Thursday 6 July 2017

MAJERUHI ATOLEWA JICHO, IGP ASEMA KITAELEWEKA


MWENYEKITI  wa  Kitongoji cha  Londo, wilayani Kibiti, mkoani  Pwani, Michael Martin (28) yuko hatarini kutoona tena baada  ya kutolewa  jicho la kulia.

Akizungumza na  gazeti hili , Ofisa  Habari wa  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Neema  Mwangomo, alisema  mwenyekiti  huyo mwishoni mwa wiki iliyopita alifanyiwa upasuaji kwa saa mbili na kutolewa jicho la kulia.

Neema alisema baada ya upasuaji huo, jicho la upande wa kushoto lilionekana  mishipa yake kupata majeraha makubwa , hivyo alipewa dawa.

Alisema kwa sasa hali yake inaendelea kuimarika baada kufanyiwa upasuaji huo, ambapo jicho lake liliharibiwa na risasi.

Martin alifikishwa  Muhimbili Juni  28, mwaka huu, usiku  akitokea Hospitali ya  Misheni ya Mchukwi  iliyopo Kibiti.

Baada ya kufikishwa hospitalini hapo,  alipelekwa  Idara ya magonjwa ya dharura na ajali, ambapo timu ya madaktari  ilimfanyia uchunguzi  na kugundua jicho lake la kulia limepasuka.

Pia, Neema alisema uchunguzi huo ulibaini  jicho la kushoto mishipa ya fahamu imejeruhiwa na kumfanyia upasuaji, Juni 29, mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alijeruhiwa katika mauaji yaliyotokea Kibiti  ambayo yalimpoteza  Ofisa  Mtendaji wa Kijiji cha  Mangwi, Mwarami Shamte na Mwenyekiti wa Kijiji hicho,  Hamis  Mtima.

Wakatio huo huo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro amesema suala la Kibiti linaenda vizuri na kuonya kuwa kama kuna watu wametumwa kwa ajili ya kuvuruga amani ya Tanzania, watapata majibu yao.

"Wale ambao wametumwa vibaya, nasi tutawajibu vibaya, hivyo wasubiri majibu yao. Sisi Watanzania hatujazoea vurugu kama hizo kwa sababu ni wamoja na tunapendana," alisema Sirro.

Aliwaomba Watanzania kuwa na ulinzi wa umma, shirikishi kwa ajili ya kujilinda na uhalifu.

"Naowaomba wananchi wa Kibiti na Ikwiriri kuanzisha ulinzi shirikishi ili waweze kujilinda...kwa sababu kuna maeneo mengine ya ndani ndani pikipiki za polisi zinashindwa kufika,"alisema Sirro.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limekabidhiwa magari manne aina ya Haval Suv na Kampuni ya Great Wall ya nchini China.

Magari hayo yalikabidhiwa jana kwa Sirro katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi lililopo Oysterbay, Dar es Salaam.

IGP Sirro aliishukuru kampuni hiyo na kuahidi kuhakikisha magari hayo yanawasaidia Watanzania ili kutatua changamoto za uhalifu.

Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Great Wall, Jianguo Liu, alisema wamekabidhi magari hayo ili yaweze kusaidia jeshi hilo katika kazi zake za kulinda usalama wa Watanzania.

No comments:

Post a Comment