Thursday 27 July 2017

HAKUNA KAMANDA WA POLISI ATAKAYEBAKI KITUONI



Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Inspekta Generali Simon Sirro amesema Makamanda wa Polisi wa Mikoa wataendelea kubaki katika vituo vyao vya kazi endapo watatimiza wajibu wao na kupunguza uhalifu katika mikoa yao.

IGP Sirro ameyasema hayo wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu katika mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kamaliza mazungumzo yake na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Mkoa yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu

IGP Sirro amesema Makamanda wa Polisi Mikoa wanapaswa kutimiza wajibu wao  katika kujali na kusimamia suala la Ulinzi na Usalama katika mikoa yao ili wananchi wakae kwa amani na mali zao ziwe salama.

“ Moja ya lengo la ziara yangu ni kuwakumbusha askari wa jeshi la polisi uwajibikaji na kuwajibika ni pamoja na kulinda watu na mali zao,  makamanda wa polisi mikoa nimewaambia kamanda ataendelea kukaa kwenye mkoa ule kama uhalifu utakuwa umepungua kwa kiasi kikubwa” amesema Sirro

Inspekta Sirro amesema ziara yake pia imelenga kuwakumbusha askari majukumu yao katika kuhakikisha wanawajibika kutimiza kiapo chao na kutenda haki ili wananchi waendelee kuliamini Jeshi la Polisi.

Kiongozi huyo pia ameelekeza viongozi wa jeshi la polisi wasiwanyime haki ya  dhamana watu wenye makosa ya kawaida ambayo yana  dhamana isipokuwa kwa makosa makubwa yakiwepo ya mauaji, kughushi na mengine yanayohitaji upelelezi.

Kuhusu suala la kuwepo kwa mahusiano mabaya kati ya baadhi ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Waandishi wa habari, Inspekta Sirro amefafanua kuwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa watimize wajibu wao kama watumishi wa Umma kwa kuwajali waandishi kama wanavyowajali wateja wengine kwa kufuata sheria na akawataka waandishi wa habari wafuate sheria, kanuni na taratibu pasipo kuvuka mipaka.

Akakimkaribisha Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini, katika Mkoa wa Simiyu Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka amemshukuru Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Boniventure Mshongi na Jeshi la Polisi kwa ujumla kwa namna wanavyoshirikiana katika suala la ulinzi na usalama.

Aidha, amemuomba Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini kuona uwezekano wa kusaidia kujenga majengo ya Ofisi na nyumba za makazi kwa ajili ya  Askari wa Jeshi la Polisi mkoani humo.

Inspekta Simon Sirro amewasili Mkoani Simiyu akitokea Mkoani Mara akiwa katika ziara yake ya kikazi ambapo pamoja na kuzungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu, Wakuu wa Wilaya ambao pni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya,  pia  amezungumza na viongozi na askari wa Jeshi la Polisi mkoani humo.

No comments:

Post a Comment