Thursday 6 July 2017

MANJI ASOMEWA MASHITAKA KITANDANI


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilihamia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kumsomea mashitaka ya kesi ya uhujumu uchumi, mfanyabiashara Yusuf Manji, akiwa amelazwa.
Kutokana na hatua hiyo, washitakiwa wenzake watatu ambao ni wafanyakazi wake, akiwemo Meneja Rasilimali Watu, Deogratius Kisinda, ililazimu wapelekwe hospitalini hapo ili wasomewe mashitaka pamoja na bosi wao.
Manji na wenzake walisomewa mashitaka saba yakiwemo ya kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na mihuri ya JWTZ, ambayo yanaangukia chini ya sheria za uhujumu uchumi na usalama wa taifa.
Kufuatia mashitaka hayo, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), aliwasilisha hati ya kupinga dhamana kwa watuhumiwa hao.
Mbali na Manji (41) na Kisinda (28), washitakiwa wengine ni mtunza stoo Abdallah Sangey (46), mkazi wa Jangwani na mtunza stoo msaidizi Thobias Fwele (43), mkazi wa Chanika.
Mahakama hiyo ilianza safari ya kuhamia hospitalini hapo saa 8.30 mchana, ambapo ilipofika  saa 9.10 alasiri, maofisa wa mahakama, wakiwemo mawakili wa serikali na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi na mawakili wa washitakiwa hao, walifika hospitalini hapo.
Msafara huo, ulielekea hadi katika ghorofa ya pili ya jengo la taasisi hiyo, kwenye wodi namba moja, ambapo upande wa jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, akishirikiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga na Tulumanywa Majigo, uliwasomea washitakiwa hao mashitaka hayo.
Manji akiwa kitandani huku ametundikiwa dripu, akiwa amevalia nguo za wagonjwa na wenzake wakiwa pembezoni mwa kitanda chake, walisomewa mashitaka ya kujipatia bidhaa isivyo halali, kukutwa na mihuri ya serikali isiyo halali na kukutwa na mali inayodhaniwa imepatikana isivyo halali.
Katika mashitaka hayo, Manji na wenzake wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe ‘A’, wilayani Temeke, Dar es Salaam, kwa pamoja walikutwa na ofisa wa polisi wakiwa na mabando 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ, zenye thamani ya sh. milioni 192.5 ambavyo vilipatikana isivyo halali.
Pia, washitakiwa hao wanadaiwa Julai Mosi, mwaka huu, katika maeneo hayo, walikutwa na ofisa wa polisi, wakiwa na mabando manane ya vitambaa hivyo, vyenye thamani ya sh. milioni 44.
Shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na mhuri wa JWTZ wenye maandishi “MKUU WA KIKOSI 121 KIKOSI CHA JESHI JWTZ”,  bila ya kuwa na uhalali kitengo ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Washitakiwa hao wanadaiwa siku hiyo, walikutwa na mhuri wa JWTZ wenye maneno “KAMANDA KIKOSI 834 KJ MAKUTUPORA DODOMA,” bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wan chi.
Manji na wenzake, pia wanadaiwa siku hiyo walikutwa na mhuri mwingine wenye maneno COMANDING OFFICER 835 KJ, MGAMBO P.O BOX 224 KOROGWE.
Washitakiwa hao wanadaiwa Julai Mosi, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na vibao vya namba za usajili za magari vyenye namba SU 383 na SM 8573 ambavyo vilipatikana isivyo halali.
Mapema wakati mashitaka yanaanza kusomwa, Manji alikuwa amekaa kitandani, lakini baadaye alilala na kujifunika blanketi na kuendelea kusikiliza mashitaka yake.
Baada ya washitakiwa hao wanaotetewa na mawakili Hudson Ndusyepo, Emmanuel Safari na Seni Malimi, kusomewa mashitaka, hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa sababu wameshitakiwa chini ya sheria za uhujumu uchumi na usalama wa taifa.
DPP AWASILISHA HATI YA KUPINGA DHAMANA
Upande wa jamhuri uliwasilisha hati ya kupinga dhamana kutoka kwa DPP, akiomba washitakiwa wasiruhusiwe kupewa dhamana.
Mawakili hao wa serikali, walidai DPP anaona washitakiwa wakiachiwa kwa dhamana watahatarisha usalama na maslahi ya nchi na kwa mujibu wa shitaka la kwanza na la pili, Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kushughulikia suala la dhamana.

MAWAKILI WA MANJI WAPINGA HATI YA DPP
Kwa upande wa mawakili wa washitakiwa hao, walipinga wateja wao kuzuiwa wasipewe dhamana kwa vile mashitaka namna yalivyo, yanaiondolea mahakama hiyo kufikiria suala la dhamana lakini kwa nia mbaya iliyoonyeshwa na upande wa jamhuri.
“Upande wa jamhuri umewasilisha hati ya DPP kupinga dhamana, kitendo ambacho tunaona kama ni matumizi mabaya ya madaraka na hakitendi haki kwa washitakiwa,” walidai mawakili hao.
Ndusyepo alidai jana Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, katika kesi namba 115 ya mwaka huu, ilikuwa isikilize maombi ya uhalali wa polisi kuendelea kuwashikilia Manji na wenzake.
“Lakini kwa kuonyesha nia ovu upande wa jamhuri umeandaa mashitaka ambayo hayaakisi mazingira ya kesi hiyo,” alidai.
HAKIMU: SINA MAMLAKA
Baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili, akiwa hospitalini hapo, hakimu Shaidi alitoa uamuzi na kusema ameona masuala hayo yanapaswa kuongelewa katika mahakama yenye mamlaka.
Hakimu Shaidi alisema kwa kuwa DPP hajaipa Mahakama ya Kisutu, mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, hivyo hawezi kuzungumza lolote. Shauri hilo liliahirishwa hadi Julai 17, mwaka huu kwa kutajwa kwa kuwa upelelezi haujakamilika.
Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo saa 10.38 jioni, washitakiwa Kisinda, Sangey na Fwele waliondolewa hospitalini hapo kwa kutumia gari la polisi aina ya Land Cruiser, lenye namba T 968 DHS na kupelekwa mahabusu kwenye gereza la Keko, huku Manji akiwa hospitalini hapo atakuwa chini ya ulinzi wa Magereza.

YALIYOJIRI KABLA NA BAADA YA KUSOMEWA MASHITAKA
Mapema, jana mawakili wa washitakiwa hao walifika katika Mahakama ya Kisutu, wakifuatilia kesi dhidi ya wateja wao.
Ilipofika saa 8.30 mchana, mawakili wa pande zote wa serikali na utetezi, waliingia katika chumba cha hakimu Shaidi, ambapo baada ya muda mfupi walitoka na kueleza kuwa mahakama inahamia Muhimbili kuwasomea mashitaka yao.
Kutokana na hilo, watu waliokuwepo mahakamani hapo wakifuatilia kesi hiyo, wakiwemo wafanyakazi wengine wa Manji, waliingia kwenye magari na kwenda Muhimbili, ambapo mawakili wake waliamua kukodi teksi tatu.
Katika jengo hilo, kulikuwa na ulinzi mkali wa askari waliovalia kiraia na wale wenye sare za kazi, ambapo waandishi wa habari waliruhusiwa kutuma wawakilishi wawili, huku ndugu na jamaa wakizuiliwa kwa kuwa wagonjwa hawahitaji msongamano.

No comments:

Post a Comment