Thursday, 15 December 2016

WASOMI, WANASIASA WAIFAGILIA CCM

BAADHI ya wasomi na wanasiasa nchini, wamepongeza mabadiliko yaliyofanywa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli, kuwa yana lengo la kukifanya Chama kiwe cha wananchi.

Juzi, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kilichokutana chini ya Mwenyekiti wake, kilifanya mabadiliko ya uongozi
kwa kupunguza wajumbe wa NEC kutoka 388 hadi 158, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku vyeo visivyotambulika kikatiba. 

Aidha, kikao hicho kilifanya mabadiliko ya muundo na uongozi wa Chama ili kuongeza ufanisi utakaowawezesha viongozi kuwatumikia wananchi na wanachama kwa ukaribu zaidi.

Rais Dk. Magufuli alimteua Rodrick Mpogolo kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Rajab Luhwavi, ambaye ameteuliwa kuwa balozi huku Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey  Polepole, akiteuliwa kuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi.

Polepole anachukua nafasi ya Nape Nnaye, ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Rais Magufuli pia alimteua Kanali Ngemela Lubinga kuwa Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Dk. Asha Rose Migiro, ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Wakizungumza na Uhuru, jana, kwa nyakati tofauti, walimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa kuifanya CCM ionekane kuwa chama cha wananchi na siyo cha mtu mmoja.

Mwanazuoni na mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Banna, alisema Rais Magufuli amefanya mabadiliko chanya ndani ya CCM.

“Hii ndiyo CCM mpya tuliyokuwa tunaisubiria. Rais Dk. Magufuli amekifanya kiwe chama cha wananchi na siyo cha mtu mmoja,” alisema.

Alisema mabadiliko hayo yamelenga kuongeza tija na kupunguza gharama za uendeshaji wa Chama na kuifanya CCM iwe ya wananchi.

“Vilevile uteuzi alioufanya kwa watu aliowateua, wana uwezo wa kukiongoza Chama. Pia alipopunguza wingi wa wajumbe wa NEC ni jambo jema,” alisema.

Aidha, aliiomba CCM kuwavuta na kuwahamamisha vijana ili waweze kujiunga nacho.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Dk. Timothy Lyanga, alisema mabadiliko yaliyofanywa na Rais Dk. Magufuli ni ya kawaida na yana lengo la kukiimarisha Chama.

Alisema mabadiliko hayo ni kwa ajili ya  kukifanya Chama kiendelee kuwa imara.

“Ukimwangalia Polepole ni mtu makini na mwenye ushawishi kwenye jamii,”alisema Dk. Lyanga.

Alisema CCM ya sasa hivi haitaki mwanachama mmoja awe na nguvu kuliko Chama na ndiyo maana Rais Magufuli amefanya mabadiliko ya kukifanya Chama kiwe kinapendwa na kila mtu.

Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini alisema: “Cheo ni dhamana na siyo mali ya mtu.”

Alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa hatua aliyochukua ya kupunguza wajumbe wa NEC, kwa ajili ya kubana matumizi ya fedha zilizokuwa zikitumika kwenye vikao hivyo.

“Kama alivyofanya kwenye serikali pia, kwenye Chama chake ameonyesha mfano ule ule wa kubana matumizi,”alisema.

MAKADA WAPONGEZA

Makada wa CCM wamempongeza Rais Dk. Magufuli kwa kuongoza vikao vya Kamati Kuu na NEC na kufanya maamuzi mazuri.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, makada hao walisema wamefurahishwa na uteuzi uliofanywa kwenye nafasi mbalimbali pamoja na mabadiliko yaliyopitishwa.

Kapteni mstaafu George Mkuchika, alisema kwenye nafasi zote zilizojazwa, wateule ni watu sahihi na anafahamu utendaji wao barabara.

Alisema amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu kwa muda mrefu na kwamba, mabadiliko yaliyopitishwa wakati huu, anayaunga mkono kwa asilimia zote, hususan suala la kupunguza idadi ya wajumbe wa NEC.

Kapteni Mkuchika, ambaye pia ni Mbunge wa Newala Mjini, alisema lengo la CCM kuongeza idadi ya wajumbe wa NEC ngazi ya wilaya, lilikuwa ni kukisogeza Chama kwa watu, lakini wengi walitumia vibaya nafasi hizo.

"Ilitakiwa wale wajumbe wa NEC kutoka wilayani, wapeleke taarifa za vikao vikuu wilayani kwao,  lakini haikuwa hivyo, wengi walikuwa wakilenga kupata sifa za kugombea ubunge na kadhalika," alisema Mkuchika.

Alisema ni uamuzi wa busara Chama kurudi kwenye misingi yake, ambapo hata wabunge wa CCM, ambapo yeye ni mjumbe, walipendekeza wajumbe wa NEC wapunguzwe kwa kuagiza kila mkoa utoe MNEC mmoja.

"Kupunguzwa kwa ukubwa wa NEC kutafanya tupunguze matumizi yasiyo ya lazima, ukizingatia bado Chama hakina mapato mapya. Kubana matumizi ni vizuri, suala analolisimamia kidete Rais wetu Dk. Magufuli," aliongeza.

Kuhusu uteuzi wa wajumbe wa sekretarieti ya Chama, Kapteni Mkuchika alisema Naibu Katibu Mkuu, Mpogolo ni mtu makini, mwenye heshima, anayejua kutekeleza majukumu yake, hivyo hana mashaka naye kwa sababu amemfahamu tangu akiwa Makao Makuu ya Chama.

"Mpogolo ni kijana safi sana, mtaratibu ana adabu, nimemfahamu tangu nikiwa ofisi ya Makao Makuu kama Naibu Katibu Mkuu na nafasi aliyopewa ni mkuu wa watumishi wote wa Chama nchi nzima, hivyo naamini hiyo kazi ataifanya vizuri," alisema.

Kwa upande wa Kanali Lubinga, alisema ni kada wa kutupwa na kwamba ameanza kumfahamu tangu TANU Youth League.

"Kanali amefanya kazi UVCCM, serikalini kama mkuu wa wilaya na jeshini, hivyo ninaamini kabisa kwamba tumepata mtu madhubuti kwenye Chama chetu," alisema.

Kuhusu Polepole, Kapteni Mkuchika alisema ofisi ya mwenezi imepata mtu kama wanavyosema waswahili, upele umepata mkunaji.

"Polepole ni mtu anayeifahamu vizuri serikali na Chama, ninadhani ameianza mapema kazi yake kwa sababu tayari ameandika makala nyingi kwenye magazeti mbalimbali nchini. Alipokewa vizuri Newala alipokuja na Tume ya Mzee Warioba, alifafanua mambo vizuri sana, hivyo nampongeza mwenyekiti wetu kwa kuwaona watu hawa," alisema. 
   
Kwa upande wake, Mussa Sima, ambaye ni mbunge wa Singida Mjini, alisema CCM iliyopitishwa juzi na NEC, ndio iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na Watanzania.

Alisema amefurahishwa na ukurasa huo mpya uliofunguliwa ndani ya Chama, kwa kuwa unatoa nafasi kwa fikra na mtazamo mpya wa uongozi kufanya kazi na kuleta mabadiliko chanya kwa manufaa ya CCM na Watanzania kwa ujumla.

Sima alitumia fursa hiyo kumpongeza Polepole kwa kuteuliwa kukizungumzia Chama, ambapo alisema ni mtu sahihi kwa nafasi hiyo kutokana na uwepo wake wa kupambanua mambo na anajua kusimamia ukweli kwa maslahi ya taifa.

"Tumepata mjenzi wa Chama, anayesimamia uzalendo na ninaamini kabisa yeye na wenzake walioteuliwa wataipeleka CCM kwenye karne nyingine ya ushindi kwenye uchaguzi wote," alisema.

Kuhusu Naibu Katibu Mkuu, Sima alisema ni mtu anayekijua Chama na serikali, hivyo ana imani kuwa CCM itaendelea kupendwa na Watanzania wengi kuliko ilivyowahi kutokea kipindi kilichopita.

Alisema suala la kupambana na rushwa kwenye uchaguzi wa Chama ni suala la msingi, ambalo kutokana na kuwaumiza wengi ni vyema likashughulikiwa ili viongozi wanaochaguliwa wawe kweli chaguo la watu kihalali na siyo kutokana na nguvu yao ya fedha.

"Mwenyekiti wetu ameonyesha kwa vitendo kuwa haipendi rushwa, siyo serikalini pekee bali hata ndani ya Chama, hivyo tunategemea mabadiliko makubwa yenye tija kwa Chama," alisema.

Aliongeza: "CCM hii ni ya kipekee, inapendeza kwa sababu imeonyesha nia ya dhati ya kuboresha misingi yake huku ikiweka mbele maslahi ya Watanzania wote."

Kwa upande wake, Dk. Mary Mwanjelwa, alisema Kamati Kuu na Halmashauri Kuu imefanya kazi kubwa mpaka kutoa maamuzi hayo mapya kwenye Chama, hivyo kila Mtanzania anapaswa kuunga mkono mabadiliko hayo.

Dk. Hasna Mwilima, alisema anampongeza Rais Dk. Magufuli kwa kuwa tangu kukabidhiwa madaraka ndani ya Chama, Julai, mwaka huu, ameendelea na sekretarieti aliyoikuta, hivyo alipata muda wa kutafakari ni viongozi gani wanaweza kumsaidia kukiongoza Chama upande sahihi.

Alisema wateule wote anawafahamu kwa nyakati mbalimbali, ambapo Polepole amekuwa akimfahamu vyema na ni mtu anayejua kazi yake.

"Naibu Katibu Mkuu mteule nimefanya naye kazi kwenye  mkoa mmoja, akiwa Mkuu wa Wilaya ya Chato na mimi Mkuu wa Wilaya kwenye wilaya nyingine, ninafahamu uwezo wake pia ndani ya Chama mimi nikiwa Katibu Mkuu UWT Taifa, yeye alikuwa pale ofisi ya Makao Makuu, hivyo nafasi hiyo inamfaa," alisema.

Kwa upande wa Kanali Lubinga, ambaye amepewa nafasi kwenye masuala ya kimataifa, alisema anafaa ndio sababu mwenyekiti amemuona na kumteua kushika nafasi hiyo.

Pia, alisema anaunga mkono uamuzi wa Mwenyekiti, Dk. Magufuli kuendelea kumpa nafasi Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, ili kuwapa uzoefu wateule kwenye kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Chama kwa miaka mingi ijayo.

Pamoja na hayo, alisema wanachama hawapaswi kuutafsiri vibaya uamuzi wa Dk. Magufuli, kuhusu mwanachama mmoja kuwa na nafasi moja ya uongozi ndani ya Chama, kwa sababu ina mantiki kubwa kwenye uongozi.

Mbunge huyo wa jimbo la Kigoma Kusini, alitumia fursa hiyo kuwatakia kila la kheri wateule na uongozi mzima wa Chama kwa kazi iliyoko mbele yao na kwamba yuko pamoja nao.

WANASIASA WENGINE WANASEMAJE

Aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alisema mabadiliko yaliyofanywa na Rais Magufuli yataongeza ufanisi ndani ya Chama.

“Ni mabadiliko mazuri, ambayo yataongeza ufanisi na kupunguza mijadala isiyo na tija. Kama tunavyojua mahali penye wengi pana mengi yasiyokuwa na tija,” alisema.

Aliongeza kuwa mabadiliko hayo yatapunguza gharama za vikao vya Chama pamoja na posho walizokuwa wanapata wajumbe wa NEC.

Aidha, alisema uteuzi wa viongozi wapya wa chama hicho umesheheni watu makini. “Nadhani wengi tunamfahamu Polepole (Humphrey) ni kijana makini, mchambuzi na mwenye uwezo wa kujenga hoja…kwa hiyo Chama kitanufaika kupitia uwezo wake,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alisema mabadiliko hayo yamelenga kupunguza msongamano katika nafasi za juu za maamuzi.

Aliyekuwa Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi, alisema mabadiliko ndani ya Chama ni jambo la kawaida, hivyo wanachama wanatakiwa kuendana na kasi ya Rais Magufuli.

WAKAZI DAR WAUNGA MKONO

Wakazi wa Dar es Salaam wameunga mkono uteuzi wa wajumbe wapya kwenye sekretarieti ya CCM, huku wakisisitiza umuhimu kwa wajumbe hao, kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwezesha kufanikiwa utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Wamebainisha kuwa uamuzi wa kupunguza idadi ya vikao ndani ya chama hicho utasaidia kuwafanya viongozi wa Chama kuwa karibu zaidi na wananchi, badala ya awali kutumia muda mrefu kufanya vikao vya ndani.

Wakitoa maoni hayo jana, kwa nyakati tofauti, Neema Allan alisema uteuzi huo wa viongozi utaleta mafanikio endapo viongozi hao watashirikiana pasipo kuwekeana vipingamizi visivyokuwa na maslahi kwa Chama.

“Lazima waweke maslahi ya chama mbele, kwani CCM kimepitia kwenye nyakati ngumu, ambapo wananchi walianza kutokuwa na imani nacho kutokana na baadhi ya waliokuwa viongozi na wanachama kutoweka mbele maslahi ya wananchi,” alisisitiza. 

James John, alisema viongozi hao wanapaswa kuwa na umoja wa kufanya kazi ili waweze kuepuka na kuondoa rushwa, hivyo uteuzi huo umekuja kwa wakati muafaka na ni vyema ukaungwa mkono.

Aliwataka kujikita katika kuondoa mpasuko miongoni mwa wanachama na makundi yaliyokuwa yakikinyima Chama ushindi.

“Kwa kweli nimefurahishwa na kauli ya Rais Dk. Magufuli, aliyosema kwamba hakutakuwa na msamaha wa mtu yeyote atakayejihusisha na rushwa,” alisema James Kondo, ambaye ni mkazi wa Mwananyamala.

Alitoa angalizo kuwa kupungua kwa vikao vya Chama ni suala ambalo linahitaji muda wa kuangaliwa vizuri kwani hata vikao vya awali vilikuwa havifanyiki mara kwa mara.

“Pia, kutumika kwa kadi moja ya Chama na kufuta kadi za jumuia kutawasaidia wanachama kulipa kodi zao kwa wakati na kuondoa utitiri wa kadi kwa wanachama.

“Mwanachama mmoja ana kadi nne za jumuia na zote zinapaswa kulipiwa ada kila mwezi,” alibainisha Kondo.

Kwa upande wake, mfanyabiashara ndogondogo, Athumani Juma, alishauri viongozi wote walioingia kwenye sekretarieti, wafanyekazi kwa bidii ili kukuza umoja na mshikamano ndani ya Chama.

IMEANDIKWA NA JACQUELINE
MASSANO, WILLIAM SECHAMBO NA
ESTHER JOHN, ALECK NANGANGI (RAIDA)

No comments:

Post a Comment