Tuesday, 24 January 2017

ASKARI WANAOUZA TOCHI WASAKWA


MKUU wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishina wa Polisi, Mohamed Mpinga, amesema upelelezi wa askari 'wanaouza' tochi kwa baadhi ya wamiliki na madereva wa mabasi yaendayo mikoani unaendelea.

Ameonya kuwa askari, ambaye atabainika kufanya usaliti huo, atachukuliwa hatua kali, ambazo zitakuwa fundisho kwa wengine.

Mpinga alisema hayo jana, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na Uhuru, ofisini kwake, kuhusu udhibiti wa mwendo wa magari yaendayo mkoani.

Alisema malalamiko kuhusu mwendo wa baadhi ya mabasi yamekuwepo na yanafanyiwa kazi taratibu ili kubaini iwapo yana ukweli kiasi gani.

“Kinachotokea ni kwamba, baadhi ya askari wetu wamekuwa wasaliti kwa kukubali kununuliwa na baadhi ya madereva na wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani.

"Badala ya kumulika, wanaweka tochi chini  kwa kuwa zimeshalipiwa, hivyo taarifa tunazo na upelelezi unaendelea ili kuwabaini wanaofanya vitendo kama hivyo.

"Hata hivyo, abiria bado hawajawa na uthubutu wa kutoa taarifa ya hali ya mwendo wa mabasi husika na hilo ni miongoni mwa yanayochocheo kununuliwa kwa tochi,”alisema.

Kamishna Mpinga alisema kama abiria watathubutu kukemea mwendo kasi, ajali zitapungua kwa kiwango kikubwa kwa sababu askari ambao sio waaminifu wataogopa kupokea rushwa.

Aidha, alitoa wito kwa abiria kutoa ushirikiano kupitia namba, ambazo zinakuwa ndani ya mabasi kwa kutoa taarifa ya mwendo wa hatari wa basi husika ili kuokoa maisha ya wengi.

Mabasi mengi, hasa yaendayo mikoa ya kaskazini, yamekuwa na mwendo kasi wa kuanzia kilomita 120 kwa saa, badala ya 80, ambao ndio mwendo unaotakiwa na wenye usalama zaidi.

Mwandishi wa gazeti hili alisafiri kwa mabasi mawili ya kampuni tofauti, ambapo pamoja na uwepo wa tochi hizo barabarani, mabasi hayo yalikuwa  na mwendokasi, ambao ni juu ya kilometa 100 kwa saa, ambao ni hatari, lakini hakuna lililokamatwa.

Mwandishi wetu pia alishuhudia baadhi ya askari wa usalama barabarani, wakipeana ishara na madereva wa mabasi hayo na kuendelea na mwendokasi huo bila kuzuizi.

No comments:

Post a Comment