Sunday, 24 September 2017

ELIMU BURE SEKONDARI ZANZIBAR KUANZA MWAKANI



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametangaza kuanzia kuwa, Julai mosi mwakani, Serikali ya Zanzibar itatoa elimu bure kwa shule zote za sekondari za serikali.

Dk. Shein aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, katika kilele cha sherehe za tamasha la elimu bila malipo, zilizofanyika kwenye uwanja wa Gombani, Wilaya ya Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema kuanzia bajeti ya mwaka ujao wa fedha, shule zote za sekondari zitatoa elimu bila ya malipo, ili kutimiza azma ya Rais wa Kwanza wa Visiwa hivyo, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kutoa elimu bure.

Aliongeza kuwa, Zanzibar ina uwezo wa kugharamia sera hiyo ya elimu.

“Hatuna sababu ya kushindwa kutoa elimu bure, iwe ya maandalizi, msingi au sekondari na naziagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango, wawe makini katika kuipanga bajeti ya Wizara ya Elimu ya mwaka 2018/2019,” alisema Dk. Shein.

Kuhusu elimu ya juu, Dk. Shein alisema utaratibu wa kutoa mikopo utaendelea hadi pale zitakapofanywa taratibu nyingine.

Alieleza kuwa ni dhahiri kwamba, katika kipindi cha miaka 53 ya Mapinduzi, mafanikio makubwa yamepatikana katika kuyatekeleza malengo ya Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964, ambapo katika kipindi chote, serikali imeendelea kutoa elimu bila malipo, ingawa siyo katika miaka 15 ya mwanzo baada ya Mapinduzi.

Alisema hatua hiyo inatokana na sababu za kiuchumi na ongezeko la idadi ya watu, ambapo serikali ililazimika kuwaomba wananchi wachangie elimu kwa utaratibu maalumu, ulioandaliwa kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Alieleza kuwa, kuanzia Julai, mwaka juzi, uchangiaji wa elimu katika shule za awali na msingi, uliondolewa na serikali inatoa elimu ya msingi bila malipo kama ilivyoamriwa baada ya Mapinduzi.

Dk. Shein alielezea mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 53 ya Mapinduzi katika sekta ya elimu kuwa ni kujenga vyuo vikuu, ufundi, vyuo vya amali na chuo cha elimu mbadala kwa Unguja na Pemba, ambavyo ni vingi kuliko wakati wa ukoloni.

Alieleza kuwa, fursa za elimu kwa fani mbalimbali zimeongezeka, ambapo zinafundishwa Zanzibar huku wataalamu 1,800 wa fani mbalimbali wakihitimu.

Rais huyo wa Zanzibar alisema, serikali inatambua changamoto za walimu na itaendelea kuchukua hatua, kwani kipaumbele ni kuimarisha ubora wa elimu, miundombinu ya elimu kwa kujenga shule mpya, kukamilisha ujenzi wa shule na kusambaza vitabu na samani.

Aliuhimiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kuongeza jitihada na nguvu maalumu katika kufanikisha michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema uongozi wa wizara yake utaendelea kuimarisha sekta ya elimu.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, mawaziri na viongozi wengine wa serikali pamoja na wananchi.

No comments:

Post a Comment