Tuesday, 24 January 2017

PAC YABAINI MADUDU MIRADI YA TBA, TANROADS


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imebaini ujenzi chini ya kiwango katika baadhi ya miradi inayosimamiwa na Wakala wa Majengo (TBA) na Wakala wa Barabara (TANROADS), katika nyumba za viongozi, miradi ya barabara na wakandarasi kutolipwa kwa wakati.

Mikoa iliyobainika kuwa na ujenzi usioridhisha ni Arusha, Singida na Kilimanjaro.

Akizungumza  jana, mjini Dodoma, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Nagy Kaboyoka, alisema PAC imebaini ujenzi usiokidhi matakwa ya serikali katika miradi ya TBA, kwenye nyumba za viongozi  maeneo ya Ikungi na Mkarama.

Nagy alisema kamati hiyo imewataka wakuu wa mikoa hiyo kwa kushirikiana na TBA, kufanya marekebisho katika ujenzi wa nyumba hizo kwa kiwango cha juu .

"Ujenzi ambao umeoneka ni wa kuridhisha ni Daraja la Sibiti, lakini miradi mingine, hususan nyumba za viongozi wetu ni wa hovyo, hivyo kamati haikuridhishwa na tunaandaa ripoti ili kutoa maagizo,"alisema.

Alisema katika miradi hiyo, imebainika hakuna usimamizi mzuri, hivyo ipo haja TBA kusimamiwa ipasavyo.

Mwenyekiti huyo alisema katika miradi ya ujenzi wa barabara, ikiwemo kutoka KIA hadi Mererani, ujenzi wake ni mbovu na baadhi ya makaravati yameanza kubomoka.

"Wakandarasi hawalipwi kwa wakati na hawakamilishi miradi hiyo na wanaifanya bora liende ,"alisema.

Pia, alisema ujenzi wa nyumba ya TBA wa ghorofa 10, Arusha mjini, umewatia mashaka wajumbe wa kamati, kutokana na kuwa wa muda mfupi, lakini nyufa ni nyingi, hivyo wapangaji kushindwa kukaa na waliopo wakihofia usalama wao.

Alisema kutokana na hatua hiyo, wamemuomba Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa jengo hilo ili kubaini viwango vya ujenzi wake.

Naggy alisema maeneo yaliyofanya vizuri katika ujenzi ni yale ya fedha za miradi ya maendeleo kutoka kwa wahisani, hivyo ipo haja serikali kukaa na TBA na TANROADS ili kubaini changamoto na kuzifanyia kazi.

"Jambo la kushangaza sehemu ambazo kamati ilijua itakuta changamoto nyingi za kiutendaji ni Chuo cha Ufundi Arusha, lakini tumekuta pamoja na kukosa fedha za maendeleo kwa miaka miwili, kinafanya vizuri na ndio tegemeo kwa wataalamu kuelekea uchumi wa viwanda,"alisema.

Katika hatua nyingine, PAC imetembelea miradi ya maendeleo, ikiwemo ya huduma za umeme vijijini (REA) na kubaini mradi huo ni kichocheo cha maendeleo.

Pia, imeagiza REA kufanyiakazi changamoto za upatikanaji huduma hizo katika baadhi ya vijiji mkoani Mbeya, Songwe na Iringa ili kufikia malengo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Nagy alisema  PAC mwishoni mwa wiki, ilitembelea mikoa hiyo na  kubaini jinsi miradi ya REA, ilivyochochea maendeleo katika huduma muhimu, ikiwemo ya elimu na miradi mbalimbali.

Alisema pamoja na jitihada hizo, bado baadhi ya maeneo hayajafikiwa, ambapo REA imeahidi kukamilisha maeneo ya vijiji hivyo katika awamu ya tatu ya mradi.

Alisema kamati hiyo imelitaka Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kuhakikisha wanatoa elimu ipasavyo kuhusu huduma hiyo vijijini, hususan katika mkopo wa huduma za umeme wa awali.

Nagy alisisitiza haja ya miradi hiyo ya umeme vijijini kuifikia mikoa yote ili kuchochea huduma za kijamii.

No comments:

Post a Comment