Sunday 25 September 2016

MWALIMU NYERERE AENZIWE KWA VITENDO- KAILIMA



Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani (Kushoto) akisalimiana na Msemaji Mkuu na kiongozi wa familia ya Baba wa Taifa Chifu Japhet Wanzagi (kulia) mara baada ya kuwasili eneo la Mwitongo wilayani Butiama. Wa Pili kutoka Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Butiama Bi. Annarose Nyamubi.

Na. Aron Msigwa – NEC, Musoma.
 
Viongozi wa vyama vya Siasa wametakiwa kuiga kwa vitendo uzalendo na moyo wa kujitoa  aliokuwa nao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake  ili kuliwezesha Taifa kupiga hatua kimaendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani  mara baada  kutembelea Kaburi na Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo wilayani Butiama.

Amesema kuwa kumbukumbu za Baba wa Taifa zilizohifadhiwa vizuri katika makumbusho hiyo zina mambo mengi ya kujifunza ambayo wanasiasa wanatakiwa kuyafanya kwa  vitendo hasa  uzalendo kwa nchi, uvumilivu, upendo  na moyo wa kujitoa kwa dhati kuwatumikia wananchi.

“Kupitia kumbukumbu hizi sisi watumishi wa Tume tumejifunza ukomavu wa demokrasia aliokuwa nao Mwalimu Nyerere akiwa ndani na nje ya Bara la Afrika,  wengi wanadhani Demokrasia ni wakati wa uchaguzi tu, kumbe demokrasia ni pamoja na kuheshimu watu wengine” Amesema Kailima.

Ameeleza kuwa maisha aliyoishi Baba wa Taifa ni mfano wa kuigwa na viongozi na watanzania wote hasa pale alipojitofautisha na viongozi wengi wa Bara la Afrika alipoepuka tamaa ya madaraka na mali kwa  manufaa ya taifa.

“Sote ni mashahidi kupitia kumbukumbu zake tumeona mahali alipokuwa anaishi mwalimu Nyerere kabla hajajengewa nyumba na Jeshi, kama Rais mstaafu wengi walitegemea asingeishi katika  eneo lile, kumbukumbu hii nzuri aliyoiacha inatufundisha watanzania kuwa mwalimu aliitanguliza Tanzania mbele kuliko maslahi yake binafsi” Amesisitiza Kailima.

Bw. Kailima amebainisha kuwa  NEC itaendelea  kumuemzi Baba wa Taifa kwa yale aliyoyafanya
na kuyasimamia kwa manufaa ya taifa huku akitoa wito kwa  viongozi wa vyama vya Siasa wawe na kiasi na waridhike na vile walivyonavyo.

“Suala la kuridhika na kuwa na kiasi linapaswa kuzingatiwa, wanasiasa  wanapaswa kuwaheshimu wananchi wanaowachagua kupitia chaguzi mbalimbali,  matokeo yanapotoka kama ni sahihi basi wanasiasa wakubaliane na maamuzi yao”  Ameainisha Kailima. 

Kwa upande wake Mhifadhi wa Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Bw. Jacob Thomas amesema kuwa  watanzania wanayo mengi ya kujifunza kupitia vitu alivyoviacha Baba wa Taifa ambavyo vimehifadhiwa katika Makumbusho hiyo.

Amesema kuwa maisha ya uadilifu aliyoishi enzi za uhai wake na mchango wake katika kuiletea
maendeleo Tanzania na Bara la Afrika vinapaswa kuenziwa kwa nguvu zote na viongozi wa Tanzania.

“Ninyi mliopata nafasi ya kuitembelea makumbusho hii mmejifunza vitu vingi kumhusu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba alikuwa ni mtu wa namna gani kwa viwango vya Afrika na dunia kutokana na kumbukumbu ya uadilifu aliyoiacha ndani na nje ya mipaka ya Tanzania”

No comments:

Post a Comment