Thursday, 26 January 2017
SHAKA AONGOZA MAMIA KUMZIKA ALLY NASRI MASASI MKOANI MTWARA
Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Shaka Hamdu Shaka (MNEC) jana aliwaongoza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na jumuiya zake, wanachama na wananchi mbali mbali wa Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara katika mazishi ya Katibu wa UVCCM wilaya Ludewa Mkoa wa Njombe Ali Suleiman Nasir aliyezikwa kijijini kwao Masasi.
Marehemu amefariki dunia Juzi usiku nyumbani kwao Masasi baada ya kuugua kifua na pumu kwa zaidi ya wiki mbili ambako alikwenda kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Akizungumza katika mazishi hayo Ndg: Kaimu Katibu Mkuu Shaka alimtaja marehemu Ali Suleiman Nasir kama ni kijana aliyekuwa mchapakakazi, aliyejituma kwa bidii, aliyekuwa tayari kukosolewa na kujirekebisha kila ilipobidi na hakuwa na nongwa.
“Tumempoteza mtendaji tuliyekuwa tukimtegemea mno katika kupigania maslahi ya Chama Cha Mapinduzi na jumuiya yetu mahali popote, huu ni msiba mzigo uliogusa hisia zetu na kutuachia na majonzi makubwa katika mioyo” Alisema kaimu Katibu Mkuu Shaka
Alimuelezea Marehemu Nasir kuwa katika maisha yake kama mtendaji alikuwa tayari na mwepesi kwa saa na wakati wowote kutii maelekezo toka Makao Makuu ikiwemo na kuridhia uhamisho toka mahali pamoja kwenda pengine kila ilipobidi na kusisitiza ingawaje pengo la Nasir linaweza kuzibika kwa vile ametii wito wa Mwenyezimungu lakini itachukua muda mwingi chama na jumuiya kumpata mtu wa aina yake ambaye wakati wote alijali na kuthamini, kutimiza ahadi na maelekezo kwa ujasiri na ushupavu.
“Mwenzetu ameitwa na Mwenyezimngu ametangulia mbele ya haki, siku zake katika maisha ya dunia zimekwisha na hakuna mwenye uwezo wa kuzuia uamuzi wa Mwenyezimungu, marehemu alikuwa ni mtumishi wa CCM akitumikia jumuiya ya vijana hivyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Abdulrahman Omari Kinana chama kinatoa pole kwenu nyote wafiwa na kuwaomba muwe na moyo wa subra, ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba, maombelezo na mtambue hili si lenu peke yenu sote tumeguswa na ndio maana tumekuja kuwakilisha, kuwafariji na kutoa mkono wa pole kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi na jumuiya ya Vijana” Alifahamisha Shaka*
Marehemu Ali Suleiman Nasir alizaliwa April 4 mwaka 1977 kijijini kwao Masasi Mkoani Mtwara nakupata elimu ya sekondari baadae chuo cha ufundi aliteuliwa kuwa katibu wa UVCCM wilaya Tandahimba, baadae alihamishiwa wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara, wilaya Lushoto mkoani Tanga, wilaya ya Same mkoani kilimanjaro aidha katika maisha yake ya utumishi ndani ya UVCCM aliwahi kuwa katibu wilaya ya Uyui mkoa wa Tabora kabla ya kupelekwa Newala mkoani Mtwara na hadi mauti yanamfika alikuwa katibu wa vijana wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe.
Marehemu Ali Suleiman Nasir ameacha mke na watoto watatu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment