Monday, 19 December 2016
MAHAKAMA YA MAFISADI YAKOSA KESI ZA KUSIKILIZA
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema serikali inafikiria kushusha kiwango cha sh. bilioni moja, kinachoanza kusikilizwa kwenye Mahakama ya Mafisadi, kuwa chini ya hapo ili watu wengi zaidi wafikishwe mbele ya mahakama hiyo.
Amesema sheria ya mafisadi imewatisha watu wengi, ambao sasa wanaonekana kuacha kuiba fedha nyingi, hivyo ni lazima kiwango hicho kishushwe ili kwenda na kasi ya wizi wa fedha za umma.
Dk. Mwakyembe alisema hayo jana, baada ya kukagua ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Kigamboni, ambayo ujenzi wake unatumia gharama nafuu.
Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, Mahakama ya Mafisadi haina kesi nyingi kutokana na watumishi wengi wa serikali na watu binafsi kuacha kufanya ubadhirifu wa fedha za serikali.
Alisema katika sheria iliyopitishwa bungeni ya mafisadi, iliweka kiwango cha shilingi bilioni moja ili mtu afikishwe katika Mahakama ya Mafisadi, lakini hadi sasa ni kesi moja tu iliyofikishwa katika mahakama hiyo.
"Tangu watu wajue ipo sheria ya mafisadi, wameacha kuiba fedha nyingi za serikali, hivyo kusababisha mahakama hiyo kukosa kesi.
"Mahakama ya Mafisadi inaanza kusikiliza kesi zinazohusisha wizi au upotevu wa kuanzia shilingi bilioni moja na wengi wanaoiba fedha wanaiba chini ya hapo, hivyo kusababisha kesi hizo kwenda mahakama za chini,"alisema.
Aidha, Dk. Mwakyembe alisema tatizo lililopo ni Watanzania wengi kutoifahamu vizuri sheria hiyo ya kuwafikisha mafisadi katika mahakama hiyo maalumu, ambayo imewekewa kiwango maalumu cha kumfikisha mhusika katika mahakama hiyo.
"Watu wengi hawafahamu vigezo vya mtu aliyeiba fedha za serikali kufikishwa katika mahakama hiyo, ndio maana watu wanasema fedha zinaibwa, lakini hawapelekwi mahakama ya mafisadi,"alisema.
Alisema watakapobadilisha sheria hiyo ya mafisadi kwa kushusha kiwango, wengi watafikishwa katika mahakama hiyo au wizi wa fedha za serikali utakwisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment