakamani.

Pia, alisema watu wanaong’oa alama za usalama barabarani na kuuza au kununua kama chuma chakavu, nao watasakwa na kuchukuliwa hatua kali huku dereva atakayekutwa anaendasha huku akiwa amelewa, kutumia simu na vioo vya giza, kutokuwa na leseni na bima nao kudhibitiwa.

Katika kutekeleza hayo, Masauni alisema utaratibu wa nukta kwa leseni za madereva utazingatia ukubwa wa kosa na atayefutiwa nukta zote 15, hataruhusiwa tena kuendesha chombo cha moto hapa nchini.

Aidha, katika mkakati huo, kutakuwa na udhibiti wa magari binafsi yenye tairi moja nyuma, ikiwemo Noah, kufanya biashara ya usafirishaji abiria na kusafiri zaidi ya kilomita 50, kuongeza viti na magari yasiyo na sifa ya kufanya bishara na vyuo vya udereva, navyo kuchukukuliwa hatua.

Alihimiza matumizi ya makundi maalumu katika barabara, ikiwemo alama za barabarani na usalama wa watoto na kuahidi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), kufanyia kazi matatizo ya miundombinu ili kuimarisha usalama.

Masauni alisema mkakati huo umeipa rungu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kubaini kwa kutumia mfumo wa kisasa, madereva wanaokimbia zaidi na kufungia kampuni na vyombo vya usafiri visivyo na sifa.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema wamepiga marufuku ulinzi shirikishi katika kazi za usalama barabarani, ikiwemo kukamata pikipiki zinazoingia mjini kwa kuwa wanachafua sifa za jeshi hilo.

Alisema wapo baadhi ya walinzi shirikishi wamekosa sifa na wamekuwa hawana utaalamu wa kutosha katika kukagua vyombo vya moto, hivyo wasifanye kazi hiyo tena.

No comments:

Post a Comment