Tuesday 9 August 2016

SAMIA: MAFISADI, WALA RUSHWA HAWANA NAFASI


Na Mwandishi Maalumu, Lindi

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Watanzania kuwa serikali ya awamu ya tano inayo dhamira ya dhati ya kuwapatia huduma bora za kijamii kwa kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Aidha, Samia amesema serikali itaendelea kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa kodi ili fedha zinazokusanywa zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.

Makamu wa Rais alisema hayo jana, kwenye kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya Nanenane, ambayo kitaifa yalifanyikwa kwenye uwanja wa Ngongo, ulioko katika Manispaa ya Lindi.

Katika hutoba yake kwa mamia ya wananchi waliofurika katika viwanja hivyo, Makamu wa Rais alisema azma ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo itatimia iwapo tu wananchi wataunga mkono jitihada za serikali katika kulipa kodi kwa wakati, kudai risiti, kufanya kazi kwa bidii na kukemea vitendo vya rushwa.

“Napenda kuwahakikishia kuwa, tunayo dhamira ya dhati ya kuendelea kuwatumikia na kuwaboreshea huduma zote za kijamii pamoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla bila kujali mikoa mnayotoka, jinsia, dini au itikadi za vyama vyenu,”alisisitiza.

Akizungumzia uimarishaji wa shughuli za kilimo nchini, Makamu wa Rais alisema maadhimisho ya sikukuu ya Nanenane ni moja kati ya juhudi  za serikali za kuboresha shughuli za kiuchumi, ambapo asilimia 75 ya wananchi wanajihusisha na shughuli za kilimo,mifugo na uvuvi kote nchini.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuzipa kipaumbele sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na kuongeza bajeti katika sekta hizo ili ziweze kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza pato la taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Makamu wa Rais alisema serikali imeweka mikakati na mipango inayolenga kusaidia uimarishaji wa shughuli za kilimo kote nchini, kwa kuongeza matrekta makubwa na madogo kutoka 7,491, mwaka 2005/2006 hadi 16,478, kwa mwaka wa fedha 2016/2017, hivyo kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 70 hadi asilimia 12.

Aidha, alisema serikali imeongeza idadi ya maofisa ugani katika kilimo kutoka 3,379, mwaka 2005 hadi 2006 hadi 8,756, mwaka 2015/2016.

Pia alisema serikali imefufua mashamba ya mbegu kwa kuhusisha sekta binafsi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa katika kuzalisha mbegu bora za mazao ya chakula nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliwahimiza wananchi kote nchini, kulipa kodi ipasavyo ili fedha zitakazopatikana zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliwataka wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara, ambayo watauza ndani na nje ya nchi katika hatua ya kukuza pato la familia na taifa kwa ujumla.

MAJALIWA: WALIOHUJUMU USHIRIKA WASHUGHULIKIWE

Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu, Solomon Mwansele ameripoti kutoka Mbeya kuwa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inafufua sekta ya ushirika na kuwachukulia hatua kali watendaji wote waliohujumu ushirika na kusababisha machungu kwa wanaushirika ili iwe fundisho kwa wengine.

Waziri Mkuu alisema mkulima, mfugaji na mvuvi mdogo au mmoja mmoja, hawezi kupunguza umaskini bila ya kuwa na chombo cha kuwaunganisha na kuwapa nguvu ya kutetea bei ya mazao yao.

Aidha, alisema ushirika imara utawasaidia kutafuta soko na kupata mikopo ya riba nafuu.

Waziri Mkuu, Majaliwa alisema hayo jana, wakati akifunga rasmi Maonesho ya Nanenane mwaka huu, kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwenye viwanja vya John Mwakangale, vilivyoko mjini Mbeya.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, pamoja na umuhimu wa kuwepo kwa ushirika, tasnia hiyo imewaumiza wakulima wengi na kuwafanya kukata tamaa katika uzalishaji, kutokana na usimamizi mbovu, ubadhirifu na ubabe wa baadhi ya viongozi wa ushirika.

“Wahimizeni na kuwashawishi wakulima, wafugaji na wavuvi kujiunga  katika vikundi vya ushirika vya uzalishaji na SACCOS. Aidha, elimu ya ushirika inayotolewa kwenye maonyesho ya mwaka huu, iwe changamoto kwenu kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,” alisema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali haitamvumilia mfugaji anayelisha katika maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuendelea kuyalinda maeneo hayo.

Aidha, alisema ameridhishwa na jitihada zinazoendelea kufanywa na wakulima wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, katika kuinua kiwango cha utaalamu na teknolojia inayotumika, hasa katika uzalishaji wa mazao, uvuvi na mifugo.

Amesema kutokana na utaalamu aliouona kwenye mabanda aliyoyatembelea, hana shaka kuwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi kwa ujumla watakuwa wamepata mafunzo stahiki na elimu muhimu katika kuboresha sekta hizo.

“Nitumie nafasi hii kwenu kutoa wito kwa wazalishaji wote kwa bidhaa mbalimbali, zikiwemo za mifugo na kilimo, kuweza kutumia vizuri utalaamu na teknolojia hizi, mnaporudi kwenye maeneo yenu,” alisema Majaliwa.

Aliongeza kuwa wafanye hivyo ili kujiongezea tija na kipato, lakini pia kuboresha hali ya kimaisha. Alisema ni mategemeo yake kuwa watakuwa chachu ya maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi kwenye maeneo wanayotoka.

Alisema wakulima, wafugaji na wavuvi, wamepata tija kwa kuwa wataalamu wameweza kuwaeleza hatua mbalimbali za kufikia kwenye maendeleo.

“Lakini vilevile wataalamu wataendeleza kazi hiyo, kutoa maelezo hayo siku nzima ya leo kabla hawajaondoa vifaa vyao hapa uwanjani, hivyo ni vyema kwa wale, ambao hamjapata nafasi, muende kumalizia kupata maelezo sahihi ya kitaalamu kutoka kwa watalaamu waliopo,” alisema Majaliwa.

Aliwataka wakulima wa kanda hiyo kuendelea kuboresha kilimo kwa kuzingatia maelekezo ya watalaamu na kutoa mfano wa banda la Magereza, ambako alikuta vipando mbalimbali, ambavyo vimeonyesha utalaamu mkubwa na mabadiliko makubwa ya uboreshaji kilimo.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema Magereza wametumia eneo dogo la robo eka kwa kupanda mazao ya alizeti, mboga mboga na kuzalisha kiwango kikubwa cha mazao, ikilinganishwa na kilimo, ambacho wakulima wamekuwa wakipanda mahindi kwenye ekari moja, wanavuna magunia saba.

Wakati huo huo, serikali imesema licha ya mikoa ya Kanda ya Nyanda Juu Kusini kuongoza kwa uzalishaji wa kilimo nchini, lakini inakabiliwa na udumavu wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, kwa zaidi ya asilimia 40.

Imeelezwa kuwa hali hiyo ya afya inakinzana kabisa na ukweli kwamba, mikoa hiyo ndiyo wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema hayo jana, wakati akifunga maonyesho ya wakulima, kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwenye viwanja vya John Mwakangale mjini Mbeya.

“Ni matumaini yangu kuwa maonyesho haya yatakuwa chachu ya kuelimisha jamii kuhusu masuala ya lishe na nilipopita kwenye mabanda, nimekuta vyakula mbalimbali vimesagwa kwa ubora, ambao unaweza ukaleta tija kwa vijana wetu na watoto wetu wa chini ya miaka mitano,” alisema.

Aidha, Majaliwa alisema licha ya Tanzania kujaliwa kuwa na bahari, maziwa na mito, rasilimali hizo hazijaweza kutumiwa kikamilifu kutokana na changamoto mbalimbali.

Alisema moja ya changamoto hizo ni uvuvi haramu, unaoharibu mazalia ya samaki, matokeo hasi ya mabadiriko ya tabia nchi, ikiwemo ongezeko la joto duniani, zana duni za uvuvi na kuongezeka kwa ushindani katika soko la dunia la samaki.

“Wavuvi wamekuwa wanakosa maarifa ya teknolojia ya kisasa, hivyo ili kutatua changamoto za uvuvi na kuwawezeha wavuvi kuongeza tija na kukuza uchumi wa kitaifa, serikali imeandaa mpango mkakati wa Taifa kwa maendeleo ya kilimo, kupitia ufugaji wa samaki,” alisema Majaliwa.

No comments:

Post a Comment