Monday 27 March 2017
JWTZ YAANZA KUILIPA TANESCO BILIONI MOJA
JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limekubali kulipa deni inalodaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), la zaidi ya sh. bilioni tatu.
JWTZ imekubali kulipa sh. bilioni moja huku TANESCO ikiendelea kuwadai deni lililobaki la sh. bilioni mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeho, alisema vikosi vyote vya jeshi vinadaiwa, hivyo ni lazima fedha hiyo ilipwe.
Mabeho alisema watajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kuhakikisha wanalipa deni la TANESCO, ambayo ilitangaza kutoa muda wa wiki mbili kwa wadaiwa wote kulipa madeni yao.
“Kuna mitambo inatakiwa saa 24, isizimike kwa hali ya kiusalama wa taifa, hivyo inatupasa kupunguza deni huku tukiendelea kutafuta namna ya kulimaliza,"alisema.
Pia, alisema ufinyu wa bajeti unasababisha jeshi kudunduliza deni kubwa kiasi hicho, ambapo alisema sio TANESCO pekee yake wanaowadai, bali kuna wazabuni wengine wanaowadai fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Hata hivyo, aliwataka watoa huduma nchini wazingatie masuala ya ulinzi na usalama.
Aidha, Jenerali Mabeho alivitaka vikosi vya Mzinga na SUMA JKT, vijikite zaidi katika uzalishaji mali ili viwe vinajitegemea vyenyewe.
Jenerali Mabeho alivitaka vikosi hivyo vijikite zaidi katika uanzishwaji wa viwanda ili wazalishe bidhaa nyingi na waweze kuuza kwa jamii.
Alisema kwa sasa jeshi lipo imara na litaendelea kuwa imara katika kulinda ulinzi wake wa kila siku kwa taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment