Sunday, 18 December 2016

KINANA AWAKA, ATOA MWEZI MMOJA CCM DAR KUHAKIKI MALI ZAKE




KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana, ameagiza uongozi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, kuhakiki mali zake zote ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Alitoa agizo hilo jana, alipokuwa akizindua jengo la makazi la Chama, lililoko Upanga, Dar es Salaam.

Kinana alisema baada ya mwezi mmoja, anatarajia kufanya ziara kwenye mkoa wa Dar es Salaam, kwa ajili ya kupitia na kuzihakiki mali hizo.

“Najua sitaweza kuzipitia mali zote, lakini nitapitia wilaya zote na nitachagua mali ambazo nitazipitia.

“Mkoa unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mali zisizohamishika na zinazohamishika ni Dar es Salaam, hivyo nawaagiza viongozi mzifuatilie na kuzihakiki mali hizo,”alisema Kinana.

Alisema mali hizo zinatakiwa kutumika vizuri ili ziweze kukinufaisha Chama na wanachama wake kwa sababu ni mali za wana CCM.

Aidha, alisema mara baada ya kumaliza ziara hiyo na kujiridhisha, atakutana na halmashauri kuu za wilaya na baadaye kukutana na halmashauri kuu ya mkoa kwa ajili ya kupeana maelekezo.

Kinana alisema mali hizo zinatakiwa kuwa mikononi mwa CCM kwa manufaa ya Chama na ziendeshwe kibiashara na kisasa ili ziwe na tija.

Mbali na Dar es Salaam, Kinana alisema ana mpango wa kutembelea mikoa 13, inayoongoza kwa kuwa na wingi wa mali za CCM kwa ajili ya kuhakiki na kufuatilia.

Kuhusu kikao cha NEC kilichokaa wiki hii, alisema kilipunguza idadi ya wajumbe kwenye nafasi zote ili kubana matumizi ya uendeshaji wa vikao  na kupunguza mijadala isiyokuwa na tija ndani ya vikao.

“Tumepungaza idadi ya vikao ili kupunguza urasimu, kwa sababu watu wanakuwa wengi, kikao kikubwa na wakati mwingine mazungumzo yanakuwa marefu ambayo hayana tija,” alisema.

Aidha, Katibu Mkuu alisema wameamua kupunguza madaraka kwa viongozi ili kupunguza mlundikano wa vyeo.

“Utakuta mtu ni mwenyekiti wa CCM, mbunge, waziri, mjumbe wa NEC yaani vyeo vyote anavyo yeye, hivyo inakuwa ngumu kumjadili hata akiwa ametenda kosa,” alisema.

Akijitolea mfano, alisema: “Hata mimi (Kinana) kama ninataka kugombea ubunge ni lazima niache cheo changu cha ukatibu mkuu.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la CCM, Anna Abdallah, alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni saba na samani za sh. milioni 300.

Aliiomba CCM kuwa na kitengo maalumu cha kitaalamu kitakachosimamia na kuratibu miradi ya Chama.

Alisema CCM ina mali nyingi, lakini hazina kitengo maalumu kinachozifuatilia mali hizo. “Mali za CCM ni nyingi, lakini hazijulikani, bila ya kuwa na utaratibu maalumu zitapotea bure.”

Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Zakhia Meghji, alisema lengo la miradi hiyo ni kuifanya CCM iweze kujitegemea kiuchumi na  kimapato.

“Mwenyekiti wetu Rais Dk. John Magufuli alikitaka Chama kujitegemea kwa sababu kina miradi mingi na hii itakuwa ni changamoto kubwa kuhakikisha Chama chetu kinaweza kujitegemea,” alisema.

Aliongeza kuwa mapato yatakayopatikana kwenye miradi hiyo hayaimarishi tu pale kitega uchumi kilipo, bali kinaimarisha Chama kizima.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Mababida, alisema CCM ina wasomi wengi, lakini hawana weledi na uwezo wa kuiendesha miradi hiyo.

“Tunahitaji mtu wa kuendesha miradi hii na kuisimamia, anatakiwa mtu mwenye sifa na  vigezo atakavyopewa na Chama,” alisema.

No comments:

Post a Comment