Monday, 19 December 2016

MAJALIWA AWAJIA JUU VIGOGO WA UTALII NCHINI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema sekta ya utalii nchini bado haijatangazwa ipasavyo na kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa nchini pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorongoro, kuanza mara moja kutangaza utalii wa nchi.

Majaliwa, alitoa agizo hili jana, wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa, ambapo alisema inashangaza kuona Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu JK Nyerere wa Jijini Dar es Salaam, umejaa mabango ya kampuni mbalimbali, hususan za simu, licha ya uwanja huo kuwa lango kuu la kuingiza watalii nchini.

“Hakuna hata bango moja la kielektroniki katika Uwanja wa JK Nyerere, linalotangaza utalii. Kuanzia sasa, wakurugenzi wote wawili ninawaagiza kutangaza utalii wa nchi. Kwa kuanzia nataka barabara ya Nyerere kuanzia Tazara hadi Airport, kuwe na mabango yanayotangaza utalii wa nchi na siyo mabango ya kampuni za simu, bongo fleva na mengine.

“Pia, nataka nione mabango yenu katika eneo la Terminal one, Terminal Two na eneo lote la VIP katika uwanja wa JK Nyerere,”alisema.

Aidha, Waziri Mkuu alioonyesha kukerwa na kitendo cha utalii wa nchi kwenda kutangazwa katika timu ya Sunderland, wakati wakiwa wanafanya mazoezi huku wakijua bayana kuwa timu hiyo kwa sasa haina mashabiki wengi.

"Niliumia sana katika mkutano wangu AICC wakati mwenyekiti wa TATO taifa, alipoeleza kuwa utalii wa nchi unatangazwa kwenye timu ya Sunderland wakati ikifanya mazoezi.

“Kwa nini msitangaze kwenye timu kubwa kama Barcelona, Man city na nyingine nyingi, ambazo zina wapenzi wengi, kama mmeamua kutangaza utalii kupitia timu za mipra. Nani siku hizi anaangalia Sunderland?"Alihoji.

Pia, aliwataka wakurugenzi hao kuanza kufanya mchakato wa kuomba kupanda bustani nzuri za maua katika eneo la  barabara mpya ya Arusha Meat- Tengeru, (By pass) ili waweze kuweka matangazo yanayotangaza vivutio vya utalii wa Tanzania.

“Chukueni eneo la katikati ya barabara ya Arusha Meat-Tengeru, mpande bustani nzuri za maua halafu muweke mabango ya kutangaza utalii. Arusha ni kitovu cha utalii  nchini,”aliagiza.

Majaliwa alitumia majumuisho hayo kuzitaka Tasisi zisizo za Kiserikali (NGO) 19, kujitathimini juu ya utendaji wao katika wilaya ya Ngorongoro, hususan tarafa ya Loliondo na kuacha mara moja tabia ya kuichonganisha serikali na wananchi wake.

“Nimepata taarifa zenu kuwa mnakwenda kutoa tamko lenu juu ya maaagizo ya serikali jijini Dar es Salaam, nendeni mkatoe, lakini msimamo wa serikali uko pale pale na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), atakuja kukagua matumizi yote ya fedha mnazozipata na shuguli za kijamii mnazozifanya ili kuona kama zinaendana na mapato yenu,"alisisitiza.

Alizitaka asasi hizo za kiraia kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia malengo yake ya usajili na siyo kufanya vinginevyo, ikiwemo kuchochea migogoro ya ardhi kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment