Wednesday, 25 January 2017
MHASIBU WA MRADI WA MAJI KARATU ATUMBULIWA
MKUGENZI wa Halmashauri ya Karatu, Waziri Morris, amemuagiza mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo, kufanya ukaguzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Kambi ya Simba, kilichoko kata ya Mbulumbulu.
Morris ametoa agizo hilo kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa sh. milioni 4.7, uliodaiwa kufanywa na mhasibu wa mradi huo, Selestine Dafii.
Kufuatia ubadhirifu huo, Morris amemsimamisha kazi Daffi ili kupisha ukaguzi huo, ambao ulianza rasmi jana na kuagiza akabidhiwe taarifa hiyo ya ukaguzi ifikapo keshokutwa.
Morris, alitoa agizo hilo mwishoni mwa, wiki wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho, ambao walimuandikia barua ya kumweleza kuhusu ubadhirifu huo, kwa ajili ya kupata msaada wa ukaguzi kutoka ofisi yake.
Akizungumza na wananchi hao, Morris alisema serikali ya awamu ya tano haina mzaha na mtu au kikundi cha watu kinachofanya ubadhirifu wa mali ya umma kwa ajili ya maslahi yake binafsi.
“Mkaguzi wa ndani ataanza ukaguzi wa mradi huo wa maji kwa siku nne na Januari 27, atanikabidhi taarifa hiyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mara moja kwa wale wote waliohusika kutafuna fedha za maji,” alisema mkurugenzi huyo.
Aliongeza: “Mwenyekiti wa kamati ya maji, Joseph Petro, Katibu wake, Antonia Willium na kamati nzima ya maji, mwenyekiti wa kijiji na wengine wote watakaobainika kuhusika katika ubadhirifu wa mradi huu, tutawachukulia hatua kali za kisheria bila kujali itikadi ya chama chake cha siasa au cheo chake."
Alisema licha ya kuchukuliwa kwa hatua hiyo, atavunja kamati nzima ya maji ili wanakijiji hao waweze kuchagua kamati nyingine, ambayo inazingatia kanuni na sheria.
“Haiingii akilini mradi wa maji una akaunti benki, halafu mtu anakusanya fedha za maji na kukaa nazo nyumbani kwake kama mali yake. Lakini pia mwenyekiti wa kamati kushindwa kuitisha mkutano mkuu wa kijiji kama inavyoelekezwa kuwa kila baada ya miezi mitatu mapato na matumizi yasomwe kwenye mkutano mkuu. Kushindwa kufanya hivyo ni kosa kisheria,” alisema.
Kupitia mkutano huo, mkurugenzi huyo alisema baada ya ukaguzi huo kumalizika, utafuata ukaguzi wa mapato ya mradi wa shamba la kijiji, lenye ukubwa wa ekari 125, mradi wa trekta mbili, mradi wa kuuza moram na mradi wa ghala la kuhifadhia mazao.
“Miradi yote hii lazima ikaguliwe, hatuwezi kuwa na kijiji tajiri kama hiki, ambacho mapato yake ni kati ya shilingi milioni 80- 00, kwa mwaka, halafu ukaguzi usifanyike wakati kuna viongozi wachache wanatafuna fedha zenu kimya kimya,” alisisitiza.
Awali, wananchi hao walimlalamikia mkurugenzi huyo kuwa, kijiji chao kina mapato mengi, lakini hakuna ripoti ya mapato na matumizi inayosomwa kwa wakati katika mkutano mkuu wa viongozi wa kijiji hicho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment