Monday, 19 December 2016
NASSARY: ANAYEPINGANA NA SERIKALI YA MAGUFULI KICHAA
MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassary (CHADEMA), amesema kiongozi yeyote, ambaye hatakubaliana na kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kutekeleza majukumu ili kuwaletea wananchi maendeleo, atakuwa ni kichaa.
Nassary, alitoa kauli hiyo jana, wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya siku 10 ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mkoani hapa, kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha.
“Kiongozi, ambaye hatashirikiana na kukubalina na serikali ya awamu ya tano katika kutekelza majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo, atakuwa ni kichaa.
“Tutashirikiana na serikali hii ya awamu ya tano kwa hali na mali kwa kuwa imeonyesha dira na dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi wanyonge maendeleo ya kweli,”alisema mbunge huyo.
Kwa mujibu wa Nassary, yeye na wabunge wenzake, ambao hakuwataja majina, wamezungumza na kukubalina kuunga mkono serikali ya awamu ya tano na kwamba, huo utakuwa ndio msimamo wao kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Tumezungumza na wabunge wenzangu na haya ninayoyasema ndiyo msimamo wetu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi tunaowawakilisha,”alisema
Awali, katika kikao hicho, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Mbunge Nassary alimwandikia barua pepe ya kuomba udhuru na kwamba, hataweza kuhudhuria ziara yake kwa kuwa yuko masomoni nje nchi.
“Nilipokea barua pepe kutoka kwa mbunge mwenzangu, Nassary akinijulisha kuwa asingeweza kushiriki ziara yangu jimboni kwake kwa kuwa yupo masomoni nje ya nchi na mimi nilikubalina na udhuru wake,”alisema.
Hata hivyo, alimpongeza Nassary kwa kushindwa kuvumilia na kulazimika kusafiri usiku kucha kutoka Uingereza na hatimaye kujumuika na viongozi wenzake wa Arusha, katika majumuisho ya ziara hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment