Friday 24 March 2017

RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE AKUTANA NA RAIS SASSOU NGUESSO WA CONGO BRAZAVILLE



Rais Mstaafu na Kamishna wa Kamisheni ya Kupendekeza Namna Bora ya Kugharamia Fursa ya  Elimu  Duniani  ( Education Commission on Financing Global Education Opportunity) juzi tarehe 21 Machi, 2017, amekutana na Rais wa Jamhuri ya Congo alipomtembelea Ikulu yake jijini Brazaville.

Katika nafasi yake ya Mjumbe Maalum wa Kamisheni hiyo, Rais Mstaafu amemkabidhi  Rais Sassou Nguesso Ripoti ya Kamisheni hiyo yenye mapendekezo ya namna Dunia inavyoweza kukabili janga la Elimu kwa kuwekeza katika Mpango wa Kizazi cha Elimu (A Learning Generation). Mpango huo unalenga kuleta mapinduzi makubwa ya Elimu katika nchi zinazoendelea ndani ya Kizazi Kimoja  (miaka 30). Azma kuu ya Mpango huo ni kuwezesha ifikapo mwaka 2040, watoto wote kote duniani wawe wanapata elimu iliyo sawa, na kwa kiwango cha ubora unaolingana dunia nzima.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa sasa, hali ya elimu katika nchi zinazoendelea inalingana na ile ambayo nchi zinazoendelea zilikuwapo miaka 70 iliyopita. Aidha, ripoti inasisitiza kuwa, ikiwa nchi zinazoendelea zitaendelea kwa kasi ya sasa, itazichukua nchi hizo kati ya miaka 90 na 110 kufikia viwango vya sasa vya nchi zilizoendelea. Aidha, ripoti inatahadharisha kuwa takribani ajira bilioni 2 zitakufa ifikapo mwaka 2050 kutokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo asilimia 70 ya kazi hizo ziko katika nchi zinazoendelea. Hivyo, nchi zinazoendelea zinapaswa kuangalia upya aina ya elimu na stadi zinazotolewa ili kuendana na wakati ujao.
Kwa ajili hiyo, Kamisheni inapendekeza njia mpya na bora za kufanya mageuzi katika elimu ikiwemo kuongeza usimamizi, kupanua fursa, kuingiza ubinifu na teknolojia na kuongeza uwekezaji katika elimu kwa kushawishi ushiriki wa Jumuiya ya Kimataifa na Sekta Binafsi. Iwapo mapendekezo hayo yatatekelezwa, nchi zinazoendelea zinaweza kufidia pengo hilo ndani ya miaka 30 ijayo. Rais Mstaafu ameiomba Namibia kujiunga na Mpango huo.
Rais Mstaafu amempongeza Rais Nguesso kwa mafanikio makubwa ambayo Congo imeyapata katika sekta ya elimu ikiwemo hususan elimu ya awali na msingi. Kwa mujibu ya Ripoti ya Kamisheni, endapo itafanya mageuzi yanayopendekezwa, Congo ina uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kuwa na Kizazi cha Elimu ifikapo mwaka 2040.
Kwa upande wake, Rais Nguesso amepokea kwa furaha taarifa hiyo na kuelezea nia na dhamira ya nchi yake ya kujiunga na Mpango wa Kizazi cha Elimu. Ameelezea utayari wa nchi yake kufanya mageuzi katika sekta ya elimu na kushirikiana na Kamisheni katika kufaniklisha azma hiyo. Amesisitiza umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza fedha na uwekezaji katika sekta ya elimu katika nchi za kati na zinazoendelea.

Rais Mstaafu amemaliza ziara yake nchini Congo na kuelekea nchini Ghana kukutana na Rais wa Ghana Mhe. Nana Akufo-Addo.

No comments:

Post a Comment