Wednesday, 25 January 2017
KAMATI YA BUNGE YABAINI MADUDU MANISPAA YA DODOMA
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imetembelea mradi wa umwagiliaji kwa njia ya matone katika kijiji cha Gawaye, kilichoko Manispaa ya Dodoma, ambao umegharimu zaidi ya sh. milioni 800 na kuwepo na ubabaishaji mkubwa katika utekelezaji wake.
Katika ukaguzi wa mradi huo, wajumbe wa kamati hiyo walishangazwa kuona umechukua muda mrefu kukamilika na kudai kuwa, ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi minane, lakini mpaka sasa imepita miaka sita haujakamilika.
Ziara hiyo ilifanywa na kamati hiyo jana, katika Manispaa ya Dodoma, kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali, kutokana na hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuangalia thamani ya fedha kama imetumika ipasavyo.
Aidha, wajumbe hao wamebaini kuwa, kuna fedha zimetumika kununulia mbolea na miche zaidi ya sh. milioni 200, wakati wananchi ndio walitakiwa kutafuta vitu hivyo.
Akihoji kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo, Joseph Selasini (Rombo,CHADEMA), alisema ameshangazwa kuona sh. milioni 190, zimetumika kununua mbolea ya samadi kwa ajili ya kupanda miche ya zabibu, wakati mbolea hiyo inapatikana kwenye maeneo hayo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vedasto Ngombale, alisema kilichobainika kwenye mradi huo ni kuwa, umetekelezwa kinyume na mkataba unavyoainisha kutokana na wananchi kutotekeleza majukumu yaliyoanishwa kwenye mkataba.
Ngombale alisema mradi huo una wananchi 100 na kila mmoja amepatiwa hekari moja na kwamba, kama wananchi wangetekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kazi, ambayo angeifanya mkandarasi na kukamilisha, alitakiwa kulipwa sh. milioni 661, kati ya sh. milioni 803, za mradi huo.
Aliuagiza uongozi wa manispaa hiyo kushughulikia suala la umeme kwa ajili ya kisima cha kusukuma maji kwenye mradi huo, kwa kuwa mahitaji ya lita 800 za mafuta kwa ajili ya kujaza maji kwenye bwawa, wananchi hawataweza kumudu gharama hizo.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Chikota, alisema kwenye andiko la mradi huo, haukulenga kununuliwa mbolea na miche ya zabibu, bali wananchi walitakiwa kufanya kwa nguvu zao.
Kwa upande wa uongozi wa chama hicho cha ushirika, walisema matamshi ya kisiasa ndio yaliyokwamisha mradi huo kwa kuwa wanachama waliambiwa watapatiwa mikopo, jambo ambalo limewapa shida.
"Kutokana na mkandarasi kutaka kutekeleza na sisi tulikuwa hatuna mbolea, tukalazimika kuomba halmashauri tukope fedha za mradi kununulia mbolea ya samadi shilingi milioni 197 na shilingi milioni 112, tulinunua nyaya na viatilifu na tukaahidi tukipata mkopo, fedha hizo zingerejeshwa,”alisema katibu wa chama hicho.
Aidha, alisema kutokana na hali hiyo, waliomba mkopo Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) wa sh. milioni 400, lakini hawajapewa.
Akijbu hoja za wajumbe, Ofisa Kilimo wa manispaa hiyo, George Mhina, alisema walifikia maamuzi ya kukikopesha chama hicho fedha za kununulia mbolea na miche, kwa kuwa bila kufanya hivyo wangemkwamisha mkandarasi kutekeleza mradi huo.
Pia, alisema uzalishaji kwa sasa katika mradi huo unafanyika kwenye hekari 36, kati ya 100.
Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Godwin Kunambi, alisema baada ya kuona kwenye mradi huo kuna tatizo, alikaa na mkandarasi na alichokisema upande wa utekelezaji, hasa kwa wananchi, hawakuwa tayari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment