Wednesday, 3 August 2016

OLE SENDEKA AWANANGA VIONGOZI WA CHADEMA





MSEMAJI Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, amewananga viongozi wa CHADEMA na kuwaita wapinga operesheni ya kupambana na mafisadi inayoendeshwa na Rais Dk. John Magufuli, ndiyo maana walikimbia muswada wa kupitisha sheria ya uanzishwaji wa Mahakama Maalumu ya Mafisadi na kuamua kuziba midomo kwa makaratasi.

Aidha, amewananga kwa kupotosha ukweli wa agizo la Rais Magufuli la kuzuia mikutano ya kisiasa nchini, ili kupisha shughuli za maendeleo na kwamba, kwa hili hawatafanikiwa kwa kuwa wananchi wamemuelewa vizuri kiongozi wao kuhusu katazo hilo.

Sendeka alisema hayo jana, alipokuwa akizungumza katika harambee ya kuchangia fedha kikundi cha Enaboishu cha Wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Longido.

Alisema binafsi hawashangai viongozi hao kutokana na harakati zao hizo kwa kuwa wameshaona jitihada zao pamoja na malengo yao kamwe hawatayafikia kutokana uchapakazi wa Rais Magufuli katika kipindi kifupi cha uongozi wake.

Alisema nia ya kuikwamisha serikali ya Rais Magufuli ilianza kuonekana mapema kuanzia pale walipoanza kususia vikao vya bunge lililomalizika, kwa kisingizio cha kunyimwa demokrasia, jambo ambalo sio la kweli, bali waliukimbia muswada wa kuwashughulikia mafisadi.

Alisema hilo la kuziba midomo na kukataa kabisa kuzungumzia kuhusu kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi, hawakulifanya kwa bahati mbaya, bali walilifanya kutokana na kutambua kuwa watu wanaotarajiwa kushughulikiwa kwa ufisadi  wamo ndani ya chama chao baada ya kuwapokea.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe, aliwapongeza wanawake wa kikundi hicho kwa kuchagua maendeleo badala ya vurugu za kisiasa, ikiwemo kushabikia maendeleo na kuamua kuitisha harambee hiyo.

Alisema katika mkoa wa Arusha, vijana wamechoshwa na vurugu hizo na wameamua kuchagua maendeleo na kwamba, wamewataka viongozi wa CHADEMA kutanguliza familia zao katika maandamano siku hiyo ya Septemba Mosi, kama ilivyosisitizwa na Rais Magufuli na siyo watoto wa masikini.

Mdoe alisema kauli ya upotoshaji kwamba Rais Magufuli kazuia shughuli za wanasiasa sio ya kweli kwani wanaruhusiwa kufanya mikutano yao na wananchi wao katika majimbo na kata zao, lakini sio kwenda katika majimbo mengine kufanya mikutano na kuwahamasisha wananchi kuichukia serikali yao.

Katika harambee hiyo, jumla ya sh. milioni 25, zilipatikana zikiwa fedha taslimu sh. milioni  8.9, ahadi pamoja na mifugo kama ng’ombe mmoja, mbuzi wanne, kondoo wanne pamoja na saruji mifuko 100.

No comments:

Post a Comment