Monday 8 August 2016

VIGOGO ATC WATUMBULIWA


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewasimamisha kazi vigogo wawili wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), akiwemo Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Injinia Jonathan Mfinanga.

Viongozi hao wamesimamishwa baada ya kusababisha mchakato wa kuwapata marubani wenye uwezo ili waende kozi Canada, kwa ajili ya kurusha ndege mbili zitakazonunuliwa na serikali kutokwenda vizuri.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo jana wakati wa ziara yake katika Bandari ya Itungi iliyopo wilayani Kyela.

“Lililotokea ni kuwa niliagiza wachukuliwe marubani ambao wana uwezo ili tuwapeleke Canada na niliwaambia ATC kuwa huu ni mchakato muhimu, nataka marubani hao waende” alisema Profesa Mbarawa.

Aliongeza kuwa walichaguliwa marubani, lakini kidogo mchakato huo haukwenda vizuri, hivyo alitoa maelekezo kwamba mashirika yote ikiwemo ATC, watu lazima wawe na nidhamu ili wakifanya vitu wafanye vya uhakika.

“Nimeletewa ripoti ile leo (jana) asubuhi kwamba kuna tatizo limejitokeza na nikasema kila aliyesababisha tatizo hili awajibike, na wale watu walikuja ofisini kwangu ambapo niliwauliza mara mbili kama hiyo list ipo vizuri, hamna matatizo na wakanijibu mheshimiwa ipo vizuri,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema tatizo litatatuliwa kwa sababu muda haupo, wale marubani wanatakwa wasafiri kesho (leo) hivyo tukisema tuanze kufanya mambo mengine, itatuchelewesha.

Profesa Mbarawa alisema kozi hiyo inaanza Agosti 8, mwaka huu, hivyo ametoa maagizo kwamba wale waliokuwa wamehusika hata kwa kufanya uzembe kidogo serikali haiwezi kukubali, bali lazima wasimamishwe kazi mara moja.

Hivyo alisema Injinia Mfinanga na Kapteni Sadik Muze aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji, lazima wachukue dhamana.

Kwenye ununuzi wa ndege, alisema ni jambo kubwa na kuwa serikali inalisimamia kwa nguvu zote.

"Tunataka kununua ndege mbili ambapo manunuzi yameishaanza kufanyika, na tumeishapeleka malipo ya awali dola za Marekani milioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa ndege hizo," alisisitiza.

Profesa Mbarawa alisema  wanategemea ndege hizo zitaingia nchini Septemba 14, mwaka huu na katika kuzileta kuna mambo mengi yanatakiwa kufanyika.

No comments:

Post a Comment