Sunday, 18 December 2016
NEEMA YAJA KWA WAMACHINGA DAR
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametangaza neema kwa machinga kwa kuagiza kuunda uongozi wa mpito, utakaoshughulikia kupata ufumbuzi wa changamoto na masuala yote yatakayowahusu wafanyabiashara hao.
Aidha, ametangaza kutoa sh. milioni 100, iwapo machinga wataunda chama chao cha kuweka na kukopa (SACCOS).
Katika hatua nyingine, Makonda amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Scholastical Liana, kumwandikia barua Mwenyekiti wa Bodi ya Soko la Kariakoo ili kuitisha kikao haraka cha wanahisa wote wa soko hilo.
Alisema kikao hicho kitazame upya muundo wa soko, makusudio ya kuanzishwa kwake na kupitia kiundani utozwaji ushuru na huduma za kupata umiliki wa vizimba sokoni hapo.
Sambamba na hilo, Makonda alimtaka mkurugenzi huyo wa jiji kufanya mkutano wa hadhara ili kuwaeleza wafanyabiashara hatma yao ili wajue wanachostahili kufanya na wasio stahili mara baada ya mapitio hayo.
Makonda alitoa maagizo hayo wakati wa ziara yake katika Soko Kuu la Kariakoo na Mtaa wa Congo, iliyolenga kusikiliza na kutatua kero za wafanyabishara.
Mbali na maagizo hayo, akiwa sokoni Kariakoo, Makonda aliagiza uchunguz wa kina ufanyike kujua vyanzo vya mapato katika soko hilo, kukaagua stakabadhi zote za malipo zinazotolewa ili kujua kama fedha inayolipwa inaingia moja kwa moja katika soko hilo.
Pia, alitaka uchunguzi wa kina kufanyika juu gharama za vitambulisho vya wafanyabiashara katika soko hilo, ambapo kila mfanyabiashara ilidaiwa kuwa anatozwa sh.15,000, kwa ajili ya kitambulisho.
“Mkurugenzi wa jiji upitie idadi ya watumishi waliopo sokoni kama ni idadi halali na wanapaswa kuwepo katika soko letu. Kuna idadi kubwa ya wafanyakazi, huenda tukapata watumishi hewa katika Soko la Kariakoo, ambao wanakwamisha jitihada za Rais katika kuwatetea wanyonge,” alisema Makonda.
Aliongeza: "Wakati wa kunyoosha mambo umefika, kama kuna wafanyabishara wamehodhi vizimba zaidi ya 10, ndani ya soko waviachie. Tunazo taarifa kwamba, kuna wafanyabishara wanamiliki vizimba hata zaidi ya 10 na kazi yao kubwa ni kukusanya kodi, wajiandae kuviachia vibanda hivyo ili hata wale wanyonge waweze kuvipata."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment