Tuesday 9 August 2016

VIGOGO WAWILI TANESCO WATUMBULIWA

NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, amewasimamisha kazi maneneja wawili wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), waliokuwa kwenye kituo cha kupooza umeme cha Kurasini.

Kalemani alifikia hatua ya 'kuwatumbua majipu' vigogo hao, Dar es Salaam, juzi,  kwa kosa la kutosimamia ipasavyo majukumu yao pamoja na uzembe.

Aidha, alimuagiza Msimamizi Mkuu wa Mradi wa TEDAP, Emmanuel Manirabona, kuweka mameneja wapya kituoni hapo haraka iwezekanavyo ili wananchi wasipate kero za huduma ya umeme.

Dk. Kalemani alichukua uamuzi huo, wakati wa ziara ya kushtukiza kukaguavituo vitano vya kupooza umeme pamoja na njia kuu ya kusafirisha umeme wa msogo wa kilovoti 132, ulioanza kujengwa mwaka 2012 na kutarajiwa kukamilika mwaka 2013, jijini  hapa.

"Mradi huu ulianza 2012 na ulitakiwa kukamilika mwaka 2013, ikiwa ni ndani ya miezi 18 tu, lakini hadi sasa ni zaidi ya miaka minne bado haujakamilika. Hii haikubaliki hata kidogo, hatuwezi kuwa na miradi isiyokwisha. Inaonekana kuna uzembe mkubwa hapa,"alisema Dk. Kalemani.

Alisema ujenzi wa kituo hicho umetekelezwa kwa asilimia 5, tofauti na vituo vingine.

Pamoja na hatua hiyo, waziri huyo pia aliwataka makandarasi wanaotekeleza mradi mkubwa wa umeme wa TEDAP kwa jiji la Dar es Salaam, kukamilisha mwishoni mwa Septemba, mwaka huu, ili jiji liwe na umeme wa kutosha na wa uhakika.

Alifafanua kuwa serikali haiwezi kufanya kazi na mikataba ya makandarasi isiyokwisha kwa wakati, hivyo aliiagiza TANESCO kuangalia upya mikataba ya makandarasi wote nchini wanaotekeleza miradi ya umeme na kuchukua hatua ama kuihuisha au kuifuta.

Aidha, aliwataka makandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi wa kituo cha Kurasini, kurejea katika eneo la kazi.

Aliongeza kuwa katika vituo vya kupoza umeme vya Gongolamboto, Mbagala na Kipawa, kazi kubwa iliyobaki ni kuvuta nyaya na kuunganishwa katika njia kuu ya umeme, hivyo makandarasi hao wahakikishe wanamaliza kazi hiyo kwa wakati.

Alitoa rai kwa wafanyakazi wa  TANESCO nchi nzima kutoka maofisini na kufuata wateja ili kuwapatia huduma bora.

No comments:

Post a Comment