Thursday, 15 December 2016
WAFUASI CUF WATWANGANA MAKONDE MAHAKAMANI
HALI ndani ya chama cha Civic United Front (CUF), imezidi kuwa mbaya baada ya watu wanaodaiwa wanachama wa chama hicho, kupigana hadharani ndani na nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyoko Dar es Salaam.
Tukio hilo la aibu na fedheha kwa chama hicho lilitokea jana, kuanzia saa 7.00 mchana, wakati Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alipokuwa anaingia mahakamani hapo, akiwa na walinzi wake, ambapo ghafla wanachama wengine walianza kuwarukia wafuasi wa mwenyekiti huyo na kuanza kuwapiga.
Mapambano hayo ya ngumi za kavu kavu yalisababisha wafuasi wanaosadikiwa kuwawako upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad, kuingizana hadi katika maktaba ya mahakama hiyo na kusababisha taharuki kwa baadhi ya wafanyakazi wa mahakama hiyo na watu wengine waliokuwa wakifuatilia kesi zao.
Mapambano hayo hayakuishia hapo, kwani baada ya Jaji Sakieti Kihiyo, kutoa maamuzi ya kutupilia mbali ombi lililopelekwa na Bodi ya CUF kwamba, lilikuwa halina mashiko kwa mahakama hivyo, wafuasi hao waliendelea kupigana na kusababisha watu watatu kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Tukio hilo ambalo lilidumu kwa takribani dakika 15, lilisababisha vurugu kubwa na taharuki eneo la mahakama hiyo.
Baadhi ya wafuasi hao walikuwa wakipigana ndani na nje ya geti, ambapo mabaunsa wa pande zote mbili kwa maana ya upande wa Maalim Seif na Profesa Lipumba, walikuwa wakizichapa kavu kavu na wengine walitumia vitu vyenye ncha kali.
Wakati purukushani hizo zikianza, baadhi ya wafuasi wanaomuunga mkono Profesa Lipumba, walimuondoa mwenyekiti huyo kwa staili ya kininjaninja, ambapo walimzingira bila ya kuonekana na kumuingiza kwenye gari na kuondoka kwa haraka.
Wakati wafuasi wa chama hicho wakiendelea kupambana, wapitanjia walikusanyika na kuwashangaa kutokana na tukio hilo la ajabu.
Majeruhi wa tukio hilo waliondolewa na wenzao na kupelekwa hospitali kwa ajili ya kupata matibabu, ambapo walikuwa wakionekana wakitokwa damu nyingi sehemu za shingoni.
Polisi walitoa amri ya kuwataka wananchi kuondoka eneo la mahakama kwani muda wa kazi ulikuwa umemalizika, hivyo wafuasi hao walitawanyika na kupanda kwenye magari na kurudi sehemu walikotoka.
Kesi hiyo ilifika mahakamani hapo kwa ajili ya kutolewa maamuzi, ambapo mahakama hiyo imetupilia mbali ombi lililopelekwa na Bodi ya CUF, kutaka Jaji Kihiyo anayeendesha shauri hilo ajitoe.
Bodi hiyo ilifungua kesi ya madai dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba na wanachama 11 wa chama hicho.
Bodi hiyo ilitaka Jaji Kihiyo ajiondoe katika shauri hilo, ambapo maombi yaliwasilishwa na Wakili Nassoro, ambaye alidai wateja wake wana sababu mbili muhimu za kumkataa jaji huyo.
Wakili Juma Nassoro alieleza msingi wa hoja ya kwanza unajengwa na kesi hiyo wakati ilipotajwa Novemba 11, mwaka huu, ambapo Jaji huyo aliibua hoja inayohusu uhalali wa wadhamini, ambayo ilikuwa na mwelekeo wa kuwaonyesha nini wafanye.
Pia, hoja nyingine ni kauli iliyotolewa na jaji huyo kwamba, shauri hilo limefunguliwa haraka haraka, hivyo kutokana na sababu hizo, wateja wake wameomba Jaji Kihiyo, ajitoe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment