Monday, 19 December 2016

SERIKALI SASA YAAGIZA FARU JOHN AFUKULIWE

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema timu aliyoiunda kwa ajili ya kuchunguza kifo cha Faru John, imetua Sasakwa VIP Grumet, Serengeti kwa ajili ya kuchukua vinasaba vya masalia ya mnyama huyo. 

Amesema baada ya kuchukua vinasaba vya mabaki ya Faru John, pia timu timu hiyo itakwenda eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kwa ajili ya kuchukua vinasaba vya watoto wake ili vilinganishwe na pembe iliyowasilishwa ofisini kwake, kuweza kubaini kama kweli ni ya mnyama huyo au laa.

"Tume niliyoiunda kwa ajili ya uchunguzi wa Faru John imetua VIP  Grumet Serengeti, ili kujiridhisha kama kuna kaburi lake na kuchukua vinasaba na baada ya hapo, watakwenda Creter Ngorongoro kwa ajili ya kuchukua vinasaba vya watoto wake ili vipimwe na kubaini kama pembe iliyowasilishwa kwangu, Desemba 9, mwaka huu, ni ya Faru John,"alisema.

Alisema wakati Faru John akiwa VIP Grumet, zilitolewa taarifa zilizodai kuwa ni mgonjwa, lakini daktari alipompima mara ya kwanza, alibaini faru huyo hakuwa mgonjwa.

Majaliwa alisema taarifa kama hizo zilitolewa tena kwa mara ya pili, lakini daktari alipompima tena alibaini hakuwa mgonjwa na kwamba, baada ya hapo ghafla zilitoka taarifa za kifo chake.

Kwa mujibu wa Majaliwa, serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka Afrika Kusini, hivyo ni lazima rasilimali hizo muhimu za taifa zilindwe.

"Haiwekani Daktari ampime Faru John mara mbili kwa nyakati tofauti na kubaini siyo mgonjwa, halafu ghafla taarifa zinakuja amekufa. Haiwezekani, serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua wanyama hawa toka Afrika Kusini, lazima tuwalinde,"alisema.

Desemba 6, mwaka huu, Waziri Mkuu akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa, akizungumza na watumishi wa NCAA, alisema Faru John aliondolewa na watumishi wa NCAA, pamoja na watumishi wawili wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na kumpeleka VIP Grumet, ambako walikuwa wameahidiwa sh. milioni 200, lakini badala yake walipewa sh. milioni 100.

Alisema ni aibu kwa faru kuondoka kreta huku Waziri wa Maliasili  na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, hadi leo akiwa hajui kama kuna tukio kama hilo hadi alipotoa taarifa hiyo.

“Ninatoa siku mbili nipate taarifa zote mezani kwangu, kuanzia taarifa za vikao mnavyodai vilikaa, barua ya maombi ya kumtoa Faru John hapa, taarifa ya daktari pamoja na pembe yake, maana mnasema alikufa na nakala zote za barua ziwe halisi na sio za kudurufu,”alisema.

Watumishi waliotajwa na Waziri Mkuu kushiriki mchakato wa kumuondoa Faru John kutoka NCAA ni Cathbety Lemanya, ambaye ni mkuu wa kanda katika eneo la kreta.

Wengine ni Israel Noman na Patrice Mattey, wote wakiwa watumishi wa NCAA pamoja na watumishi wawili wa TANAPA, Kileo na Macha, aliowataja kwa jina moja moja, ambapo alisema awali alikuwa katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, lakini alihamishiwa NCAA kwa kazi maalumu ya kumhamisha Faru John, ambapo baada ya kazi hiyo, alihamishiwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Kuhusu Macha, alisema alikuwa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, lakini alihamishiwa NCAA, kwa ajili ya kazi hiyo maalumu ya kumuondoa Faru John na kumpeleka Sasakwa VIP Grumet.

"Naagiza Kileo na Macha kwa pamoja warudishwe hapa mara moja, waje kujibu Faru John yuko wapi. Haiwezekani faru aondoke kreta bila kuwepo taarifa za kina,”alisema.

No comments:

Post a Comment