Thursday 20 July 2017

RAIS MAGUFULI ATANGAZA KIAMA KWA WAUZA MAFUTA





RAIS Dk. John Magufuli ametoa siku 14, kwa wamiliki wote wa vituo vya mafuta, kufunga na kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti.

Alitoa agizo hilo jana, wakati akizungumza na wananchi wa Biharamulo mkoani Kagera, kabla ya kufungua barabara ya lami ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga.

Rais Dk. Magufuli aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo na kusisitiza kuwa, wamiliki watakaokiuka agizo hilo, vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

“Kwa hili, natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam, hakikisha unayo hiyo mashine ndani ya siku 14,” alisisitiza Rais Dk. Magufuli.

Pia, aliwataka wafugaji waliovamia Hifadhi ya Burigi mkoani Kagera, kuondoa mifugo yao mara moja na alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salum Kijuu, kuendelea na operesheni ya kuondoa mifugo iliyovamia hifadhi hiyo na maeneo mengine yasiyoruhusiwa.

Aliwaagiza wafugaji kote nchini, kuchunga mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kulisha mifugo na alionya kuwa, vitendo vya wafugaji kuingiza mifugo katika hifadhi na mashamba ya wakulima, havikubaliki.

“Mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya, simamieni hilo. Ninajua bado kuna ng’ombe mle hifadhini, simamieni kwa kuzingatia sheria za hifadhi.

“Wafugaji wajifunze namna ya kufuga. Kama unaona una ng’ombe wengi na huwezi kuwatunza uza. Hata mimi nimeuza ng’ombe wangu, niliona wamekuwa wengi siwezi kuwatunza, viwanda vipo,”alibainisha Rais Dk. Magufuli.

Kuhusu kero ya uhaba wa maji inayowakabili wananchi wa Biharamulo, Rais Magufuli alieleza kusikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji katika mji huo.

Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Bukoba (BUWASA), Alen Mwita, kuhakikisha mashine zilizonunuliwa zinafungwa na kuanza kutoa maji ifikapo Julai 30, 2017.

Baada ya kuzungumza na wananchi wa Biharamulo, katika mkutano wa hadhara, uliofanyika katika kituo cha mabasi, Rais Magufuli alifungua barabara ya Kagoma – Biharamulo – Lusahunga, ambayo inaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Kigoma, Shinyanga na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda.

Barabara hiyo ina urefu wa kilomita 154 na imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 190.4, zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.

Mapema jana, Rais Dk. Magufuli alitembelea seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Katoke, alikosoma elimu ya sekondari, ambako aliendesha uchangiaji uliofanikisha kupatikana mifuko 1,000 ya saruji na mabati 150, kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa majengo ya seminari hiyo.

Pia, alitoa sh. milioni moja kwa ajili ya kutengeneza dirisha la bweni alilolivunja wakati akiwa kidato cha pili na madirisha mengine yanayohitaji matengenezo.

Akiwa njiani kwenda Ngara, Rais Magufuli, ambaye alisimamishwa na wananchi wa Nyakahura, aliwahakikishia kuwa serikali itaifanyia matengenezo barabara ya Nyakahura – Rusumo – Ngara na aliahidi kumtuma Waziri wa Maji na Umwagiliaji, kwenda kuangalia namna ya kutatua tatizo la maji na alichangia sh. milioni 10, katika ujenzi wa majengo ya shule.

Leo, Rais Magufuli ataendelea na ziara yake mkoani Kagera, ambako atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika mchana.

No comments:

Post a Comment