Tuesday, 24 January 2017

TANZANIA, UTURUKI ZATIA SAINI MIKATABA TISA



 Rais Dkt. John Pombe Joseph magufuli akisalimiana na Mwakilishi kutoka Uturuki  Bw, Ziya Karahan wakati wa chakula cha jioni alichomwandalia Rais huyo leo jijin Dar es Salaam. Mwenye tai nyekundu ni Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

 Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akipeana mkono na Mke wa Rais Dkt. Magufuli Mama Janeth Magufuli leo jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Rais Dkt. John Pombe Joseph magufuli na Mama Janeth Magufuli wakigonga cheers wakati wa hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa mahususi kwa ajili ya Rais huyo wa Uturuki leo jijin Dar es Salaam.
 Baadhi ya wageni waalikwa katika dhifa ya chakula cha jioni  kwa ajili ya kumuaga Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan leo jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt. John Pombe Joseph magufuli akipiga ngoma baada ya kufurahishwa na burudani kutoka kwa Bendi ya Mrisho Mpoto na Banabana wakati wa chakula cha jioni alichomwandalia Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan leo jijin Dar es Salaam. Picha na: Frank Shija – MAELEZO.

SERIKALI za Tanzania na Uturuki zimetiliana saini mikataba tisa yenye lengo la kuzinufaisha nchi hizo  katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya kiuchumi, kibiashara, uchukuzi, kidiplomasia, utalii na elimu.

Hafla ya kutiliana saini mikataba hiyo ilifanyika jana, Ikulu, jijini Dar es Salaam, katika siku ya pili na ya mwisho ya ziara ya kikazi ya Rais wa Uturuki, Recep Erdogan, aliyewasili nchini juzi na kupokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza kwenye  hotuba yake fupi iliyotumia takriban dakika 20, Rais Dk. John Magufuli, alisema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni mwanzo wa uhusiano  imara baina ya nchi hizo kwa miaka mingi ijayo.

Dk. Magufuli alisema moja kati ya mambo muhimu aliyoyazungumza na Rais Erdogan, ni kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge, ambapo Rais huyo ameonyesha nia ya kusaidia kukamilika kwa ujenzi huo haraka.

Alisema ujio wa Rais huyo wa Uturuki, ambaye ameichagua Tanzania kama nchi yake ya kwanza kuzuru barani Afrika, tangu kuchaguliwa kwake na kusaini mikataba mingi kiasi hicho, ni fahari kwa Tanzania na watu wake.

"Tunashukuru kwa ujio huu, nimeongea na Rais Erdogan, kwa kupitia Benki ya Uturuki ya Exim, watukopeshe fedha kiasi tukamilishe ujenzi wa reli yetu ya kisasa na ameuliza urefu wake, nimemwambia kama kilomita 4,000 hivi na zaidi, akasema ni chache sana, hivyo atatusaidia," alisema.
  
Rais Dk. Magufuli alisema hapa nchini, kwa takwimu za mwaka jana, Uturuki ina biashara zenye mitaji ya Dola za Marekani 190, kutoka mitaji ya Dola milioni 66, iliyokuwepo miaka mitano iliyopita.

Alisema si hivyo tu, pia kuna jumla ya kampuni 30, zenye uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 305, ambapo kwa ujumla wake, zimetoa ajira kwa Watanzania 2,950, hivyo nchi hizo zina undugu wenye manufaa bila kuwepo shaka.

"Hii ni safari yake ya kwanza Afrika, ninaamini tutanufaika zaidi kwa sababu kule kwetu kuna usemi usemao, 'mtoto wa kwanza  hunyonya maziwa mengi ya mama', hivyo nasi tutapata mikataba mingi zaidi," alisema.  

Aliongeza: "Kati ya mikataba tuliyotia saini leo, ipo inayohusu usafiri wa anga. Turkish Air ni shirika kubwa na tayari linafanya safari  zake kwenye viwanja mbalimbali hapa nchini, kikiwemo Zanzibar, Dar es Salaam na Kilimanjaro, tunataka kuongeza mahusiano zaidi kwenye sekta hii."

Rais Magufuli alisema pia  kuwa serikali yake inatambua Uturuki ni nchi ya saba duniani kuzalisha mazao ya kilimo, hivyo kwa kuwa asilimia 80, ya Watanzania hutegemea kilimo, watahakikisha wanatumia fursa ya undugu huo kuendeleza sekta ya kilimo.

"Tanzania ni nchi inayoendelea, ninachokiamini ni kwamba, hakuna uchumi thabiti bila mahusiano, bila urafiki na bila kushirikiana. Tumeanza, naamini tutafanikiwa na ninakuhakikishia Rais Erdogan tuko pamoja na wewe," alisema Rais Magufuli.

Pamoja na hilo, Rais Magufuli alimshukuru Rais huyo kwa kumpokea kwa ukarimu Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Uturuki, Elizabeth Kiondo, ambaye alichaguliwa kuiwakilisha Tanzania nchini humo hivi karibuni.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa jinsia, aliamua kumteua balozi mwanamke kwenye nchi hiyo, ambayo haikuwahi kuwa na balozi kutoka hapa nchini na kwamba, baada ya uzinduzi wa ofisi ya balozi huyo mjini Ankara, imani ya Tanzania ni kuimarika kwa diplomasia.

RAIS MAGUFULI KUFANYA ZIARA UTURUKI
Dk. Magufuli akizungumza kwenye hotuba yake, alisema anaweza kwenda nchini Uturuki ili kuongeza uhusiano baina ya nchi hizo, hasa ikizangiwa amepewa mwaliko na Rais Erdogan kuhudhuria uzinduzi wa ofisi rasmi ya balozi wa Tanzania mjini Ankara.

Kauli hiyo inakuja huku ikikumbukwa kuwa, tangu kuapishwa kwake Novemba 5, 2015, hajawahi kufanya ziara nje ya Afrika, mbali na kuzuru nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, zote za Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Rais wa Uturuki, Erdogan alisema mazungumzo yaliyofanyika kati yake na Rais Dk. Magufuli, yameleta matokeo mazuri katika kukuza ushirikiano wa kibiashara, uchumi, utalii, reli na sekta ya ujenzi.

“Makubaliano tulioyafikia ni kielelezo kizuri katika kuimarisha ushirikiano wetu. Uturuki itaweka vitega uchumi vikubwa zaidi pamoja na kuinua wajasiliamali kwa lengo la kukuza biashara baina ya mataifa haya mawili, kutoka Dola Milioni 150 hadi kufikia Dola Milioni 500, kwa mwaka,” alisema.

Alisema kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 4,500, kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaosoma Uturuki, ambapo kati ya hao, 38 wanatoka Tanzania. Aliweka bayana kuwa, serikali yake itaongeza nafasi zaidi kwa wanafunzi kutoka nchini.

Rais Erdogan alibainisha kuwa sera ya nchi yake kwa Afrika ni usawa, kwani haitaki kujenga ushirikiano wenye kunufaisha upande mmoja, hivyo imelenga kushirikiana na Tanzania kwa sababu ni taifa lenye amani na idadi kubwa ya watu.

Rais huyo hakusita kuelezea ukarimu wa Tanzania huku akisifu vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti, Visiwa vya Zanzibar pamoja na Ziwa Tanganyika.

Alitoa mwaliko kwa Rais Dk. Magufuli, kutembelea Uturuki, hususan wakati wa ufunguzi wa ubalozi wa Tanzania katika jiji la Ankara.

Kiongozi huyo alielezea tukio la jaribo la mapinduzi lililofanyika nchini humo Julai 15, mwaka jana, ambapo raia 240 waliuawa na wengine zaidi ya 2500 kujeruhiwa.

Erdogan alisema kushindikana kwa jaribio hilo ni kitendo cha kishujaa kilichofanywa na wananchi wa Uturuki, katika kutetea demokrasia dhidi ya watu waliotaka kuipindua serikali yake.

“Tunao ushahidi kuwa, jaribio hilo lilifanywa na chama cha kigaidi cha FETO, ambacho kipo kwenye nchi mbalimbali duniani, hivyo natumia nafasi hii kuwataarifu kuwa makini na chama hicho ili nchi zingine zisipate matatizo kama yaliyotupata sisi,” alisema.

Baadhi ya mawaziri walizungumzia fursa mbalimbali, ambazo Tanzania itanufaika nazo baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo tisa muhimu.

MAWAZIRI WALONGA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alieleza kuwa, mkataba wa ushirikiano kwenye masuala ya utalii kati ya Tanzania na Uturuki, utasaidia kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii kwa kubadilishana taarifa muhimu.

Alisema pia kuwa, utawezesha wataalamu wa masuala ya utalii na uhifadhi, kupata mafunzo nchini Uturuki ili kusaidia kuongeza idadi ya watalii nchini.

“Uturuki ni miongoni mwa nchi zenye makumbusho kubwa duniani, ambapo kwa mwaka zaidi ya watalii milioni 10, wanaitembelea nchi hiyo kulinganisha na Tanzania, ambayo inatembelewa na watalii milioni moja kwa mwaka,” alisema.

Profesa Maghembe alisema, mkataba huo pia unalenga kuvutia wawekezaji katika ujenzi wa hoteli za kitalii kwenye fukwe za bahari ya Hindi.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema ujio wa Rais huyo ni fursa nyingine kwa Tanzania kutokana na ujumbe alioambatana nao wa wafanyabiashara 150, ambao watawekeza kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Alisema Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji, ambazo Uturuki imeziona na kuahidi kuzitumia kwa manufaa ya nchi zote mbili, ambapo kwa kutumia mikataba iliyosainiwa, nia zao zinatiwa nguvu kwenye utekelezaji wake.

"Rais Erdogan amekuja na wafanyabashara 150, tumekutana nao na kuzungumza, ikiwa ni pamoja na kuwaeleza fursa tulizonazo, hususan za uwekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa, tunafanya kazi na kazi inaendelea," alisema waziri huyo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya, alisema mkataba uliosainiwa kwenye sekta ya elimu ni mkombozi wa Watanzania, kutokana na nia yake ya kufungua milango kwa Watanzania wengi kusoma nchini Uturuki kupitia nafasi za bure za masomo (Scholarship).

MIKATABA ILIYOTIWA SAINI
Mikataba tisa iliyotiliwa saini jana na Mawaziri wa Tanzania na Uturuki kwa niaba ya serikali zao ni ya ushirikiano wa Shirika la Ndege (ATCL) na lile la Uturuki, Turkish Airline; Ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji la Uturuki na ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Uturuki. 

Mingine ni ushirikiano wa elimu na utafiti baina ya nchi hizo mbili; Ushirikiano wa viwanda vidogo (SIDO) na viwanda vya kati vya Uturuki (COSKEB); Ushirikiano wa masuala ya utalii kati ya Tanzania na Uturuki na ushirikiano wa viwanda vya ulinzi kati ya nchi hizo.

Sekta ya Afya haikusahaulika kwenye mikataba hii, kwa sababu kulisainiwa mkataba wa mahusiano ya afya kati ya Tanzania na Uturuki huku pia diplomasia ikipewa nafasi kwa kusainiwa mkataba wa ushirikiano kati ya Chuo cha Diplomasia  cha Tanzania na Chuo cha Diplomasia cha Uturuki.

Wakati huo huo, Rachel Kyala, anaripoti kuwa, Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan, alitoa msaada wa viti 25 vya wasiojiweza, ambapo vitano alivikabidhi kwa kituo cha watoto wenye ulemavu cha Matumaini, Mbagala na 20 kwa ajili ya kituo cha kulelea wazee cha Nungwi, Kigamboni, Dar es Salaam.

Vilevile ametoa msaada wa mashine tatu za joto kwa ajili ya kutunza watoto wanaozaliwa kabla ya wakati 'njiti' ( incubator) kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  (MNH).

Mama Emine, ametoa msaada huo katika ziara maalumu na mwenyeji wake, mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli,  alipotembelea ofisi ya Wakala wa Uratibu na Ushirikiano wa Uturuki (TiKA), Dar es Salaam, jana.

Akikabidhi misaada hiyo, Mama Emine, alisema lengo ni kudumisha uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki, ambapo wameamua
kuzisaidia nchi zenye uhitaji katika kutatua changamoto mbalimbali.

Alisema watatumia rasilimali zao kusaidia nchi nyingi zaidi duniani, hususan Tanzania, ambayo aliahidi Uturuki itaisaidia kwa moyo wote.

"Natarajia kutakuwa na mshikamano zaidi baina ya nchi hizi mbili na tutafanya mambo mengi ya maendeleo, hatutabagua dini wala rangi katika kuisaidia Tanzania dhidi  ya changamoto inazokabiliana nazo," alisema Mama Emine.

Pia, alitembelea Makumbusho ya Taifa na Kijiji cha Makumbusho, ambapo alisema amebaini baadhi ya masuala katika historia  yanayofanana na Uturuki.

Akiwa Makumbusho ya Taifa, alionyeshwa jengo la mila lenye umri wa miaka takriban 80, ambalo lilichakaa vibaya na hatimaye kukarabatiwa na serikali ya Uturuki kupitia TiKA, kwa gharama ya jumla ya sh. milioni 70.

Mama Janeth, alimshukuru mgeni wake kwa misaada hiyo na nia aliyoionyesha ya kusaidia walemavu, wasiojiweza na wasichana ambapo alisema ni maeneo, ambayo yeye pia anasukumwa kuyashughulikia.

"Nimefurahi kuona unao moyo wa kusaidia maeneo ambayo mimi pia ndio lengo langu kusaidia. Nakuhakikishia tutashirikiana ipasavyo kutatua changamoyo hizo kwa wahusika," alisema.

Aliyekuwa waziri wa nchi,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,  Ajira, Vijana na Walemavu, Dk. Abdallah Possi, akipokea msaada kwa niaba ya walemavu na wasiojiweza, alisema amefarijika kutokana na msaada huo wa serikali ya Uturuki na utatumika kama ulivyokusudiwa.

"Msaada huu  umekuja kwa wakati muafaka kwani lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuondoa matabaka baina ya makundi mbalimbali katika jamii," alisema.

No comments:

Post a Comment