Monday 27 March 2017

BUNGE LASHITUKIA MCHEZO MCHAFU KATIKA KUSAFIRISHA MCHANGA WA DHAHABU NJE


HATIMAYE Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limeingilia kati sakata la usafirishaji wa mchanga wa dhahabu na kuamua kuunda kamati itakayopitia sheria na mikataba yote ya madini na biashara hiyo.

Uamuzi huo ulifikiwa jana, jijini Dar es Salaam na Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya kutembelea bandarini na kujionea makontena yenye mchanga yakiwa yamerundikana.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa dhahabu na baadaye kubainika kuwapo kwa makontena zaidi ya 276 bandarini.

Bunge limesema ipo haja kamati hiyo kubaini anayesimamia maslahi ya nchi kimataifa katika biashara hiyo, wahusika wa biashara hiyo ni kina nani na wanafaidika vipi na thamani halisi iliyopo katika madini hayo.

Akizungumza jana, Spika Ndugai alisema ili kupata ukweli wa biashara hiyo, Bunge litaunda kamati itakayopitia sheria ya madini na mikataba ya usafirishaji mchanga wenye dhahabu ili kubaini kila kisichojulikana kwa maslahi ya taifa.

Ndugai alisema makontena zaidi ya 54,000 ya mchanga wa dhahabu, husafirishwa kila mwaka kwa zaidi ya miaka 20, hali ambayo inatia shaka kwa kuzingatia wafanyabiashara hao wanadai dhahabu iliyopo katika mchanga huo ni asilimia 0.02.

“Haiwezekani, lazima tujiulize humu katika mchanga wanadai madini yanayopatikana ni asilimia 0.02, lakini mwekezaji gani bado anakubali kutoa mchanga huu kutoka mgodini huko Buzwagi, agharamie, asafirishe hadi bandarini, asafirishe tena na kufuata taratibu zote kwenda nje ya nchi, kwa dhahabu hiyo kidogo anafaidika nini? Naamini kamati itabaini mengi zaidi,”alisema.

Alisema Bunge linatambua wananchi wana maswali mengi kuhusu biashara hiyo na idadi kubwa ya makontena yaliyopo na  yanayosafirishwa yamelishtua Bunge, hivyo kamati yake itahakikisha wanaishauri serikali ili kuchukua hatua za haraka.

Alisema alichobaini katika mchanga huo kuna dhahabu, shaba na fedha, hivyo ipo haja kujua kwa undani kuhusu wafaidika wa biashara hiyo.

Ndugai alisema kamati hiyo baada ya kupitia mikataba yote ya madini na sheria zake,  itachunguza nchi inafaidika vipi ili kupunguza mzigo wa serikali katika utegemezi wa bajeti yake.

“Timu hii tutaipa uwezo kupitia mikataba vizuri kwa kuwa rasilimali za madini ni utajiri wa nchi. Tunategemea misaada kutoka nje, ikiwa tuna rasilimali za kutosha, huenda hata tusingehitaji hiyo misaada, lazima kuchukua hatua,”alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, alisema makonteni 20 ya awali yalibainika kuwa ni shaba na 256, yaliyokutwa juzi, asilimia 90 sio mchanga bali ni mawe ya dhahabu.

Mhandisi Kakoko alisema TPA itaendelea kuhakikisha hakuna kontena lolote la mchanga wa dhahabu litakalosafirishwa nje ya nchi.

Awali, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justine Ntalikwa, alisema ipo haja ya kuundwa kamati maalumu ya wataalamu kupima sampuli ili kubaini thamani halisi ya madini iliyopo.

Profesa Ntalikwa alisema kwa sasa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), ndio wanahusika katika upimaji sampuli ya awali, ambapo katika baadhi ya makontena, walibaini asilimia kubwa ya madini yaliyopo ni shaba na dhahabu iliyopo ni asilimia 0.02.

Machi 23, mwaka huu, Rais Dk. Magufuli alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam, alikagua makontena 20, yaliyokuwa na shehena ya mchanga wa dhahabu, ambapo alipiga marufuku  usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi.

Aidha, aliagiza makontena hayo 20, kuwekwa chini ya ulinzi hadi uamuzi utakapofikiwa.

Rais Magufuli alisema wawekezaji wamekuwa wakikiuka taratibu kwa muda mrefu na nchi imekuwa ikiliwa na kukosa faida katika rasilimali zake.

Kufuatia hatua hiyo ya Rais Magufuli, juzi TPA ilikamata makontena mengine 256, yenye mchanga wa dhahabu, yakiwa yamehifadhiwa kwenye Bandari Kavu ya MOFED, tayari kusafirishwa nje ya nchi.

Makontena hayo kutoka migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Pangea, yalikuwa na lakiri za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika hatua za mwisho za taratibu za forodha.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, kuanzia jana.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilisema nafasi ya katibu mkuu wa wizara hiyo itajazwa baadaye.

No comments:

Post a Comment