Thursday 3 November 2016

KIAMA CHA WAFANYAKAZI SHIRIKA LA POSTA CHAJA


BODI mpya ya Shirika la Posta Tanzania, imesema itahakikisha inaondoa madudu yote yanayolifanya shirika hilo lisiende mbele.

Imesema wapo baadhi ya wafanyakazi wanajinufaisha binafsi kwa kutumia rasilimali za shirika hilo, ambapo imewatangazia kiama na kusema watakuwa wa kwanza kuondolewa ili shirika lisonge.

Akizungumza na uongozi jana, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, Haruni Kondo, alisema atahakikisha bodi hiyo inakwenda sawa na serikali ya awamu ya tano katika kuondoa madudu yote yanayolifanya shirika lidorole.

Alisema huu siyo wakati wa kuongelea siasa, kinachotakiwa ni kufanya maendeleo kwa kuwa siasa zimehubiriwa kwa muda mrefu na kwamba, kilichobaki ni kuonyesha vitendo kwa ajili ya maendeleo ya shirika.

Pia, alisema wafanyakazi wa Posta pamoja na bodi yote wanatakiwa kubadilika na kuhakikisha wanaondoa kasoro za sasa, ikiwemo urasimu ambao unasababisha kutokuwepo kwa maendeleo.

“Shirika la Posta linazo rasilimali nyingi, ambazo zinaliwa na wajanja wachache wasiopenda maendeleo ya shirika,"alisema.

Mwenyekiti huyo alisema hivi sasa wana mpango wa kukaa pamoja na kuangalia wafanyakazi hewa ndani ya shirika hilo, kwa kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazosababisha lidumae.

“Tutaanza kupekua vyeti vya kila mfanyakazi, tukimbaini asiyetufaa, tutamuondoa ili asiwe analipwa mshahara wa bure,”alisema.

Aliongeza kuwa, atahakikisha mikataba yote ndani ya shirika hilo inapitiwa upya ili kuiondoa ile ambayo haina manufaa na maslahi kwa taifa.

Aliwataka wajumbe wa bodi hiyo pamoja na wafanyakazi wa shirika hilo, kutoshiriki vitendo vya ubadhirifu ili kuliongezea kasi ya maendeleo na kufikia malengo uanayotarajiwa.

No comments:

Post a Comment