Wednesday 16 November 2016

MAJALIWA AICHARUKIA TANESCO

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameliagiza Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), kuhakikisha linaendelea kutoa umeme wa uhakika kwa wananchi ili azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa nchi ya kipato cha kati kwa uchumi wa viwanda, itekelezwe kwa vitendo.

Alisema sifa kuu ya serikali makini ni kutekeleza ahadi inazozitoa, jambo linalofanywa na serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo ya nishati.

Majaliwa alisema kazi zinazofanywa na TANESCO kwa wakati huu, zinaakisi utekelezaji wa ahadi, ambayo serikali imeitoa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, kuwa itafikisha huduma za umeme wa uhakika kwa Watanzania wakiwemo wa vijijini.

Pia, alisema ili kuliwezesha shirika kutekeleza majukumu yake, serikali imetenga sh. trilioni moja, kwenye bajeti yake ili kuhudumia usambazaji wa umeme nafuu, ambapo kupitia mradi wa REA, jumla ya vijiji 8,000 vitafikiwa.

Kwa mantiki hiyo, alibainisha kuwa malengo ya serikali ya kuwafikishia huduma ya umeme wa uhakika asilimia 75 ya wananchi ifikapo mwaka 2025, yatafikiwa kwa uhakika kutokana na unafuu wa gharama ya kuunganisha umeme, ambayo ni sh. 27,000 pekee.

Waziri Mkuu alizungumza hayo jana, jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi mkubwa wa kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme mkoani humo, ambao umetekelezwa kwa ushirikiano wa serikali za Tanzania na Finland kwa gharama ya takriban sh. bilioni 74.6.

Katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda na Biashara za Kimataifa wa Finland, Kai Mykkanen, jijini Dar es Salaam, mkoa wa Dar es Salaam, ulihakikishiwa kuwa na umeme wa uhakika kutokana na teknolojia iliyotumiwa na TANESCO kuendesha mitambo yake.

Mfano wa teknolojia hiyo ni iliyotumiwa kwenye mradi huo, ambao  kukamilika kwake kunamaanisha upatikanaji wa umeme bila usumbufu wa mgawo na kukatika kusiko na mpangilio, kutokana na uwezo wa vifaa kutambua haraka sehemu yenye hitilafu kabla wateja hawajatoa taarifa.

Utekelezaji wa mradi huo, ambao Waziri Mkuu ameshauri ujengwe kwenye miji mingine nchini, ikiwemo Arusha, Mbeya, Mwanza na Dodoma, unajumuisha ujenzi wa sehemu nne, ikiwemo kituo cha kupoza umeme cha KV 132 na ujenzi wa kituo cha udhibiti wa mfumo wa usambazaji umeme (SCADA).

Pamoja na hizo, pia ujenzi wa njia ya umeme chini ya ardhi kwa ajili ya kuunganishia vituo vya Kariakoo, Railway, Sokoine, eneo la katikati ya mji na ujenzi wa mfumo wa njia ya usafirishaji umeme chini ya ardhi kwa msongo wa kV 132, kutoka Makumbusho hadi Jangwani Sekondari.

Akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo kwa niaba ya Rais, Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa alisema ni mafanikio kwa serikali kufanikisha mradi huo, ambao utaendelea kuifanya Dar es Salaam kuwa kitovu cha biashara na viwanda nchini.

Alisema serikali haitarajii kukatika kwa umeme mara mradi huo utakapoanza kufanya kazi, kama ambavyo TANESCO kwa kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake, Feschesm Mramba ameahidi kwenye hafla hiyo.

Waziri Majaliwa alisema umeme ni mhimili wa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla, hivyo wakati serikali ikihimiza uanzishwaji wa viwanda, ni wajibu wa TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo.

Alitumia fursa hiyo pia kuwataka Watanzania kuwekeza kwenye viwanda katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, kwa sababu TANESCO wana uwezo wa kuhudumia kiasi chochote cha umeme kinachohitajiwa na kiwanda chochote nchini.

Hata hivyo, alitoa rai kwa wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini, kutumia nafasi zao kama wenyeviti wa kamati za ulinzi, kusimamia na kuilinda miundombinu ya umeme wa TANESCO kwa sababu serikali inatoa fedha nyingi kuijenga.

"Ninaagiza Ma-RC na Ma-DC nchi nzima, simamieni miundombinu ya TANESCO, serikali inatumia fedha nyingi kuijenga, mtakayembaini anahujumu, mkamateni mumfikishe kwenye vyombo vya sheria," alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara wa Finland, Mykkanen, alisema ushirikiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo, ndio uliosababisha nchi yake kuona umuhimu wa kusaidia Tanzania kwenye upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kuanzia na mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema kwenye malengo yao kama serikali ya Finland, walikubaliana kuwa kila mradi uwe na matokeo chanya, jambo ambalo limeonekana kwenye mradi huo wa TANESCO, hivyo wanayo furaha kubwa.

Waziri huyo alisema kwa mradi huo, ambao pia umejengwa na kampuni za Finland, utaondoa kero za kukatika kwa umeme mara kwa mara, hivyo uzalishaji utaongezeka kwenye maeneo mengi ya nchi.

Alisema umeme kuwa uti wa mgongo wa maendeleo ni jambo lisilofichika na kwamba Finland, wana maendeleo makubwa kutokana na kuwekeza kwa muda mrefu kwenye vyanzo vya nishati, ikiwemo maji, upepo na nishati jua.

Pamoja na hilo, waziri huyo aliyeambatana na Balozi wa Finland hapa nchini, alibainisha kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania kutatua changamoto za nishati ili ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia sekta ya viwanda yawe dhahiri.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba, akitoa taarifa ya mradi huo, alisema umeanzishwa kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo alisema mbali ya mradi huo, ipo mingine yenye lengo kama hilo ndani ya Dar es Salaam na mikoani, ukiwemo wa TEDAP, unaotekelezwa kwenye maeneo ya Gongo la Mboto na Kipawa, Kurasini, Chang'ombe na Mbagala.

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni Ubungo, Mburahati, Uwanja wa Ndege wa KIA -  Kilimanjaro, Viwandani - Dar es Salaam na Njiro - Arusha.

No comments:

Post a Comment