Tuesday 28 March 2017

RAIS DKT MAGUFULI AAGIZA WIMBO WA "WAPO" WA MSANII NEY WA MITEGO UPIGWE VYOMBO VYOTE NA YEYE KUACHIWA HURU MARA MOJA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kuachiwa huru kwa Msanii wa Muziki wa Kizazi kipya, Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego (pichani) na wimbo wake kuruhusiwa kupigwa  katika vyombo vyote vya Redio na Televisheni.

Wimbo huo unaojulikana kwa jina la "Wapo"  ulikuwa umefungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema leo na yeye mwenyewe kukamatwa akiwa mkoani Morogoro alipoenda kikazi.

Akizungumza na waandishi wa habari mchana huu mjini Dodoma wakati akitoa taarifa hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harison Mwakyembe amesema uamuzi wa kuruhusiwa kupigwa kwa wimbo umetoka kwa Mheshimiwa Rais John Magufuli baada ya kupokea ujumbe wa kumtaka auruhusu  wimbo wa msanii huyo kupigwa katika vyombo vyote.

"Wimbo unaozungumziwa Rais Magufuli anaupenda sana. Na  ameomba Ney wa Mitego aachiwe huru na aendelee na kazi zake. Ila anaweza kuuboresha zaidi wimbo wake huo kwa kuongeza vitu zaidi, kama vile wakwepa kodi, watumia dawa za kulevya nk". alisema Dk. Mwakyembe.

Mwakyembe alisema kuwa Rais amefurahishwa na wimbo wa Ney wa Mitego na kumshauri kama inawezekana aendelee kuwataja watu wengine kama vile wauza unga, wakwepa kodi, wabwia unga, wezi na wengine wasio na maadili mema katika jamii.

No comments:

Post a Comment