Wednesday, 25 January 2017

SILAHA KIBAO ZATEKETEZWA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameongoza shughuli ya uteketezaji wa silaha haramu 5,608, zilizopatikana kwa njia ya kusalimishwa, kukamatwa kwenye matukio ya uhalifu na ambazo hazifai kutumika.

Shughuli ya uteketezaji wa silaha hizo haramu ilifanyika jana, katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa Marekani.

Waziri Mwigulu aliwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kuwafichua wanaomiliki silaha kinyume cha taratibu na sheria, kwani wanaomiliki silaha bila kufuata taratibu ni wazi hawana nia njema na amani ya nchi.

Alisema tatizo la uzagaaji wa silaha ni la dunia nzima, hivyo ni vyema wananchi wakashirikiana na vyombo vya dola ili kuzuia silaha ndogo na nyepesi kuzagaa nchini.

"Madhara ya kuzagaa silaha kiholela yapo mengi, ikiwa ni pamoja na kuathiri maendeleo ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii. Pia kunachangia vitendo vya kihalifu, hivyo kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake,"aliagiza Mwigulu.

Waziri huyo alisema Tanzania inaungana na Umoja wa Mataifa kupiga vita uzagaaji wa silaha ndogo na nyepesi nchini.

Alisema hivi karibuni, walifanya uhakiki wa silaha, ambapo asilimia 62.16, ya wamiliki halali wa silaha za kiraia, walihakikiwa na asilimia 37.84, hawakuhakikiwa na kwamba, ifikapo Juni 30, mwaka huu, leseni zao zitakoma kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na risasi.

"Muda huo ukiisha, wale wote ambao hawajafanya uhakiki wa silaha zao, watasakwa popote walipo na watakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa kuwa watakuwa wanamiliki silaha kinyume cha sheria,"alisema Waziri Mwigulu.

Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema silaha haramu zilizoteketezwa, ambazo hazifai kutumika ni bastola 21, Shotgun 606, SMG 166, Rifle 300, Toy Pistol 21, FN Rifle 3, magobore 4,487, G3 1 na SRA 3.

Alisema wamechagua shuguli hiyo kufanyika Kigoma, kwa sababu takwimu za uhalifu zinaonyesha mikoa ya ukanda huu ndiyo kwenye silaha nyingi za haramu zinazokamatwa katika matukio mbalimbali.

"Katika silaha tulizoteketezwa jana, mkoa wa Kigoma unazo silaha 424, Kagera 100, Rukwa 189, Katavi 81, Simiyu 16, Mwanza 88, Geita 82 na Mara 100. Ukanda huu una silaha 1,060, kati ya 5,608, sawa na asilimia 18.9 ya silaha zote,"alisema.

No comments:

Post a Comment