Wednesday 25 January 2017

POLEPOLE AFICHUA SIRI TATU ZA USHINDI CCM


BAADA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuibuka na ushindi wa kimbunga katika uchaguzi mdogo wa marudio wa ubunge wa Jimbo la Dimani na udiwani kwenye kata 19 za Tanzania Bara, Chama kimeweka bayana siri tatu muhimu zilizokiwezesha kupata ushindi.

Katika uchaguzi huo, kwenye jimbo la Dimani, mgombea wa CCM, Juma Ali Juma, alipata ushindi wa kura 4,860, sawa na asilimia 78.74, dhidi ya mpinzani wake, Abdulrazak Khatib Ramadhan wa CUF, aliyepata kura 1,234.

Ushindi huo umedhihirisha anguko kubwa la CUF, visiwani Zanzibar, kwani katika uchaguzi wa mwaka 2015, licha ya kushika nafasi ya pili, kilipata wastani wa kura 2,300, lakini kwenye uchaguzi wa marudio kura zake zimeshuka kwa zaidi ya asilimia 50.

Hivyo ili kujinusuru na hali hiyo, CUF kimetakiwa kumtafuta mchawi aliyepo ndani ya chama hicho Zanzibar, badala ya kulalamika.

Aidha, CCM imejizolea viti 19 vya udiwani kati ya 20, huku CHADEMA ikipata kiti kimoja na kukifanya Chama kudhihirisha kuwa bado kinakubalika kwa wananchi.

Kufuatia ushindi huo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, ameelezea siri tatu muhimu zilizokiwezesha Chama kupata ushindi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, jana, Polepole alitaja siri ya kwanza kuwa ni namna ya mageuzi mapya ya kimuundo na mfumo yaliyolenga kuiwezesha CCM kurudi kwenye mikono ya wananchi kwa serikali yake kujikita zaidi kushughulikia kero zinazowakabili Watanzania, kufanikiwa.

Alisema mabadiliko hayo yamelenga kukifanya Chama kirejee kwenye msingi mkuu wa kuanzishwa kwake, baada ya kuvunjwa kwa vyama vya TANU cha Tanganyika na ASP cha Zanzibar.

Siri ya pili ya ushindi huo aliyoieleza ni matokeo ya mafanikio ya serikali katika kuweka mikakati ya kubana mianya ya wakwepa kodi na vita dhidi ya ufisadi.

“Adui yetu mkubwa ni rushwa na vitendo vya ufisadi nchini.
Watanzania ni mashahidi kwani mwelekeo wa serikali umekuwa thabiti na tumeona watuhumiwa wa vitendo hivyo wakichukuliwa hatua,” alisema.

Alieleza siri ya tatu kuwa imetokana na kazi nzuri ya utendaji wa serikali kwenye utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Chama.

Katibu huyo wa Itikadi alisema, ahadi ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne, imekuwa na uhalisia mkubwa.

“Zaidi ya yote ni huduma za kiuchumi, ambazo zimeendelea kutekelezwa, ambapo Chama tunaipongeza serikali na kuikumbusha katika maeneo mengine tuliyowaahidi wananchi, ikiwemo kuendelea kutenga asimilia 10 ya mapato ya halmashauri kwa ajili ya vijana na wanawake.

“Hii itatoa nafasi kwa vijana na wanawake kupata fursa za mitaji na mikopo yenye masharti nafuu, hivyo suala hilo linapaswa kuwekewa msisitizo zaidi,” aliongeza.

Polepole alisema serikali inaendelea na mipango ya ujenzi wa viwanda, vinu vya usagaji mkoani Iringa na Mwanza pamoja na kiwanda cha mafuta ya alizeti, mambo ambayo tayari Chama kimetoa maelekezo kwa serikali.

Alibainisha kuwa, ununuzi wa ndege kwa ajili ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), umesaidia kuwawezesha wananchi kusafiri kwenye maeneo mbalimbali katika kufanya shughuli muhimu za kiuchumi.

Chama kimewataka wanachama kurudisha fadhila za ushindi huo kwa wananchi kwa kuwachagulia viongozi wenye mioyo ya kizalendo na wachapakazi waliokuwa tayari kuwasikiliza wananchi katika uchaguzi wa ndani utakaofanyika mwaka huu.

Kufuatia ushindi wa CCM kwenye uchaguzi mdogo kote nchini, baadhi ya makada wamesema ni uthibitisho kwamba, kulikuwa na usaliti mkubwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wamesema kutokana na umadhubuti wa CCM kwa wananchi wake, haikupaswa kupata matokeo iliyoyapata kwenye uchaguzi ule uliosababisha baadhi ya majimbo yasiyotarajiwa kuchukuliwa na upinzani.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe, aliliambia Uhuru kuwa, wanachama na baadhi ya viongozi walifanya kazi kubwa kuikosesha CCM ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu, hivyo baada ya kuwachambua, ushindi wa juzi ndio utamaduni halisi wa Chama.

Alisema mkoa wa Arusha, ambao uliathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukaskazini uliokuwepo mwaka 2015, kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika juzi, umerekebishika na Chama kuibuka na ushindi mkubwa.

"Tumefanya kazi kubwa. Wana-Arusha wamebaini kuwa CCM ndio mkombozi wao, wametupa ushindi  mkubwa, hizi ni salamu kwa upinzani kwenye uchaguzi ujao," alisema Mdoe.
.
Aidha, alisema siri ya ushindi kwa kiasi kikubwa ni wana-CCM mkoani Arusha, kushikamana na kukipigania Chama, badala ya kumpigania mtu, kama alivyoelekeza Mwenyekiti wa Taifa, Rais Dk. John Magufuli.

Mbunge wa Lushoto (CCM), Shaban Shekilindi, alisema ushindi huo wa CCM kwenye  uchaguzi mdogo wa ubunge Dimani, Zanzibar na udiwani kwenye kata 19, ni ishara ya nguvu ya Chama.

Alisema kutokana na uongozi thabiti wa Mwenyekiti wa CCM, Dk. Magufuli, wananchi  wamerudisha imani kwa Chama, ambapo wametambua hakuna matumaini kwenye vyama vya upinzani.

"Hali hii inatokana na uthabiti wa Chama na viongozi wake kwenye ngazi zote, kuanzia juu kwa  mwenyekiti ambaye ni Rais wetu, Dk. Magufuli," alisema.

Aidha, mbunge huyo alisema ushindi huo ni rasharasha ya uchaguzi mkuu wa 2020, kutokana na  hasira iliyonayo serikali ya CCM kwenye kutimiza ahadi zilizoko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya  2015-2020.

Kwa upande wake, Katibu wa Wazazi Mkoa wa Dodoma, Ephraim Kolimba, alisema kata zote mbili zilizoguswa katika uchaguzi huo wa mwishoni mwa wiki, zimekwenda CCM.

Alisema CCM ya sasa ni habari nyingine, ambayo vyama vya upinzani hawawezi kuielewa zaidi ya kutafuta kasoro ambazo hata hivyo hazipo.

Ephraim alisema Rais Dk. Magufuli, anastahili kupongezwa na kupewa heshima ya ushindi huo kutokana na uongozi na maamuzi yake tangu alipoingia madarakani.

"Vijana ndio sehemu kubwa ya wapigakura siku hizi, Rais alipoingia tu kateua vijana wengi kwenye nafasi mbalimbali serikalini na kwenye Chama, unadhani nini kitazuia ushindi kwa mtindo huo," alisema kwa majigambo.

Pamoja na kuwashukuru wananchi, makada hao walitoa ushauri kwa wananchi kuepuka  kuingizwa kwenye mkumbo wa msiba usiowahusu, ambao wapinzani wameujenga wakidai Serikali ya CCM imeleta maisha magumu, madai ambayo hayana ukweli.

No comments:

Post a Comment