Tuesday 9 August 2016

MAJALIWA AWASHUKIA MAOFISA WAVURUGAJI TRA NA UHAMIAJI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, imeitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuimarisha kitengo cha tathmini ili kuweka viwango halali, ambavyo havitawakandamiza wafanyabiashara.

Pia, ameagiza kuwepo kwa uwazi kuhusu viwango stahili vya kodi wanavyotakiwa kulipa wafanyabiashara ili kila mmoja atambue stahili yake.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi, alipozungumza na viongozi wa mikoa ya Mbeya, Katavi, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Iringa na Njombe, baada ya kuwasili mkoani Mbeya, kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Maonyesho ya Nanenane kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, yaliyofanyika jana mkoani Mbeya.

"TRA waendelee kukusanya mapato vizuri, ila kuna wakusanya kodi wanaotaka kuharibu mkakati wa serikali kwa kufanya mambo ya hovyo, ikiwemo kuwaongezea wafanyabiashara viwango vikubwa vya kodi zaidi ya ile wanayostahili.

"Jambo hilo limefanya suala la kodi liwe ni kama tatizo au adhabu, kitu ambacho sio sahihi. Naagiza watendaji wa TRA wanaofanya hivyo, wasakwe na wachukuliwe hatua

‘‘Wafanyabiashara mnaoonewa kwa chuki binafsi na watendaji wa TRA, toeni taarifa ili muweze kufanya biashara zenu kwa uhakika bila ya wasiwasi. Lengo ni kukufanyeni muweze kulipa kodi sahihi kwa mujibu wa sheria,“alisema.

Ili kufanikisha mpango huo, Waziri Mkuu aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya, kuwasikiliza wafanyabiashara wenye malalamiko ya kweli ya kutotendewa haki katika kutozwa kodi kwa sababu mchango kupitia kodi ni kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa taifa.

Katika hatua nyingine, Majaliwa aliitaka Idara ya Uhamiaji kuwadhibiti watumishi wasio waaminifu, ambao wamekuwa wakichukua rushwa kutoka kwa raia wa nje ili kuwaingiza nchini bila ya kuwa na vibali maalumu.

"Ni lazima tuhakikishe hakuna uingiaji holela wa wageni, hususan wasio na vibali maalumu kwani bila ya kudhibiti suala hilo, tunaweza kutoa mwanya kwa wabaya wetu wasio na nia njema na taifa. Watu watakaobainika wameingia nchini bila ya vibali, wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria,“alisema.

Alisema mipaka kushindwa kudhibitiwa na kuruhusu uingiaji wageni bila vibali, kunasababisha serikali kushindwa kuteleza ipasavyo mipango yake ya kuwahudumia wananchi kulingana na idadi halisi.

Mbali na Idara ya Uhamiaji, pia Waziri Mkuu alisema wakuu wa mikoa ya mipakani wana jukumu la ziada la kuhakikisha wanadhibiti mipaka yote na kuhakikisha hakuna watu wanaoingia nchini bila ya kuwa na vibali.

Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa mikoa yote kuendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika maeneo yao na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu ili Watanzania waweze kutekeleza shughuli zao za maendeleo kama walivyojipangia.

“Natambua kuwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yenu, endeleeni kuimarisha hali ya ulinzi na usalama. Nchi hii tunahitaji iwe tulivu na salama na ni wajibu wenu kuhakikisha kwamba lolote linalotokea mnalikabili vilivyo,“alisema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, alipokuwa akisoma taarifa kwa Waziri Mkuu, alisema mkoa wake una jumla ya viwanda 1,653, kati ya hivyo vikubwa ni tisa, vya kati 19 na vidogo 1,625  na bado wanaendelea kuzisimamia halmashauri kutenga maeneo zaidi kwa ajili ya kuongeza na kupanua viwanda.

Makalla alisema katika eneo hilo la viwanda, mkoa una kiwanda kimoja cha kusindika nyama cha Tanganyika Pachers, kilichoko wilayani Mbeya, ambacho hakijawahi kufanya kazi tangu kilipojengwa na kufungwa mitambo mwaka 1975.

Alisema usimamizi wa kiwanda hicho uko chini ya Masajili wa Hazina na kwamba, tayari kuna muwekezaji amepatikana kwa ajili ya kukiendesha, hivyo ameiomba serikali kuharakisha taratibu za mikataba ili kiweze kuanza kufanya kazi.

No comments:

Post a Comment