Monday 31 October 2016

MTOTO WA KIGOGO AHUKUMIWA KULIPA FAINI MILIONI 138.3


Na Furaha Omary

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, imemhukumu Pirmohamed Mulla, kulipa faini ya sh. milioni 138.3, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumiliki nyara mbalimbali za serikali kinyume na sheria.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Michael Mteite, alimpa mshitakiwa huyo adhabu hiyo, baada ya kukiri kosa hilo la kukutwa na nyara hizo zenye thamani ya sh. 13,839,000, aliposomewa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Oktoba 27, mwaka huu.

“Mahakama inakutia hatiani, hivyo inakupa adhabu ya kulipa mara 10 ya thamani ya nyara (sh. 138,390,000) au kifungo cha miaka 20 gerezani,” alisema hakimu huyo.

Baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mshitakiwa huyo aliweza kulipa faini hiyo kupitia risiti ya malipo ya serikali namba 8870022.

Aidha, mahakama ilitaifisha nyara hizo na kuamuru ziwekwe chini ya himaya ya Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mshitakiwa huyo aliomba huruma ya mahakama kwa madai kwamba, ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana umri mdogo wa miaka 25.

Kwa upande wao, Mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na Abel Kihaka, waliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwake na wengine, kwa sababu  makosa ya uhujumu uchumi yanayohusiana na nyara za serikali ni makubwa na yanaathari kwa kizazi cha sasa na kijacho na uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa jamhuri, Mulla  alikamatwa nyumbani kwake huko Ubaruku Highland Estates, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, na maofisa wa Kikosi Dhidi ya Ujangili na Jeshi la Polisi, baada ya kupatikana kwa taarifa za kiintelijensia kuwa anajihusisha na nyara za serikali kinyume na sheria.

Inadaiwa usiku wa Oktoba 24, mwaka huu, maofisa hao baada ya kufika nyumbani kwa mshitakiwa, walifanya upekuzi na kukuta nyara mbalimbali za serikali, ikiwa ni kilo 46 za nyama ya Tandala, Mbawala, Swalapala, Tohe, Njiwa Poro, Kangapori na pembe za Tandala na Tohe, ambazo zina  thamani ya sh. 13,839,000.

No comments:

Post a Comment