Monday 8 August 2016

MAKAMBA: CCM HAINA MISINGI YA RUSHWA



KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, amesema CCM haina misingi ya rushwa, ndio maana wote waliochafuka kwa tatizo hilo ama wanaondolewa au wanakimbia wenyewe.

Amesema tuhuma zilizotolewa na Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja, kuwa yeye ni muasisi wa rushwa ndani ya Chama, ni za uongo.

"CCM kama taasisi haina na inakataza rushwa. Moja ya ahadi za mwanachama inatamka wazi kwamba, rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa, ingawa wapo wanachama wanaolalamikiwa na kuhusishwa na rushwa, akiwemo Mgeja (alipokuwa CCM),"alisema.

Makamba alisema hayo jana, wakati akizungumza na Uhuru, baada ya gazeti moja la kila siku (sio Uhuru), kuandika habari iliyokuwa na kichwa cha habari 'Makamba Mwasisi wa Rushwa-Mgeja', ambayo ndani yake inadai Katibu Mkuu huyo mstaafu ndiye aliyechochea rushwa.

Makamba alisema kilichoelezwa na Mgeja ni uzushi na uongo wa wazi kwa kuwa wakati wote wa ukatibu mkuu wake, alikitumikia Chama kwa uadilifu bila ya kuongozwa na rushwa ili kupindisha au kutoa haki.

Alisema badala yake ni Mgeja ndiye aliyekuwa na tuhuma za rushwa na ufisadi kwani mbali na CCM, hata taasisi mbalimbali alizowahi kuziongoza zilighubikwa na tatizo hilo na kusababisha zingine kufilisika.

Makamba alisema moja ya taasisi hizo ni Chama cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU), ambacho Mgeja aliwahi kuwa mwenyekiti wake, ambako alihusishwa na ufisadi mkubwa uliosababisha kifilisika.

Mbali na SHIRECU, pia alipokuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, alikuwa akilalamikiwa na wana-CCM, hususan wanaotaka kuwania nafasi za uongozi kwamba, walikuwa hawapati nafasi hizo hadi Mgeja ashibe.

"Tunatambua kwamba wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, alikuwa mbebaji wa mfuko wa fedha za mgombea mmoja wa urais na kupita akigawa rushwa. Alipokuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, alikuwa akilalamikiwa sana kwamba ili mwanachama ateuliwe kuwania uongozi, lazima Mgeja ashibe.

"Kilichotokea SHIRECU chini ya Mgeja kinajulikana....kilichotokea Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT), wakati huo kikiongozwa na Mgeja mkoani Shinyanga kinajulikana.

"Kilichompeleka huko aliko sasa kisiasa ni njaa. Mgeja aache unafiki. Nilipokuwa Katibu Mkuu wa CCM, alikuwa akiniita 'Brother' na alikuwa akinisifu kila kikao, kulikoni leo? Urafiki wa Mgeja ni wa paka, unategemea bakuli la maziwa kalishika nani. Nimevunja kanuni ya kutobishana na mjinga,"alisema Mzee Makamba.

Makamba alisema Mgeja anaongozwa na tamaa inayomfanya asichukie rushwa, ndio maana alipoondoka CCM, mmoja wa wanachama waliokatwa kuwania urais katika uchaguzi huo kwa sababu za rushwa, naye aliondoka na kumfuata aliko.

Alisema yeye ni kiongozi safi na ataendelea kuwa hivyo kwa maslahi ya wana-CCM na taifa zima kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment