Sunday, 25 September 2016

SERIKALI YA ZANZIBAR YAOKOA SHILINGI BILIONI 9.7 ZA MATIBABU

 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeokoa kiasi cha Tsh. Bilioni 9.7 kutokana na upasuaji wa maradhi ya mishipa ya fahamu, uti wa mgongo na vichwa maji uliofanywa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja tokea kuanzishwa kwa huduma hizo miaka miwili iliyopita.

Hayo yalielezwa leo Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo yaliofanywa kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Taasisi ya Maendeleo ya Elimu inayohusiana na upasuaji wa Mishipa ya Fahamu, Uti wa mgongo na Vichwa maji (NED) Dk. Jose Picer akiwa na Makamo wa Rais wa Taasisi hiyo Dk. Mahmood Quiresh.

Katika mazungumzo hayo ambapo Madaktari hao bingwa walikuwa wameongozana na uongozi wa Wizara ya Afya chini ya Waziri wa Wizara hiyo  Mahmoud Thabit Kombo, ambao walipongeza mashirikiano makubwa wanayoyapata katika kutekeleza shughuli zao hapa nchini.

Pamoja na hayo, madaktari hao walieleza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa yaliopatikana kutoka kwa Taasisi hiyo ni pamoja na kufanya upasuaji huo kwa wananchi wa Zanzibar wapatao 500 wakiwemo watoto, wanawake na watu wazima.

Madaktari hao walimueleza Dk. Shein kuwa gharama hizo ni kwa ajili ya taaluma na upasuaji mbali na gharama nyengine ambazo Serikali ingeweza kutumia katika usafirishaji, gharama za malazi na chakula kwa wagonjwa na wauguzi wao pale wanapowasafirisha kwenda nje ya nchi.

Kwa upande wake Dk. Jose Picer alitoa pongezi na shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa juhudi zinazochukuliwa katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi wa Zanzibar zikiwemo huduma za afya.

Dk. Picer alieleza kuwa juhudi hizo ni za kupongezwa kwani zimeweka kuokoa maisha ya wananchi walio wengi sambamba na kuokoa fedha nyingi za umma ambazo zingelitumika kuwapeleka wagonjwa hao nje ya nchi.

Nae Dk. Mahmoud Qureshi alimueleza Dk. Shein kuwa mafanikio hayo yote yaliopatikana katika sekta hiyo ya afya yanatokana na amani na utulivu mkubwa uliopo hapa Zanzibar kwani bila ya mambo hayo muhimu mafanikio ya upasuaji huo yasengeweza kufanyika.

Dk. Quresh alieleza kuwa kutokana na umuhimu mkubwa wa maendeleo ya taasisi hiyo kuna kila sababu ya kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu ambao watasaidia kufanya upasuaji huo huku akiahidi kuwa Taasisi ya NED itaendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa madaktari hao pamoja na taasisi hiyo kwa juhudi zao za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha na kuiendeleza sekta ya afya hapa nchini .

Dk. Shein alipongeza juhudi zilizofanywa na viongozi hao wa NED katika kuhakikisha jengo la Taasisi ya mishipa ya fahamu, uti wa mgongo na vichwa maji linajengwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja na kukiri kuwa kabla ya kuwepo kwa huduma hizo hapa nchini fedha nyingi zilikuwa zikitumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha Hospitali ya Mnazi Mmoja inarejesha hadhi yake iliokuwepo hapo siku za nyuma kutokana na huduma mbali mbali muhimu zilizokuwa zikitolewa pamoja na kuwa na madaktari bingwa waliobobea katika fani mbali mbali.

Alisema kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika kutoa huduma za afya historia ambayo ilikuwa kabla ya Mapinduzi na kuimarishwa zaidi baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Dk. Shein alieleza kuwa licha ya kuwepo changamoto mbali mbali zikiwemo ongezeko la idadi ya watu hapa Zanzibar ikilinganishwa na idadi iliyopo kabda ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 bado Serikali imekuwa ikichukua juhudi kubwa katika kuimarisha sekta ya afya.

Sambamba na hayo Dk. Shein alieleza haja ya kuimarishwa mafunzo kwa madaktari wazalendo hasa katika kada hiyo huku akieleza kuwa nchi nyingi wahisani na mashirika yasio ya kiserikali yamekuwa yakivutiwa kuisaidia Zanzibar kutokana na amani, utulivu na upendo uliopo hapa nchini.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment