Wednesday, 25 January 2017

MASHAHIDI WAELEZA OLE SABAYA ALIVYOJIFANYA OFISA USALAMA


NA LILIAN JOEL, ARUSHA

MASHAHIDI  wawili katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Lengai Ole Sabaya, wametoa ushahidi wao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha, mbele ya Hakimu Gwatwa Mwamkuga.
 

Shahidi wa kwanza katika ushahidi huo akiongozwa na Mwanasheria wa Serikali, Mary Lucas,  Inspekta Rogathe Steven kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha, aliieleza mahakama hiyo kuwa, Agosti 3, mwaka jana, aliagizwa kufanya upelelezi wa Ole Sabaya, kujifanya ifisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na kulala katika Hoteli ya Sky Way, iliyoko Makao Mapya,
ambapo aliacha kitambulisho chake cha TISS.

Alisema baada ya kufika katika hoteli hiyo, alijitambulisha kwa meneja wa hoteli hiyo, Philip Siake, ambaye alidai kuwa Ole Sabaya alilala  katika hoteli hiyo kwa siku tano na kutumia vinywaji, ambapo gharama yake ilikuwa sh. 309,000.

Shahidi huyo aliendelea kuileza mahakama kuwa, baada ya kushindwa kulipa fedha hizo, alicha Ipad yake na kitambulisho chake cha TISS,  kama dhamana na kuahidi kurudi kwa ajili ya kulipa kiasi hicho cha fedha.
                            
Alisema baada ya maelezo hayo, meneja huyo aliwakabidhi kimbulisho cha Ole Sabaya cha TISS na Ipad hiyo, ambapo polisi walianza kumsaka Ole Sabaya dhidi ya tuhuma hizo.

Aidha, shahidi aliendelea kuileza mahakama kuwa, baada ya kupata tetesi, alikwenda Hoteli ya Sky Way na kulipa deni lake hilo, ambapo alipatiwa stakabadhi namba 0983.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, alifanikiwa kumtia mbaroni Ole Sabaya, Agosti 26, mwaka  jana, katika eneo la CCM Mkoa wa Arusha na kumpeleka kituo kikuu cha polisi, ambapo alihojiwa na kukiri kudaiwa katika hoteli hiyo na kumweleza shahidi kuwa, amelipa kiasi hicho cha fedha na kumpa stakabadhi ya malipo namba 0983, yenye nembo ya Sky Way.

Shahidi huyo alieleza mahakama hiyo kuwa, baada ya kumhoji Ole Sabaya, aliwasiliana na ofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa Mkoa wa Arusha, ambapo walionana na ofisa mmoja aliyemtaja kwa jina la Editha Muyoke, kwa ajili ya kijiridhisha kama kweli Ole Sabaya alikuwa mtumishi wao.

Shahidi huyo alisema baada ya majibu hayo, aliwasiliana na Idara ya Utumishi na Utawala ya Usalama wa Taifa, makao makuu yaliyoko Jijini Dar es Salaam, ambapo walizungumza na mkuu wa  kitengo cha utumishi na utawala, Doroth Koshuma, ambaye alimuuliza kama wana mtumishi aitwaye Lenga T. Ole Sabaya, ambapo ofisa huyo alijibu kuwa hawana mtumishi kama huyo katika kumbukumbu zao.

Akiongozwa na wakili wa serikali, shahidi huyo aliiomba mahakama kupokea kitambulisho hicho cha TISS, Ipad na stakabadhi ya malipo ya Ole  Sabaya, ambapo hakimu alikubali kisha kuomba viendelee kuhifadhiwa polisi kwa ajili ya usalama.

Kwa upande wake, shahidi wa pili, Doroth Koshuma, akiongozwa na Mwanasheria wa Serikali, Mary aliieleza mahakama kuwa,  alipata wito wa kuitwa na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai, kwa ajili ya mahojiano katika kituo kikuu cha polisi, ambapo alifika.

Alidai alipohojiwa endapo anamfahamu mtumishi wa idara ya usalama wa taifa, ajulikanaye kwa jina la Lengai Ole Sabaya, alijibu hakuna mtumishi kama huyo.

Baada ya maelezo hayo,  Mary alimuomba Hakimu Gwatwa kumuonyesha shahidi kitambulisho cha Ole Sabaya, kama ni kitambulisho sahihi cha usalama wa taifa.

Baada ya Doroth kuonyeshwa kitambulisho, aliieleza mahakama hiyo kuwa, yeye kama mkuu wa kitengo cha utumishi katika idara ya usalama wa taifa, hawana kitambulisho kama hicho na kwamba hakitambui.

Kufuatia majibu hayo, Mary aliiomba mahakama imruhusu shahidi huyo kutoa kitambulisho halisi cha usalama wa taifa ili kiweze kupokelewa kama kielelezo mahakamani hapo.

Hakimu Gwatwa alikubali ombi hilo, ambapo Doroth alitoa kitambulisho chake.

Baada ya Doroth kukagua kitambulisho hicho cha Ole Sabaya, aliieleza mahakama hiyo kuwa, kitambulisho hicho sio mali ya usalama wa taifa na hawajawahi kuwa na mtumishi wa idara ya usalama wa taifa mwenye jina kama hilo.

Akimuhoji Doroth, wakili wa utetezi, Edna Haraka, alimuuliza ni nani anatengeneza vitambulisho? Je, kinaweza kutengenezwa na mtu yeyote?

Doroth: Sifahamu kwa kuwa sio kazi yangu.

Wakili Edna:  Vitambulisho vya ofisi yako vinatengenezewa wapi?

Dorth: Ofisini kwangu.

Wakili Edna: Kitambulisho kina kazi gani?

Doroth: Kitabulisho chochote kazi yake kubwa ni kumtambulisha mtu husika na kazi anayoifanya.

Baada ya majibu hayo, Edna aliieleza mahakama kuwa, hana swali jingine la kumuuliza  shahidi huyo.

Awali, wakati kesi  hiyo ikiendelea, Hakimu Gutwa, alimuonya Ole Sabaya kwa kufanya fujo zisizo na sababu mahakamni hapo, kwa kuandika vimemo kila mara wakati wakili wake akiwahoji mashahidi hao wawili.

“Mtuhumiwa wakili yuko hapa kukuwakilisha, wewe unafanya fujo za nini? Nimtoe wakili wako nje ubaki peke yako?"

No comments:

Post a Comment