KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, amesema watahakikisha Chama kinakuwa kimbilio la wananchi wasio na sauti.
Kauli hiyo aliitoa jana, kwenye Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM mjini Dar es Salaam, alipokuwa akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnaye.
Polepole alisema atahakikisha kuwa CCM inatetea wanyonge na inaendelea kuwa kimbilio kwa wale wasiokuwa na sauti.
“Msingi wa Chama chetu ni utetezi wa wanyonge. Tutahakikisha kinaendelea kuwa kimbilio la wasio na sauti,” alisema.
Kuhusu serikali tatu, alisema: “Mimi ni mwanachama wa CCM kwa imani na ninazishika ahadi za chama, mojawapo nitasema ukweli daima fitina kwangu mwiko.
“Msimamo wangu ni madhubuti kwenye Chama changu na kwa taifa langu, iliyo haki nitasimamia haki, iliyo kweli nitasema kweli wakati wote huwa sibadilishi maneno.”
Akizungumza kabla ya kukabidhi ofisi, Nape aliishukuru CCM kwa kumwamini na kumpa jukumu la kuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi kwa miaka mitano.
“Namshukuru sana Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kuniamini, pia nawashukuru wanachama wenzangu wa CCM kwa kuwa pamoja katika miaka mitano,” alisema.
Nape alisema watu wengi waliamini kuwa ameisaidia CCM, lakini ukweli ni kwamba, yeye ndiye aliyesaidiwa na Chama.
“CCM imenisaidia mimi zaidi kuliko mimi nilivyoisaidia. CCM ni shule. Nina uzoefu mkubwa, ambao nimeupitia, una milima na mabonde,” alisema.
Aidha, Nape alisema katika jambo kubwa ambalo hataweza kulisahau alipokuwa CCM, ni kufanyakazi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
“Nilipata bahati kubwa sana ya kufanya kazi na Kinana, kwa kweli namshukuru kwani amekuwa ni zaidi ya mwalimu kwangu,” alisema Nape.
No comments:
Post a Comment