Monday, 19 December 2016

SERIKALI YAUNDA TUME YA MOTISHA


SERIKALI imesema imeunda Tume ya Motisha na Mishahara, ambayo itahusika na uboreshaji wa maslahi ya watumishi wote nchini.

Imesema tume hiyo tayari imeanza kazi ya kupitia malimbikizo yote ya watumishi wa umma katika idara mbalimbali ili waweze kulipwa stahili zao.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa, ambapo alisema tume hiyo pia inafanya uhakiki wa watumishi waliostaafu na waliofariki, ambao wanaendelea kulipwa mishahara na kuchukuliwa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu.

"Serikali imeunda tume kwa ajili ya motisha na mishahara ili kuwezesha watumishi wa umma kulipwa mishahara kwa wakati  na kupata motisha ili waweze kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kila siku kwenye utumishi wa umma,"alisema.

Alisema tume hiyo itakuwa mwarobaini utakaomaliza malimbikizo ya madeni ya watumishi.

Aidha, aliwaagiza watumishi wote wanaoajiriwa kwamba, mwisho wa kuripoti katika vituo vyao vya kazi iwe tarehe tisa ya kila mwezi ili waweze kuingia kwenye orodha ya malipo kwa wakati.

"Watumishi endeleeni kutuamini, tunathamini mchango wenu ambao unaifanya serikali kuaminika na wananchi. Tuna nia ya dhati ya kuboresha maslahi yenu,"alisema.

Majaliwa alitumia kikao hicho kuwakumbusha watumishi hao uwajibikaji katika maeno yao ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuwa na nidhamu.

Aliwataka wakuu wa idara kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya halmashauri zao pamoja na kuwa na nidhamu ya fedha za miradi hiyo ili ijengwe kwa kiwango kinachotakiwa.

"Wakuu wa idara simamieni kikamilifu miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuwa na nidhamu ya fedha zinazotekeleza miradi kwa kuzielekeza katika maeneo husika ili itekelezeke kwa kiwango,"alisema.

Aidha, aliwaonya watumishi wanaoshindwa kutumiza majukumu yao katika maeneo yao ya kazi na kuwataka wabadilike mara moja.

"Serikali haitaki kukwazwa na watumishi wanaoshindwa kutimiza wajibu. Tukigundua mtumishi una mkakati wa kutukwaza, tutakuondoa haraka bila kuchelewa,"alisema.



No comments:

Post a Comment