Tuesday 15 November 2016

WADAIWA SUGU MIKOPO YA ELIMU YA JUU KUFIKISHWA KORTINI


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema inatarajia kuwafikisha mahakamani wadaiwa sugu 142,470, ambao mikopo yao ilikwishaiva.

Wadaiwa hao ni waliokopa kuanzia tangu mwaka 1994-1995 hadi Juni mwaka huu, ambapo walikopa sh. 239,353,750,176. 27.

Akizungumza mjini Dar es Saalam, jana, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru, alisema kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2004, iliyoanzisha bodi hiyo, majukumu yake ni kutoa mikopo na kukusanya madeni ya fedha zilizokwishatolewa.

Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa inatoa notisi ya siku 30, kwa wadaiwa hao ili walipe kiasi chote cha madeni yao na kwamba, baada yao hapo HESLB inakamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani.

Alisema kwa mujibu wa sheria, wadaiwa hao wamevunja sheria iliyobainishwa kwenye kifungu cha sheria namba 19 A (1) ya sheria hiyo, ambapo wanatakiwa kulipa madeni na gharama za kuwatafuta na kuendesha kesi.

Badru alisema HESLB ilipoanza shughuli zake, ilirithi deni la sh. 51, 103, 685,914, ambazo ni fedha zilizokopeshwa kwa wanafunzi 48,378, kupitia kwa iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia tangu mwaka 1994 hadi Juni, 2005.

“Kuanzia Julai, 2005 hadi Juni 30,mwaka huu, bodi imetoa sh. 2, 544, 829,218,662.50, kwa wanafunzi 330,801, hivyo kufanya jumla ya fedha zilizokopeshwa tangu mwaka 1994/95 hadi 2015/2016, kuwa sh. 2,595,932,575.56 , ambapo wanafunzi wamefikia 379,179,” alisema mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi Mtendaji huyo aliongeza kuwa, kati ya mikopo yote iliyotolewa kuanzia 1994/95 mpaka Juni mwaka huu, mikopo iliyoiva ni sh.1,425,782,250,734.31, zilizotolewa kwa wanufaika 238,430.

Alisema wanufaika hao, ambao wamemaliza kipindi chao cha matazamio hadi kufikia Septemba, mwaka huu, mikupuo iliyoiva ni sh. 427,708,285,046.48.

Aidha, Badru alisema hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa na bodi hiyo ni kuwasiliana na wadhamini wa wadaiwa hao ili wawasilishe taarifa zao ama wawalipie madeni yao.

Badru alisema HESLB inaendelea kuchukua hatua ya kuwasilisha majina ya wadaiwa hao kwenye taasisi zinazotunza taarifa za ukopaji kwenye taasisi za kifedha ili kutathmni tabia zao kabla ya kukopeshwa au kuwadhamini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mikopo kutoka HESLB, Dk. Abdul Mussa Ally, alisema hali ya urejeshaji wa mikopo ni nzuri na kwamba, katika kipindi cha mwaka jana wa fedha sh. bilioni 36 zilikusanywa.

Alisema katika kipindi cha Julai hadi Oktoba, mwaka huu, HESLB ilikusanya sh. bilioni 25, pia ukusanyaji wa fedha hizo unazidi kuongezeka, ambapo kwa mwezi ilikuwa sh. bilioni mbili hadi kufikia bilioni 6.7

No comments:

Post a Comment